BM BARBERSHOP KINONDONI

Tuesday, November 13, 2012

MWANAFUNZI ACHOMWA KISU KWA WIVU WA MAPENZI



Na Lazaro Kaaji, Musoma

MWANAFUNZI wa Chuo cha Utalii cha Musoma Rose Kanyambo (21) ameshambuliwa kwa kisu na John Ogola anayesemekana alikuwa mpenzi wake na kumsababishia majeraha sehemu mbalimbali za mwili. Tukio hilo lilitokea Novemba 2 mwaka huu saa mbili asubuhi katika bweni la chuo hicho lililoko mtaa wa Kamnyonge, manispaa ya Musoma.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Absalom Mwakyoma, alisema chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi.
Alisema aliyejeruhiwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Ogola ambaye pia ni mwanafunzi wa chuo hicho lakini baadaye waliachana na Rose kuanzisha uhusiano na mwanaume mwingine.

Kamanda Mwakyoma alisema mtuhumiwa aliona kuwa hakutendewa haki kutokana na kwamba alikuwa akimgharamia msichana huyo kwa kila alichotaka na ndipo akaamua kumchoma kwa kisu mgongoni na ubavuni hali iliyomsababishia maumivu makali na kukimbizwa Hospitali ya Mkoa wa Mara kwa matibabu.

Akizungumza hospitalini hapo Rose alisema kabla ya tukio hilo Ogola alikuwa akimfuata mara kwa mara akimshawishi awe mpenzi wake. “Alikuwa akinisumbua mara kwa mara akinitaka nikubali kuwa mpenzi wake lakini mara zote nilikuwa nikimkatalia ombi lake ndiyo maana ameamua kunichoma kisu,” alisema Rose.

Baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika chuo hicho walisema kuwa Rose na Ogala walikuwa katika mahusiano ya kimapenzi kwa muda mrefu na kwamba Ogala ndiye aliyekuwa akimgharamia Rose mahitaji yake. Mtumiwa amekamatwa na anatarajiwa kufikishwa mahakamni mara uchunguzi utakapokamilika.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment