Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinapinga kauli za
Serikali, Jeshi la Polisi na Chama Cha Mapinduzi (CCM) zenye kulipotosha taifa
kuhusu mashambulizi na mauji yanayoelezwa kufanywa na askari Mkoani Morogoro na
badala yake uchunguzi huru ufanyike haraka kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa
Vifo (Inquest Act). Kauli zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani zina
mwelekeo wa kulilinda Jeshi la Polisi ambalo askari na maafisa wake ni sehemu
ya watuhumiwa wa mauaji badala ya kuwezesha ukweli kuthibitika na hatua
kuchukuliwa kwa wahusika.
Hivyo kutokana na kujirudiarudia kwa mauaji yanayofanywa na vyombo
vya dola CHADEMA kinatoa mwito Rais Jakaya Kikwete ambaye kwa mujibu wa katiba
ibara ya 33 ni mkuu wa nchi, kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu aingilie
na kuwezesha uchunguzi wa kina.
Ikumbukwe kwamba tarehe 27 Agosti 2012 Jeshi la Polisi Mkoani
Morogoro lilifyatua risasi za moto na kupiga mabomu ya machozi wananchi na
wanachama wa CHADEMA waliokuwa wamejikusanya kwa ajili ya kuelekea kwenye
mkutano halali wa CHADEMA na kusababisha kifo cha raia mmoja asiye na hatia na
kujeruhi wengine wawili.
CHADEMA kinaukumbusha umma kwamba kwa mauaji hayo na mengine
katika maeneo mbalimbali nchini serikali inayoongozwa na CCM kupitia vyombo vya
dola inaendelea kukiuka ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ambayo inatambua kwamba uhai ni haki ya msingi wa raia wote.
CHADEMA hakikubaliani na hatua zilizochukuliwa na Serikali mpaka
sasa kuhusu tukio husika pamoja na maelezo yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya
Ndani tarehe 28 Agosti 2012 ambayo kwa sehemu kubwa yametokana na taarifa
zisizo za kweli kutoka kwa maafisa wa Jeshi la Polisi ambao ni sehemu ya
watuhumiwa wa mauaji husika. CHADEMA haina imani na timu iliyoundwa na Mkuu wa
Jeshi la Polisi kuchunguza tuhuma za askari kufyatua risasi na mabomu ya
machozi na kusababisha mauaji kwa kuwa tayari serikali na jeshi la polisi
wametoa maelezo yenye kutofautiana kwa kiwango kikubwa na maelezo ya mashuhuda
waliokuwepo na ushahidi wa picha za eneo la tukio.
Wakati Serikali na Jeshi la Polisi wakitoa maelezo kuwa marehemu
alikutwa umbali wa mita 300 na kupelekwa hospitali na wasamaria wema, mashuhuda
wameeleza wazi kuwa askari walifika jirani na eneo lake na afisa mmoja
akaonyesha ishara na ndipo risasi za moto na mabomu ya machozi yakafyatuliwa
mojawapo kumpata marehemu na kudondoka. Mashuhuda wote waliohojiwa wanaeleza
kwamba bunduki ya polisi ndiyo ilielekezwa na kufyatuliwa kwa marehemu, maelezo
pekee yanayotofautiana ni kuwa baadhi wameeleza kuwa ni bunduki ya risasi za
moto na wengine wa wameeleza kuwa ni bunduki ya kufyatulia mabomu ya machozi.
Mara baada ya kudondoka gari hilo liliondoka na gari lingine la
polisi lilifika likiongozwa na Kamanda wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia cha Mkoa
ambaye alitoa amri ya gari lingine kumbeba Ali Zona na kuondoka naye, hivyo si
kweli kwamba matukio hayo yalitokea mbali na eneo bali pembeni ya meza ya muuza
magazeti huyo karibu na barabara ya kwenda Iringa eneo ambalo polisi ilikuwa
ikifanya mashambulizi.
Kauli zilizotolewa na Serikali kuwa Jeshi la Polisi lilizuia
maandamano ya CHADEMA yaliyopangwa kufanyika Mkoani Morogoro kwa sababu ya
sensa ya watu na makazi si za kweli kwa kuwa sababu pekee zilizotolewa na
ufinyu wa barabara na kuwa maandamano yalipangwa siku ya kazi. Ushahidi wa
suala hili ni barua ya Jeshi la Polisi lenyewe ya 23 Agosti 2012 yenye Kumb.
Na. MOR/A.25/1/VOL. II/202.
CHADEMA kinaujulisha umma kwamba Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro
ndilo lililoacha kuheshimu utawala wa sheria na makubaliano yaliyofikiwa baada
ya mazungumzo yaliyohusisha kikosi kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi
kikiongozwa na Kamanda wa Operesheni za Jeshi hilo Simon Siro na hivyo kuwa
chanzo cha mauaji yaliyotokea na madhara mengine kwa wananchi waliokuwepo
maeneo yaliyorushiwa mabomu ya machozi.
Ikumbukwe kwamba awali CHADEMA ilipanga kufanya maandamano na
mikutano katika Jimbo la Morogoro Mjini tarehe 4 Agosti 2012 na kuwasilisha
taarifa kwa Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, Polisi wakakataa kufanyika kwa maandamano na mikutano
kwa kisingizio cha sikukuu ya nane, mgomo wa walimu na ratiba kugongana na ile
ya mikutano ya CCM sababu ambazo zilibainika kwamba hazikuwa na msingi wowote.
Baada ya mvutano na mazungumzo CHADEMA ilikubali kutii sheria na
kuzingatia matakwa ya Jeshi la Polisi pamoja na kuwa yalitolewa kinyume cha
Sheria kwamba maandamano na mkutano wa CHADEMA vifanyike mara baada ya siku ya
kuanza kwa sensa tarehe 26 Agosti 2012 na CHADEMA ilipendekeza tarehe 27 Agosti
2012 ambayo Jeshi la Polisi liliikubali.
Polisi walifanya hivyo wakielewa ukubwa wa barabara za Morogoro na
pia wakitambua kwamba ilikuwa ni siku ya kazi, hata hivyo tarehe 23 Agosti 2012
Jeshi la Polisi na kuandika barua ya kueleza kwamba imetoa kibali cha mkutano
(suala ambalo si mamlaka yake kisheria) na pia ikakataza maandamano.
CHADEMA ikaamua kwa mara nyingine tena kurudi katika meza ya
mazungumzo mengine kati ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro tarehe 24 Agosti
2012 ambapo polisi ilikubali maandamano ikiwemo ya watembea kwa miguu na
kupendekeza njia mbadala na tarehe 26 Agosti 2012 mazungumzo yakaendelea kwa
lengo la kukagua barabara.
Hata hivyo, kufuatia shinikizo la Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Morogoro Faustine Shilogile kinyume na Sheria ya Jeshi la Polisi ambayo imetoa
mamlaka kwa Mkuu wa Polisi Wilaya kuhusu taarifa za mikutano polisi ikarejea
katika msimamo wa kukataza mapokezi ya watembea kwa miguu na badala yake tarehe
26 Agosti 2012 bila sababu zenye misingi ya kisheria na zisizozingatia
haki za kikatiba ikapendekeza kwamba yafanyike mapokezi kwa kutumia magari.
Maelezo ya Waziri wa Mambo ya Ndani iwapo vyama vya siasa
visiporidhika na mazingira kama hayo yapo mamlaka ya kukata rufaa yanapotosha
kwa kuwa Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa hazijaweka
utaratibu wa rufaa hivyo njia pekee ya kisheria ni kutumia mahakama.
Jeshi la Polisi lingeheshimu utawala wa sheria na mazungumzo
lingeruhusu CHADEMA ifanye maandamano na kutoa ulinzi mpaka eneo la mkutano kwa
muda mfupi badala yake jeshi hilo likaamua kutumia nguvu kubwa na kusababisha
mauaji, barabara kufungwa kwa muda mrefu na kuathiri wananchi waliokuwa
wakiendelea na kazi zao.
Iwapo wanachama na wananchi waliokuwa wamekusanyika kuwapokea
viongozi na kuelekea kwenye mkutano wangekuwa wamekiuka sheria Jeshi la Polisi
lingeweza kuwamata kwa mujibu wa sheria, hata hivyo hakuna kiongozi yoyote wa
CHADEMA aliyefunguliwa jalada mpaka sasa katika kituo chochote cha polisi kwa
kudaiwa kukiuka sheria.
Kinyume chake Jeshi la Polisi ambalo lilikuwa kwenye mazungumzo
limekubali kuwa mapokezi yafanyike kwa kwa msafara wa vyombo vya usafiri tarehe
27 Agosti 2012 likaamua kupiga mabomu ya machozi kwa wananchi na wanachama wa
CHADEMA waliokuwa wamekusanyika eneo la Msamvu wakiwasubiri viongozi bila hata
ya kusubiri kuona iwapo yangefanyika matembezi ya miguu kuelekea eneo la
mkutano au maandamano ya magari na vyombo vingine vya usafiri.
Kitendo cha Jeshi la Polisi kutumia nguvu kubwa kinyume cha sheria
na kusababisha mauaji na kufunga barabara kwa muda mrefu kiliwafanya wanachama
wa CHADEMA na wananchi kwa ujumla kutawanyika kuelekea eneo la mkutano na
wengine kuingia barabarani kutembea kuelekea eneo la mkutano na hatimaye polisi
walipoona wamesababisha hali hiyo wakaamua kulinda misafara hiyo mpaka eneo la
mkutano hali inayodhihirisha kuwa uamuzi kama huo ungechukuliwa kutoka mwanzo
yasingetokea madhara yoyote.
Kwa kuzingatia utofauti mkubwa baina ya maelezo yanayotolewa na
Serikali na Jeshi la Polisi kuhusu matukio husika na ukweli halisi
ulivyotokea CHADEMA kinasisitiza kuwa uchunguzi huru ufanyike kwa mujibu
wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act) Sura ya 24 ya Sheria za Tanzania.
CHADEMA kwa mara nyingine kinaitaka Serikali inayoongozwa na CCM
kurejea katika kifungu cha 3 cha Sheria hiyo ambacho kinatoa mamlaka ya Waziri
mwenye dhamana na masuala ya Sheria kuanzisha Mahakama ya Kuchunguza Vifo hivyo
(Coroner’s Court) katika maeneo ya serikali za mitaa kwa kushirikiana na Jaji
Kiongozi.
CHADEMA kinaikumbusha Serikali kuwa iliahidi bungeni kufuatia
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mawaziri vivuli husika kueleza
bungeni taarifa za mauaji yaliyofanywa na vyombo vya dola kwa nyakati
mbalimbali Waziri Mkuu na Mawaziri wengine waliahidi kwamba sheria hiyo itaanza
kutumika kuchunguza vifo vyenye utata hivyo katika muktadha huo uchunguzi wa
kifo cha Ali Zona haupaswi kufanywa na timu ya polisi bali sheria hiyo sasa
ianze kutumika.
Kwa upande mwingine, CHADEMA imeheshimu taratibu za maziko
zilizopangwa na familia ambapo mwili wa marehemu ulisafirishwa jana tarehe 28
Agosti 2012 kwenda Mkoani Tanga kwa ajili ya maziko na CHADEMA kuwasilisha
rambirambi zake za awali, taarifa zaidi kuhusu ushiriki kwa CHADEMA kwenye
maziko zitaelezwa baada ya majadiliano yanayoendelea na familia.
CHADEMA kwa kuheshimu mazungumzo na utawala wa sheria kwa mara
nyingine tena tarehe 28 Agosti 2012 CHADEMA kimesitisha Operesheni za Maandamano
na Mikutano yake ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) kwa rai iliyotolewa na Mkuu wa
Jeshi la Polisi (IGP) kupitisha kukamilika kwa zoezi la sensa ambayo imetokana
pia na maelezo ya mamlaka zingine za kiserikali.
CHADEMA inatambua kwamba wakati maandamano ya CHADEMA yametolewa
rai kuwa yasitishwe kupisha sensa, maandamano ya wagombea wa CCM kurudisha fomu
za uchaguzi wa ndani ya chama chao yameachwa yakiendelea katika barabara kadhaa
nchini bila kusitishwa kwa kisingizio hicho.
Aidha, wakati CHADEMA ikiheshimu mazungumzo na kusogeza ratiba
yake mbele ya tarehe 26 Agosti 2012 mpaka tarehe 27 Agosti 2012 kupitisha Sensa
hatua ambayo ilifanywa pia na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo ilitangaza
ratiba yake kuendelea baaada ya tarehe hiyo. Tume hiyo inaendelea na mikutano
yake ya hadhara inayokutanisha wananchi katika kata za mikoa mbalimbali wakati
huo huo zoezi la sensa likiendelea lakini kwa mikutano ya CHADEMA inaonekana
kufanyika kwake ni kuingilia sensa.
CHADEMA inataka Serikali na Polisi kueleza iwapo matukio haya na
mengine hayana mwelekeo wa ubaguzi na uhujumu wa vuguvuvugu la mabadiliko
linaloendelea nchini kwa kurejea ukweli kuwa maisha ya wachache yanaweza
kuwekwa mashakani lakini si mabadiliko kwa maslahi ya wengi.
CHADEMA itaeleza hatua za ziada itakazochukua baada ya kupata
ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu (post mortem) uliofanyika tarehe 28
Agosti 2012 na uamuzi wa Serikali kukubali au kukataa mwito wa kutumia sheria
ya Vifo (Inquest Act) kuwezesha uchunguzi huru.
Imetolewa
tarehe 29 Agosti 2012 na:
John John
Mnyika (Mb)
Mkurugenzi
wa Habari na Uenezi
CHADEMA
No comments:
Post a Comment