Mwandishi Wetu,
Hanang'
SIASA za makundi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),
zimetajwa kuwa chanzo cha kuangushwa kwa Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye
katika nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), kupitia Wilaya ya
Hanang’ Mkoa wa Manyara.
Sumaye ambaye anatajwa kuwa ana nia ya kugombea urais katika
Uchaguzi Mkuu ujao, alishindwa na Dk Mary Nagu ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi
ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji). Katika uchaguzi huo,
Sumaye alipata kura 481 dhidi ya Nagu, aliyepata kura 648.
Mbali na Sumaye, wajumbe wengine waliokuwa wakimuunga mkono
akiwamo Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Goma Gwantu, pia walishindwa katika
uchaguzi huo. Dalili za kushindwa kwa Sumaye, ambaye alikuwa akiungwa mkono na
wajumbe wa kamati ya siasa ya CCM wa wilaya hiyo, zilianza kuonekana wiki moja
kabla ya uchaguzi huo.
Kambi ya Dk Nagu ambayo inatajwa kwamba inaungwa mkono na
kambi ya Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, ilionekana kuwa na “ushawishi”
mkubwa katika vikao vya kamati ya siasa ya mkoa na kwenye Kamati Kuu ya CCM. Hali
hiyo, ilitokana na ukweli kuwa Dk Nagu kama taratibu ambazo zilihitajika,
hakupewa baraka na kamati ya siasa ya wilaya hiyo, kugombea kwa kile ambacho
kilielezwa kukwepa mpasuko wa CCM Hanang' na pia kumpa heshima Sumaye.
Hata hivyo, habari zimeeleza kuwa tofauti na msimamo wa
Kamati ya Siasa ya wilaya hiyo, Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Manyara, ilionekana
kumuunga mkono Dk Nagu hasa kutokana na ukweli kuwa karibu nusu ya wajumbe wa
kamati hiyo walikuwa wagombea.
Kikao cha kamati ya siasa ya mkoa, licha ya kurejesha jina la
Dk Nagu pia, kilipendekeza kuondolewa majina ya wagombea kadhaa katika wilaya
ya Hanang' likiwamo jina la Mwenyekiti wa wilaya hiyo, Goma Gwaltu ambaye
alikuwa kambi ya Sumaye. Taarifa za kupendekezwa kuondolewa majina ya
wanaomuunga mkono Sumaye, zilitolewa na baadhi ya wajumbe wa Wilaya ya Hanang’,
lakini hata hivyo, Katibu wa CCM Mkoa wa Manyara, Ndeng'aso Ndekubali
alizikanusha.
“Kamati ya siasa ya mkoa ni kikao cha siri na nadhani ni
mapema mno kulalamikia suala hilo, ni vyema wakasubiri uamuzi wa juu, ” alisema
Ndekubali. Hata baada ya kurejeshwa majina na Nec, ilibainika kuwa wagombea
ambao Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo, iliwapa alama za chini, wamerejeshwa
katika mchakato wa uchaguzi.
Dalili za kuanguka Sumaye, pia zilijionyesha siku ya kupiga
kura, ukumbini na nje ya ukumbi kutokana na wajumbe waliokuwa wanamuunga
mkono Dk Nagu kuwa na uhakika mkubwa wa ushindi. Wakati wa kujieleza ili aombe
kura, Sumaye ambaye alionekana kama tayari amebaini nguvu ya Dk Nagu, alieleza
kushangazwa na uamuzi wa Dk Nagu kugombea nafasi hiyo, hali ya kuwa ni
waziri.
Sumaye, pia alikemea kile alichodai kuwa ni rushwa kwenye
chaguzi za CCM na kuahidi kama akichaguliwa, angeshirikiana na viongozi
wenzake kuhakikisha anawachukulia hatua kali watoa rushwa. Awali Dk Nagu
katika maelezo yake, alitumia fursa ya kuomba kura kukanusha kuwa anatumiwa na
kundi la Lowassa ili kumkwamisha Sumaye.
Dk. Nagu alifafanua kuwa yeye kama Mbunge wa Hanang’ na
Waziri, kamwe hawezi kutumiwa na kundi fulani kwa masilahi ya makundi kwani
hata yeye ana sifa za kuchaguliwa. Wakati wa maswali, Dk. Nagu hakuulizwa
wakati Sumaye aliulizwa maswali matatu ambayo aliyajibu kwa ufasaha, lakini
hakuchaguliwa.
Mwenyekiti wa CCM aliyeshindwa, Goma Gwaltu, alieleza kupinga
mambo kadhaa yaliyokiukwa katika uchaguzi, lakini hata hivyo, alisisitiza
kujiandaa kutoa tamko rasmi. “Nitazungumza siku si nyingi kuelezea uchaguzi
huu,” alisema Gwaltu. Naye Sumaye kwa upande wake, alisema anakusudia
kuzungumzia yaliyojiri katika uchaguzi huo hivi karibuni.
“Naomba uwe na subira, nitawaita wanahabari na tutazungumza.
Leo (jana) nimepigiwa simu na waandishi kama 50, wote nimewaambia kuwa
nitazungumza siku chache zijazo,” alisema Sumaye. Mbunge wa Viti Maalumu
Chadema, Rose Kamili ambaye kwa muda mrefu alikuwa diwani kwa tiketi ya CCM
kabla ya kuhamia Chadema, alieleza kuwa Sumaye aliangushwa kwa nguvu ya fedha.
Alisema kuwa kitendo cha Sumaye kutajwa kuwa anataka kuwania
urais katika uchaguzi ujao ndiyo sababu ya kutoswa katika uchaguzi huo ili kupunguza
ushindani. Kwa upande wake Gwaltu alisema kilichomwangusha Sumaye ni
makundi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Alisema kuwa makundi hayo ambayo yameanza kujipanga kwa ajili
ya kushinda katika kinyang’anyiro cha kuwania urais, yalifanya kila njia
kuhakikisha kuwa Sumaye hapenyi katika hatua hiyo, lengo likiwa ni kufanya
upinzani kuwa mdogo 2015. Kada mkongwe wa chama hicho ambaye pia ni Diwani wa
Kata ya Basotu, Samwel Kawoga alisema kuwa makundi hayo yalianza kuonekana wazi
siku chache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo.
Alisema kuwa makundi hayo ni pamoja na yale yanayoongozwa na
makada wa chama hicho wanaoutaka urais na mengine ni yale yanayoibuka kila
unapofanyika uchaguzi ndani ya chama hicho.
Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment