BM BARBERSHOP KINONDONI

Friday, September 7, 2012

PATA WASIFU WA LULU MATHIAS MAGONGO “AUNT LULU” MWANATANGA

ASILI yake ni huko mkoani Tanga yalikozaliwa mapenzi!!! Kabila lake ni Mbondei au wanabonde wa pale viwanja vya Muheza. Jina lake lilianza kukua kupitia ulimwengu wa habari. Alikuwa mtangazaji baadaye akapita kwenye Shindano la Kimwana Manywele Twanga Pepeta 2006/07 na sasa anafurukuta zaidi katika ulimwengu wa filamu za Kibongo.  Huyu si mwingine bali ni Mwanadada Lulu Mathias Semagongo ‘Aunt Lulu’. Aliyezaliwa mwaka 1987 jijini Dar es Salaam.

Lulu Mathais  alianza shule ya msingi mwaka 1993 Shule ya Msingi ya Kumbukumbu iliyopo Wilaya ya Kinondoni Mkoani Dar es Salaam na kuhitimu elimu ya kuondoa ujinga kichwani mwaka 1999.  Mwaka 2000, Aunt Lulu alijiunga na Shule ya Sekondari Kisutu wasichana na kumaliza hapo mwaka 2004 kiwango cha elimu ya Sekondari (O-Level).

UTANGAZAJI
Kipaji kwa Aunt Lulu kilijionesha waziwazi tangu akiwa shule ya msingi. Mwaka 1998 hadi 2003 alikuwa akitangaza kipindi cha watoto cha Redio One na ITV kilichojulikana kwa jina la Watoto Show.

Mwaka 2004 hadi 2006, mkali huyo aliyeonyesha cheche katika kutumia kipaza sauti, alihamia Redio Magic FM ya jijini Dar. Akiwa Redio Magic Lulu alitangaza kipindi kilichofahamika kama Ulingo wa Watoto, wakati huohuo akiwa kwenye mtandao wa vijana uliokuwa ukijishughulisha na matatizo yanayowakabili watoto chini ya mfuko wa shirika linalojishughulisha na haki za watoto duniani la UNICEF.
 
KIMWANA WA TWANGA PEPETA.
Mwenye kipaji siku zote siyo mwenzako, mwaka 2006, Aunt Lulu alijitosa kwenye Shindano la Kimwana wa Twanga Pepeta (Kimwana Manywele Twanga Pepeta) lililokuwa likitafuta mnenguaji bora. Aunt Lulu alijishindia taji hilo na kunyakuwa zawadi ya gari. Jina la Lulu lilianza kukua zaidi baada ya kupitia Kimwana Manywele.  Aunt Lulu alitumia nafasi hiyo kusoma kozi fupi za kompyuta kabla ya kujiunga na kampuni ya Bench Mark Production mwaka 2007.

LULU NDANI YA BENCH MARK PRODUCTION
Lulu Mathias alijiunga na Kampuni ya Bench Mark Production kama Assistant Producer na pia alikuwa host wa kipindi cha Wimbo kilichorushwa kupitia ITV,”

LULU ARUDI DARASANI
Mwaka 2008, mtangazaji Lulu alirudi darasani na kusoma kozi ya Kingereza pale British Council na kufanikiwa kuhitimu masomo hayo katika ngazi ya cheti (advanced certificate).


MWANZO WA SKENDO
Maisha ya Aunt Lulu yaliendelea kushamiri katika kazi ingawa pia aligubikwa na skendo za hapa na pale kama ulevi wa kupindukia na mengine mengi yanayofanana na hayo. Mara kakutwa amelewa klabu, mara kanaswa sehemu na mwanaume na mengineyo.

UTANGAZAJI TENA
Mwaka 2009 hadi 2011, Aunt Lulu mwenye matukio kibao mjini, alipata nafasi ya kutangaza katika Televisheni ya C2C. Aliposimama kutangaza mwaka 2011, aliamua kuingia kwenye darasa lihusulo taaluma yake ya utangazaji. Akajiunga na Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC) kilichopo Makumbusho jijini Dar es Salaam kupata cheti.

MUIGIZAJI WA FILAMU
Mwaka huu 2012, Aunt Lulu amekuja kivingine baada ya kugundua ana kipaji cha uigizaji. Kwa kukubali ushauri aliopewa na mpenzi wake (Bond Bin Salim), akaanza kuigiza chini ya Kampuni ya Richard Dyle Bezuidenhout (Richard wa BBA).

LULU ANAFANYA NINI KWA SASA?
Mpaka leo, Aunt Lulu bado anafanya shughuli za U-MC katika sherehe mbalimbali huku akiwa ameelekeza nguvu zake katika ulimwengu wa filamu za Kibongo.

MAFANIKIO YA LULU
Mwenyewe anasema mafanikio makubwa zaidi ni kujulikana, ukiacha kiwanja chake alichonunua ambacho bado hajaanza ujenzi.

HUYU NDIYE LULU MATHIAS MAGONGO “AUNT LULU”
















1 comment:

  1. na kweli ni lulu kweli mdau wangu karibu knjaro

    ReplyDelete