BM BARBERSHOP KINONDONI

Tuesday, November 13, 2012

WASIFU WA MAREHEMU MARIAM KHAMIS KWAHISANI YA SALUTI 5



WENGI wamezipokea kwa mshituko taarifa za kifo cha mwanamipasho Maariam Khamis “Paka Mapepe” (26), aliyefariki wakati wa kujifungua kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam leo alfajiri. Hii ni kwasababu, Paka Mapepe alikuwa kivutio kikubwa na kipenzi cha wengi, hasa kutokana na uimbaji wake uliojaa hisia nzito, kwenye tungo zote alizoimba.
Hadi mauti yanamfika, Paka Mapepe alikuwa ni msanii wa kundi lamipasho la TOT Taarab lililop0 chini ya chama tawala CCM. Alijiunga na TOT Taarab mwanzoni mwa mwaka jana, akitokea katika kundi la Five Stars Modern Taarab aliloingia mwishoni mwa mwaka 2009.
Paka Mapepe aliipa kisogo Five Stars na kuhamishia virago TOT  Taarab muda mfupi kabla ya ajali ya kundi hilo iliyoua wasanii 13, Machi, mwaka jana, Mikumi Morogoro. Akiwa Five Stars, alitikisa vilivyo kwa vibao viwili; ‘Ndo Basi Tena’ pamoja na ‘Uzushi Wenu Haunitii Doa’ .
www.saluti5.com iliwahi kuongea naye wakati wa uhai wake, kuhusiana na msiba wa wasanii wenzake wa Five Stars, ambako alisema kuwa, ni msiba uliogonga kwa kishindo moyoni mwake.

Mara kwa mara alikuwa akiweweseka na kuwaota baadhi ya marehemu wasanii wa Five Stars, kila alipokumbuka namna alivyoishi nao vema,hata pale alipobadili upepo na kuingia TOT  Taarab.

Historia yake kimuziki ilianzia mwaka 2003, mara baada ya kuhitimuelimu ya sekondari, ambako alipenda sana Taarab, kwa kuvutiwa namagwiji wa mipasho.
Baadhi ya magwiji hao waliokuwa wakimvutia Paka Mapepe ni pamoja na Zuhura Shaaban, ‘Malkia wa Mipasho’ Khadija Kopa na marehemu Nasma Khamis ‘Kidogo’. Wakati huo, kutokana na shetani muziki kumpanda kindakindaki kichwani kwake, alikuwa akiandika kwenye daftari mashairi ya baadhi ya vibao vyao na kuviimba mara kwa mara kila alipotulia.

Kati ya watu waliogundua mapema kipaji chake cha uimbaji na kukifanyia kazi, ni baba yake mdogo aitwaye Kessy Abdallah ambaye alimuunganisha kwenye kundi la Segere No2, jijini Dar es Salaam, ili kujifua zaidi.
Akiwa Segere, ambalo baadhi ya vinara wake alikuwa Mussa Msuba,
alirekodi kibao kiimoja kinachokwenda kwa jina la ‘Mpenzi Wana kabla albamu yake haijatoka, kundi lilisambaratika.
Mwaka 2007, Mussa Mipango, kati ya wacharazaji mahiri wa gitaa zito, Besi hapa nchini, aliyeko TOT Taarab hivi sasa, alimuunganishia katika kundi la Zanzibar Stars Modern Taarab ‘Watoto wa Pwani’.
Hakukaa sana Zanzibar Stars kwani mwaka huohuo, 2007 alitimkia East African Melody Taarab alikorekodi kibao ‘Paka Mapepe’ kilichotokea kutikisa vilivyo kiasi cha mashabiki kuamua jina hilo liwe la kwake moja kwa moja.
Mwaka 2008, Paka Mapepe alirejea Zanzibar Stars alikofikia kurekodi kibao ‘Huliwezi Bifu’, kabla ya vingine kama vile; ‘Raha ya Mapenzi’, ‘Narindima Mie’ na ‘Shoga Habari Ndo Hiyo’ .
Kila wakati, Paka Mapepe alikuwa akikiri kuwa, ujuzi wake kiuimbajiulikuwa unatokana na kutilia mkazo madrasa ya Shadria, jijini Dar esSalaam, alikosoma na kufikisha juzuu mbili.
Mara tu baada ya kuingia TOT  Taarab, Paka Mapepe alipewa kurekodi kibao ‘Sidhuriki na Lawama’, ambacho hata mwenyewe alikuwa akithibitisha kuwa, kilitokea kumsogeza na mashabiki wengi wa mipasho.
Kati ya watu ambao mara kwa mara alipenda kuwataja kuwa ni miongoni mwa waliochangia kumfikisha alipoishia, ni pamoja na baba na mama yake waliompa moyo tangu alipoanza kujiingiza katika muziki.
Aidha, alikuwa pia akipenda kuvishukuru vikundi vyote vya muziki wa taarab alivyopitia ikiwamo Melody na mashabiki pamoja na wapenzi wote kwa ujumla.
Aliolewa na mcharazaji mahiri wa gitaa la Besi, Haji Kijungu, aliyejaliwa kuzaa naye mtoto mmoja aitwaye Taliq (6).
Paka Mapepe alizaliwa mwaka 1986, jijini Dar es Salaam na kupata elimu ya msingi katika shule ya Amana, Ilala kuanzia mwaka 1994 hadi 2000 na sekondari ya Jamhuri kati ya mwaka 2001 na 2003.
MUNGU AMLAZE MAHALA PEMA PEPONI

No comments:

Post a Comment