BM BARBERSHOP KINONDONI

Wednesday, September 26, 2012

JK AMTEUA BI.HAWA MMANGA KUWA MWENYEKITI MPYA WA BODI YA TANROADS




Na Aron Msigwa – MAELEZO.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete amemteua Bi.Hawa Magongo Mmanga kuwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kwa kipindi cha miaka mitatu.

Taarifa iliyotolewa leo jijini Dar es salaam na Wizara ya Ujenzi na kusainiwa na Katibu mkuu wa wizara hiyo Balozi Herbert Mrango imeeleza kuwa Bi. Hawa Mmanga anachukua nafasi iliyoachwa wazi na  Bw. Abel Mwaisumo ambaye amemaliza kipindi chake cha utumishi.

Taarifa hiyo  imeeleza kuwa  uteuzi huo ni kwa mujibu wa kifungu na 9 (2) (a) cha Sheria ya Barabara Namba 13 ya mwaka 2007 na umeanza toka tarehe 19 Septemba 2012.

Aidha imefafanua kuwa kabla ya uteuzi huo Bi. Hawa Mmanga amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi zikiwemo za Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni kwa watumishi wa Umma (PSPF) na Mkurugenzi wa Pensheni wa Wizara ya Fedha.

Nafasi nyingine  aliyoshika ni ya ujumbe katika  Bodi ya Mifuko ya Serikali za Mitaa (LAPF)  na Bodi ya Taifa ya Hifadhi za Jamii.

No comments:

Post a Comment