Na
Sitta Tumma, Geita
SAKATA
la sheria mpya ya Hifadhi ya Mifuko ya Jamii nchini (SSRA), limeanza kuchukuwa
sura mpya, ambapo wafanyakazi wa mgodi wa Geita Gold Mining (GGM),
wameicharukia serikali wakiitaka iwatimue Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia
Kabaka na Mkurugenzi wa Mamlaka ya SSRA.
Mbali
na kuwataka viongozi hao wajiuzulu pia wafanyakazi hao wameitaka serikali
pamoja na Bunge kuhakikisha kipengele cha fao la kujitoa kinaondolewa katika
sheria hiyo namba 5 na si vinginevyo. Tamko hilo limetolewa juzi jioni na
mwenyekiti wa kamati teule ya kufuatilia na kupinga uundwaji wa sheria hiyo,
Deogratias Haule, katika kikao cha pamoja baina ya wafanyakazi hao.
Kwa
mujibu wa Haule, kupitishwa kwa sheria na kipengele hicho, kumeonyesha dhahiri
kwamba serikali haina nia njema na wananchi wake, hivyo ni vema Waziri Kabaka
na Mkurugenzi wa SSRA wakaachia ngazi kwani ndiyo waliohusika kuitunga sheria
hiyo kandamizi na dhalimu. “Kulingana na utata wa sheria hii inayoonekana
kupora fedha na haki zetu, sisi wafanyakazi wa sekta binafsi hatuna imani tena
na Waziri wa Kazi na Ajira pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, tunawataka
wajiuzulu mara moja nyadhifa zao,” alisema.
Kwa
makusudi Waziri Kabaka na Mkurugenzi wa SSRA, waliamua kufunika kombe
mwanaharamu apite, bila kutafakari kwa kina madhara watakayosababishwa na
kipengele cha fao la kujitoa. Kufuatia hali hiyo, wafanyakazi hao wa GGM
walihoji uhalali wa sheria hiyo kuanza kutumika haraka haraka bila kuwa na
kanuni zake, na kwamba uharaka huo una siri ndani yake.
Haule
alihoji pia sababu ya sheria hiyo kutowagusa wabunge, badala yake imetungwa kwa
lengo la wafanyakazi wengine, jambo alilodai limeonyesha ubaguzi mkubwa kwani
wabunge wanaruhusiwa kupewa mafao yao punde Bunge linapovunjwa na Rais. “Hivyo
wafanyakazi walalahoi wanaamini kwamba sheria hii haina nia njema kabisa kwa
mstakabali wa maisha yao na vizazi vyao,” alisema. Aidha alitangaza kwamba
mbunge yeyote atakayeonekana kushabikia au kupendekeza sheria hiyo iendelee
kutumika, wataunganisha nguvu zao kuhakikisha uchaguzi mkuu ujao mbunge huyo
hachaguliwi tena.
Chanzo:
Tanania Daima
No comments:
Post a Comment