CCM imesema imesikitishwa
na iliouita usanii mkubwa unaofanywa na Chadema, kuwahadaa Watanzania kwa
kufanya harambee kwa lengo la kuhalalisha mabilioni ya chama hicho
yanayodaiwa kutolewa na wafadhali kutoka mataifa tajiri duniani. Katibu
wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye
aliyasema hayo leo, Agosti 12, 2012, wakati akizungumza na
waandishi wa habari, kwenye Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, mtaa wa Lumumba
jijijni Dar es salaam.
“Itakumbukwa mara kadhaa
Chadema wamekuwa wakiitisha harambee za kisanii kwa kujaribu kuwahadaa
baadhi ya Watanzania kwa kuwaomba wakichangie chama hicho huku viongozi wa
chama hicho wakijua kuwa tayari wameshapata mabilioni toka kwa wafadhili wao.
Mfano mzuri wa usanii huu ni juzi siku ya Jumamosi, Agosti 10, 2012,
kwenye hoteli ya Serena ambapo walifanyika kiini macho cha harambee na kurushwa
moja kwa moja na kituo kimoja cha televisheni." alisema Nape.
Alisema ,umekuwa ni
utamaduni wa Chadema kuhadaa watu kwa kuitisha harambee za kisanii kina
wanapokuwa wameshapewa mabilioni ya fedha na wafadhili wao, ili mradi
wahalalishe kuwa fedha wanazotumia zimetokana na michango ya watanzania wakati
si kweli. Nape alisisitiza kuwa CCM wanao ushahidi kuhusu zinakotoka
fedha na mikataba wanayoingia Chadema na wafadhili hao na kudai kuwa kama
hawatasema wenyewe basi yeye (Nape) ipo siku atawasaidia kwa kutaja wafadhili
hao na kuanika hadarani mikataba hiyo.
“Tunao ushahidi wa
kutosha unaoonyesha mabilioni waliyopewa Chadema juzi na wafadhili kutoka nje
ya nchi kwa lengo la kuendeleza operesheni zao mbalimbali nchini. Cha
kushangaza badala ya kuwaambia wanachama wao na Watanzania kwa jumla mikataba
na wanakoyapata mabilioni haya, wanawahadaa kwa kuwachangisha na kugeuza mapato
hayo mtaji wa baadhi ya watu binafsi ndani ya chama”, Alisema Nape
Nape alidai kwamba, siri
kubwa inayofichwa kuhusu mikataba na mabilioni wanayopewa Chadema ni kwa sababu
wanaotoa fedha hizo wana ajenda ya kunyemelea rasilimali za nchi hii
zinazoanza kuonyesha matumaini ya kuwepo kwa wingi ili wapate kizikwapua kwa
urahisi kupitia mgongo wa chama hicho.
"Kwanini mabilioni
hayo yanatolewa kwa Chadema wakati huu ambapo sasa Tanzania imo katika kufanya
utafiti na ugunduzi wa rasilimali mbalimbali zikiwamo gesi na mafuta? Na Je
ufadhili huu kwa Chadema licha ya kufichwa sana na kufanywa siri, una nia njema
kwa nchi yetu na rasilimali za nchi yetu? Kwanini ufadhili huu wa mabilioni
unafanywa siri ya watu wachache hata ndani ya chama chenyewe?", Nape
alihoji.
Alisema, hatua hiyo ya
Chadema itaitumbukiza Tanzania katika machafuko yasiyoisha, kama ambavyo
inashuhudiwa katika baadhi ya nchi zenye rasilimali kama madini ambako nchi
zenye utajiri wa fedha zilijipenyeza kupitia walioitwa wapambanaji wa uhuru na
haki katika nchi hizo na hadi sasa hakuna amani.
"Migogoro mingi
tunayoshuhudia hasa katika nchi zinazoendelea pamoja na kuwepo sababu zingine
lakini moja ya chanzo kikubwa ni uwepo wa utajiri wa rasilimali mbalimbali
ambapo mataifa makubwa huzitamani na njia pekee ya kuzipata kwa urahisi ni
kuchochea migogoro ya ndani na hivyo kuwa rahisi kupora rasilimali hizo
wakati wenye nchi wanahangaika katika migogoro na kuachwa wakiwa masikini
wa kutupwa huku waadhirika wakubwa wa migogoro na vita hivi vikiwanufaisha
wakubwa.” Alisema Nape.
Nape alitoa mwito kwa
Watanzania kuwa ni muhimu macho na ulaghai huo wa Chadema na wafadhili wao na
kukitaka chama hicho na wafadhili wao kama kweli wana nia njema na Tanzania,
waweke wazi mashariti ya ufadhili huo wa mabilioni ya fedha ili Watanzania wote
wajue kama yana manufaa kwao au la hasa ikizingatiwa kuwa vyama vya siasa hapa
nchini vinaendeshwa kwa fedha za walipa kodi, hivyo Watanzania wana haki ya
kujua.
Pamoja na kuwataka kuweka
wazi mashariti yanayoambatana na mabilioni hayo Nape aliwataka Chadema waseme
hadharani wenyewe kwamba wamepewa mabilioni hayo, na kuwataka
waache mara moja kuwahadaa Watanzania na kujaribu kujipachika kuwa ni Chama cha
wanyonge kinachotegemea kujiendesha kwa michango ya watanzania huku wakiendelea
kuchukua mabilioni kwa siri kutoka nje.
“ Wasipowaeleza
watanzania ukweli , tutawasidia kuwaeleza watanzania ukweli wa kiasi
halisi cha mabilioni haya, walikozitoa na mikataba waliyoingia. Lengo la hili
ni kuhakikisha kuwa nchi yetu haiwekwi rehani kwa uroho wa madaraka wa baadhi
ya wana siasa.” Nape alisema.
Nape akawaasa wanasiasa,
kuendesha siasa za nchi kwa kuzingatia uzalendo na kukwepa kudumbukia
kwenye tamaa za madaraka kujisahau na kuwa tayari hata kuweka nchi
rehani, hasa kipindi hichi ambapo ugunduzi wa rasilimali mbali mbali hasa
madini, gesi na mafuta vikiwa vinashika kasi nchini na kwamba ugunduzi huo uwe
baraka kwa nchi badala ya laana na kuwa chanzo cha kuiuza nchi.
No comments:
Post a Comment