BM BARBERSHOP KINONDONI

Friday, August 24, 2012

SIMBA YAWAWEKEA PINGAMIZI MGONGOLWA, NCHUNGA NA MADEGA KWENYE UAMUZI WA UTATA WA MAAMUZI YA USAJILI WA TWITE NA YONDANI


IMANI MADEGA MWANASHERIA
ALEX MGONGOLWA MWANASHERIA
LYOID NCHUNGA MWANASHERIA
MABINGWA wa Ligi Kuu Bara, Simba ya jijini Dar es Salaam imewasilisha barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wakimpinga Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho hilo, Wakili Alex Mgongolwa, pamoja na wajumbe wake wawili kwa madai ya kutokuwa na imani nao.

Wajumbe waliopingwa sambamba na Mgongolwa ni waliowahi kuwa wenyeviti wa klabu ya Yanga, mawakili Lloyd Nchunga na Iman Mahugila Madega. Pingamizi hilo la Simba, linatokana na kutokuwa na imani na viongozi hao katika kuamua suala la usajili wa wachezaji waliozua utata, Kelvin Yondani na Mbuyu Twite, ambao awali Simba inadai iliwasajili kabla ya Yanga kuingilia kati na kuwanyakua.

Kamati hiyo ilikuwa ikutane jana na leo kwa ajili ya kupitia usajili wa klabu za Ligi Kuu Bara na Ligi Daraja la Kwanza, lakini kutokana na kusogezwa mbele kwa ligi hiyo, wanatarajiwa kukutana katika tarehe itakayopangwa baadaye. Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga ‘Mr. Liverpool’ alisema wamewasilisha barua hiyo ili kuomba kushughulikiwa kwa ombi lao kwa hofu ya kutotendewa haki.

Kamawaga alisema kuwa Mgongolwa pamoja na kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo, pia amepata kuwa mjumbe wa kamati za Yanga, huku Madega na Nchunga nao wakiwa ni wanachama waadilifu na waaminifu wa klabu hiyo, hivyo ni rahisi kuipendelea. Aliongeza kuwa kutokana na wajumbe hao wa kamati kuwa na damu ya Yanga, wanaamini hawatatoa maamuzi sahihi kuhusiana na suala linalohusu utata wa usajili wa wachezaji hao, hivyo TFF haina budi kutumia busara kuwaondoa.

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage, alitangaza kujiuzulu ujumbe wa kamati hiyo, kabla ya Rais wa TFF, Leodegar Tenga, kukutana naye na kumweka sawa, hivyo kubadili msimamo wake.

Kamati ya katiba ,sheria na hadhi ya wachezaji inaongozwa na mwenyekiti Alex Mgongolwa, makamu mwenyekiti Husein Mwamba na wajumbe Imani Madega,Venance Mwamoto,Omari Gumbo ,Ismail Aden Rage na Lloyd Nchunga. Suala la kujiuliza ni je vipi kuhusu Aden Rage na Omari Gumbo ambao nao ni wanachama wa Simba?Kwasasa Rage ndio Mwenyekiti na Omari Gumbo kabla ya Uongozi wa sasa alikuwa makamu mwenyekiti wa klabu hiyo.



1 comment:

  1. Kumbe ndio maana Simba wanapokwa haki zao; kesi ya mwana kondoo kumpelekea chui. Halafu wanachekelea Simba kupokwa wachezaji wao kumbe ni umafia mtupu.

    ReplyDelete