Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imechukua uamuzi magumu, baada ya kumwengua Mwenyekiki wa Chama cha soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Amin Mohamed Bakhresa katika kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu wa chama hicho.
Bakhressa ambaye alikuwa madarakani zaidi ya miaka 10 hatima yake ya kuendelea kuwania tena ndani ya chama hicho ilifikia tamati jana, baada ya kubainika hana sifa inayostahili kwa mujibu wa katiba ya DRFA.
Uchaguzi huo ambao ulipangwa kufanyika Oktoba 14, umesongezwa mbele hadi Desemba 8, mwaka huu, baada ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA iliyochini ya Mwenyekiti wake, Muhindin Ndolanga kufutwa.
Kamati hiyo ilihusika kwa kiwango kikubwa katika ukiukwaji wa kanuni na taratibu za uchaguzi na kutozingatia matakwa ya katiba ya DRFA katika mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa chama hicho.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Deogratias Lyatto, alisema kwa kuzingatia katiba ya TFF ibara ya 40(1), kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF ibara ya 10(6), 12 (1) na 26 (2) na (3), imeifuta kamati ya DRFA.
Lyatto alisema DRFA imeagizwa kuteuwa kamati mpya ya uchaguzi itakayoandaa na kutekeleza majukumu yake ikizingatia Kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF na Katiba ya DRFA.
Alisema uteuzi huo unatakiwa kufanyika kabla ya Oktoba 25 mwaka huu, ambapo mchakato wa uchaguzi utaanza upya utaanza Oktoba 29 mwaka huu.
Hata hivyo, Lyatto alisema kamati yake ilipitia rufani mbalimbali zilizowasilisha na vyama vya soka vya Mkoa wa Mbeya, Shinyanga na Dar es Salaam.
Kamati hiyomilipokea rufaa dhidi ya Mohamed Salim Bakhressa, ambaye aliomba kuwania nafasi ya mwenyekiti wa DRFA iliyowakilishwa na Michael Wambura na Juma Jabir iliomba jina liondolewa katika orodha ya wagombea kwa kuwa hana elimu ya kiwango cha kidato cha nne na hivyo kutokidhi matakwa ya Katiba ya DRFA Ibara ya 29(2).
‘Mtu yeyote anayegombea nafasi yoyote ya DRFA hana budi awe na kiwango cha elimu kisichopungua kidato cha nne," alisema Lyatto.
Lyatto alisema baada ya kupitia vielelezo kuhusu rufaa dhidi ya maamuzi ya kamati ya uchaguzi ya DRFA na kujadili maelezo ya warufani, Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na ilijiridhisha Bakhressa hana elimu ya kiwango hicho.
Alisema kwa kutokidhi matakwa hayo ya katiba ya DRFA, hastahili kugombea nafasi ya mwenyekiti wa DRFA na kamati ya uchaguzi ilikubaliana na maombi ya warufaa.
Kamati ya uchaguzi ya DRFA iliwapitisha wagombea Gungurugwa Tambaza, Mohammed Bhinda, Benny Kisaka na Hamisi Ayoub 'Mpapai' bila kuwa na vielelezo vinavyothibitisha kuwa wana kiwango cha elimu kisichopungua kidato cha nne.
Kutokana na mkanganyiko, maelezo yenye utata kutoka kwa warufani na warufaniwa na maamuzi ya utata ya kamati ya uchaguzi ya DRFA, yameufanya mchakato wa uchaguzi wa DRFA, kupoteza hadhi ya uchaguzi unaozingatia Kanuni za uchaguzi na misingi ya demokrasia na uwazi kama ilivyoainishwa kwenye kanuni za uchaguzi za TFF.
No comments:
Post a Comment