BM BARBERSHOP KINONDONI

Wednesday, August 29, 2012

MKUU WA WILAYA YA KOROGWE AMTUSI MWANASHERIA TUSI LA NGUONI



MKUU WA WILAYA YA KOROGWE AMDHALILISHA MWANASHERIA WAKE
Mkuu wa Wilaya Korogwe ndugu Mrisho Gambo amemwambia mwanasheria wa wilaya hiyo kuwa ana degree ya chupi kufuatia majibu ya mwanasheria huyo dhidi ya kesi kati ya wafanyabiashara na halmashauri. Mwanasheria huyo alishindwa kutoa maelezo ya kina juu ya sakata hilo ndipo Mkuu huyo wa Wilaya akatoa kauli hiyo (KUMCHANA).

WASIFU WA BWANA MRISHO GAMBO
Bwana Mrisho Gambo Mkuu wa Wilaya ninayotokea mimi alizaliwa Mei 22, mwaka 1982 katika Hospitali ya Ocean Road ya Dar es Salaam. Alipata Elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Ilala Boma na kuhitimu darasa la saba mwaka 1997 na kupata bahati ya kuchaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari kidato cha kwanza hadi cha nne, katika Shule ya Sekondari Kibaha na kuhitimu kidato cha nne mwaka 2001. Mwaka 2002 nilichaguliwa kujiunga kidato cha tano Shule ya Ufundi Tanga, maarufu kama Tanga Technical School na kumaliza kidato cha sita mwaka 2004.

Mwaka 2005 alichaguliwa kujiunga na elimu ya juu, katika Chuo cha Uhasibu Arusha, kusomea stashahada ya juu katika Sayansi ya Kompyuta (computer science) na kuhitimu mwaka 2008. Mwaka 2009 niliajiriwa kwa nafasi ya mchambuzi wa mifumo ya kompyuta katika Halmashauri ya Jiji la Arusha. Mwaka 2011, aliajiriwa kama msimamizi mwandamizi wa mifumo ya kompyuta wa Chuo cha Kimataifa cha Nelson Mandela. Mwaka 2011 alijiuzulu nafasi hiyo pale Chuo cha Nelson Mandela na kurudi Jiji la Arusha. Gambo alirudi Arusha kwa kuwa hakuwa ameacha kazi, bali aliomba likizo bila malipo. Baadaye aliendelea na safari yake kielimu mwaka 2010 alipojiunga tena Chuo cha Uhasibu Arusha kwa ajili ya shahada ya uzamili (masters degree) katika masuala ya uongozi na teknolojia ya habari na kuhitimu mwaka 2011.

MASWALI HAYA ALIULIZWA NA GAZETI LA RAIA MWEMA KAMA IFUATAVYO
Raia Mwema: Wewe ni mtaalamu wa masuala ya kompyuta na kwa kiasi kikubwa umepata mafanikio kielimu. Nini hasa kilikusukuma kuingia katika siasa katika umri wako huo mdogo?

Gambo: Kwanza mimi ni kada na kiongozi mwaminifu kabisa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na masuala ya siasa nilianza muda mrefu kidogo. Niliwahi kuwa kiongozi wa wanafunzi nilipokuwa shule ya msingi pale Boma na katika hili, hata Mrisho Mpoto (msanii maarufu wa muziki na maigizo) atakuwa shahidi japo yeye alinitangulia kwa mbali sana.

Pia pale Kibaha Sekondari nilikuwa Mbunge (Bunge la Wanafunzi). Nakumbuka pale nilipata changamoto sana. Unajua Kibaha Sekondari ni shule ya watoto wenye vipaji  pekee kiakili, walimu walikuwa hawafundishi sana, nikawaambia wenzangu sasa tupo kidato cha tatu mwishoni lakini masomo ya nusu mwaka hatujamaliza nafikiri hii si sawa. Nataka tuwaite walimu mmoja mmoja watueleze kwa nini hawatimizi wajibu wao ipasavyo. Wenzangu waliogopa kweli lakini tulifanya. Wakati wa likizo nikaitwa kwenye kikao cha nidhamu na kutishiwa kweli. Lakini nilibaki katika msimamo wangu kuhusu hatua tulizo zichukua kama wanafunzi kwa sababu tulimsainisha mkataba kila mwalimu na kukubaliana muda wa yeye kumaliza mada zake. Tangu kipindi hicho mahudhurio ya walimu yalikuwa mazuri na mambo yalikwenda barabara. Nilipokuwa kidato cha tano pale Tanga Technical School, niliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu katika Serikali ya Wanafunzi. Mwaka 2006, nilikuwa mwenyekiti wa CCM tawi la Chuo cha Uhasibu Arusha. Kipindi hicho cha uongozi wangu kwa kushirikiana na wenzangu wa vyuo mbalimbali vya Arusha tulifanikiwa kushawishi vijana wenzetu wengi kujiunga na CCM. Mbunge wa Mvomero, Amos Makalla alitusaidia sana katika mchakato huo. Kwa ufupi, harakati hizi za siasa nilianza kitambo kidogo. Wakati wote kwa kweli nimekuwa nikisukumwa na dhamira yangu ya kupenda kutumikia watu.

Raia Mwema: Unaelezeaje uzoefu ulioupata ukiwa katika ushiriki wa siasa za CCM katika nafasi za uongozi ngazi ya tawi kwa mfano na ngazi nyingine?
Gambo: Kimsingi, uzoefu wangu kiuongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi ni mkubwa. Nina nafasi mbalimbali ndani ya CCM na umoja wetu wa vijana katika chama chetu. Kwa upande wa Umoja wa Vijana (UVCCM), mimi ni mjumbe wa Baraza Kuu la Vijana wa CCM ngazi ya Taifa, kutokea mkoani Arusha.
Lakini pia ni mjumbe wa kamati ya utekelezaji ya vijana wa CCM Mkoa wa Arusha, pia ni mjumbe wa Baraza Kuu la Vijana wa CCM Mkoa wa Arusha na pia mjumbe wa Baraza Kuu la Vijana la Wilaya ya Arusha Mjini. Kwa upande wa Chama, mimi ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha na pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Arusha Mjini.
Kwa kweli wakati nagombea ujumbe wa Baraza Kuu la CCM Taifa, niliahidi mambo makubwa mawili. Kwanza, ni kugawa kanuni za umoja wa vijana wa CCM kwa Mwenyekiti, Katibu na Katibu Uhamasishaji kwa kata zote 101 wakati huo pamoja na viongozi wote wa wilaya na mkoa. Nilifanikiwa kugawa kanuni kama nilivyoahidi kwa lengo kuu la kuwawezesha vijana wenzangu kuijua jumuiya yetu vizuri zaidi. Pili niliahidi kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana mbalimbali wa Mkoa wa Arusha. Hili nalo nilifanikiwa kwa kiasi kikubwa. Nilitoa semina hiyo kwa kata 37 za Wilaya ya Arumeru pamoja na kata 12 za Wilaya ya Monduli. Michakato mingine inaendelea kukamilisha wilaya zilizobaki. Tuliahidi pia kuanzisha SACCOS ambayo aliyekuwa Mbunge wa Arusha, Felix Mrema na Mbunge mwenzake, Elisa Mollel walituchangia kiasi cha milioni moja kila mmoja. Lakini cha kushangaza hadi leo hazijulikani zimeenda wapi. Binafsi nasubiri kikao kijacho cha vijana ili niweze kuuliza vizuri. Kama kuna mtu kakaa nazo hizo fedha kwa manufaa yake binafsi lazima arudishe na riba maana fedha hizo zilitolewa tangu mwaka 2009. Kwa ujumla naamini kwa kiasi kikubwa nimekidhi matarajio ya ninaowaongoza.

Raia Mwema: Hivi karibuni umetangaza nia ya kugombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki. Je, nini hasa kilikusukuma hadi kutangaza nia hiyo?
Gambo: Kwa kweli nimesukumwa na mambo mengi sana kufikia uamuzi huu. Kwanza nimefanya kazi na asasi za vijana kwa zaidi ya miaka kumi. Nimepata fursa ya kuwakilisha vijana kwenye nchi mbalimbali kwa masuala tofauti. Nakumbuka mwaka 2006 kupitia asasi iitwayo YUNA niliwakilisha vijana wa Tanzania nchini Kenya, kwenye mkutano wa masuala ya Afrika Mashariki na Kati, na malengo ya Millenia. Mwaka 2007 nilialikwa nchini Zimbabwe kwenda kutoa mada kwenye mkutano wa masuala ya Amani na Migogoro barani Afrika. Pia nimeshiriki kwenye majadiliano mbalimbali yanayohusu masuala ya Afrika Mashariki. Nakumbuka wakati ule imeundwa Tume ya Profesa Wangwe ya kuchukua maoni ya Watanzania kuhusu mchakato wa kuharakisha kuwa na Shirikisho la Afrika Mashariki. Nilikutana kwenye kikao hicho na Mbunge Pindi Chana, Mzee Joseph Butiku na Zitto Kabwe. Vijana maoni yetu yalikuwa wazi kuwa hatupingi kuungana lakini kama nchi tunahitaji maandalizi ya kutosha ili watu wetu waweze kunufaika na Shirikisho hilo. Tukasema nchi zilizoendelea mfano za Ulaya, wao wametumia zaidi ya miaka kumi  kukubaliana kuwa na sarafu ya moja na bado hawakuweza kukubaliana nchi zote.Sasa kwa nini sisi tunataka kuchukua chini ya miaka 15 kukamilisha hatua zote  nne tena bila maandalizi? Yaani tukamilishe ushuru wa forodha, soko la pamoja, sarafu moja na Shirikisho la Afrika Mashariki kwa kipindi kifupi, kwa shinikizo la nani? Na haraka ya nini? Pia mwaka 2007, nilichaguliwa kuwa mwenyekiti wa asasi ya vijana kwa nchi zote tano za Afrika Mashariki. Nchi za Tanzania, Uganda Kenya, Rwanda na Burundi zote zilileta wawakilishi wao kwenye uchaguzi uliofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa AICC Arusha. Nakumbuka John Mnyika, Mbunge wa sasa wa Ubungo ndiye alikuwa mwandishi wa mkutano ule. Tulimwomba afanye kazi hiyo kwa kuwa yeye alikuwa na uwezo na uzoefu mkubwa kuandika ripoti za mikutano mikubwa.
Pia nimeshiriki kwenye mijadala mbalimbali ya masuala ya Afrika Mashariki kwenye ushuru wa forodha na soko la pamoja katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
Pamoja na hayo, niliwahi kuwa msaidizi wa Mbunge wa Afrika Mashariki Dk. George Nangale. Nilifanya naye kazi kama mtafiti msaidizi. Nilijifunza mengi sana kutoka kwa Dk. Nangale, wakati  wote alikuwa anapenda kufanya mambo ambayo mwishowe yanaleta matokeo chanya kwa jamii. Nakumbuka namna alivyo kuwa anasukuma muswada wa “Transboundary and Ecosystem”. Naambiwa sasa huo muswada uko kwenye hatua za mwisho. Kwa ujumla utaona nimepata uzoefu wa kutosha kwenye mambo haya ya EAC. Lakini pia vijana ni zaidi ya asilimia 65 ya watu wote wa Afrika, binafsi naamini kundi hili la vijana halijapata uwakilishi mzuri. Wenzetu kule Rwanda wametenga nafasi moja kwa ajili ya vijana.  Nafikiri ni wazo jema kwa Tanzania Bara tukawa na nafasi moja kwa ajili ya kundi la vijana. Pia kuna kitu wenzetu  wazungu wanaita “succession planning”. Nina amini kwamba tunapaswa tuanze kuwaunga mkono na kuwainua  viongozi vijana wenye uwezo ili kuanza kufanya hiyo Succession Planning (maandalizi ya viongozi). Pamoja na hayo nataka kuwa sauti ya wanyonge, sauti ya under – preveleged na si sauti ya wanasiasa pekee. Kwa mantiki hiyo, nina amini kuwa nina kila sababu ya kuwania nafasi hiyo.

Raia Mwema: Waliojitokeza kuwania nafasi ya ubunge wa Afrika Mashariki ni wengi mno, umejipanga kwa namna gani kushiriki ili hatimaye ushinde?
Gambo: Jambo la kuvutia ni kwamba, uchaguzi wa wabunge wa Afrika Mashariki wapiga kura wake ni wabunge wetu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa imani yangu binafsi, wabunge wetu hao ambao ni makini, huwezi kuwadanganya kwa njia yoyote kwani wana uwezo mkubwa wa kupima uwezo, ari na dhamira ya kila mgombea kwa sababu nao ni wazoefu katika masuala ya chaguzi zenye ushindani mkali na wengi ni wanataaluma waliobobea katika masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Binafsi, naamini nina uwezo mkubwa wa kuwa mbunge bora wa Afrika Mashariki bila kujali idadi ya wagombea wenzangu ni kubwa au ndogo na msimamizi wangu katika mchakato huu ni Mwenyezi Mungu. Mungu hamwachi mja wake.

Raia Mwema: Endapo utafanikiwa kushinda ubunge wa Afrika Mashariki, nini vipaumbele vyako kiutendaji kama mbunge?
Gambo: Jumuiya ya Afrika Mashariki ni jumuiya yenye michakato mingi ya msingi. Pamoja na mambo mengine, nitahakikisha vijana wa Tanzania na wananchi kwa ujumla wanapata fursa ya kushiriki ipasavyo kwenye michakato yote inayohusu Jumuiya hiyo ya Afrika Mashariki.
Kwa mfano ni Watanzania wachache sana ambao wanajua kuwa katika ile hatua ya ushuru wa forodha ilitolewa miaka mitano kwa nchi za Afrika Mashariki pamoja na Tanzania kupeleka bidhaa nchini Kenya bila ushuru ili kutoa mwanya kwa nchi kama Tanzania kujipanga kutokana na tofauti yake kiuchumi na Kenya.
Sasa wasli linalojitokeza ni je, Watanzania wangapi walinufaika na fursa hiyo? Wabunge wetu wa wakati  huo walifanya juhudi za kutosha? Na je, Wizara ya Afrika Mashariki iliweka msukumo wa kutosha?
Nakumbuka wenzetu wa Kenya walizindua mkakati wao wa mawasiliano kwenye masuala ya EAC, mkakati huo waliuita “EAC Communication Strategy”. Hapa kwetu sijawahi kusikia kitu kama hicho, inawezekana kipo lakini bado binafsi sijasikia. Kwa hiyo, kipaumbele changu cha kwanza kitakuwa ni kuhakikisha Watanzania wanapata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu mambo yanavyokwenda pale EAC.
Binafsi nilifurahishwa na ziara ya mipakani ya hivi karibuni ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta. Nakumbuka alikwenda Namanga na Holili, kule alitatua changamoto nyingi ambazo asingeweza kuzitatua akiwa kwenye kiti chake pale ofisini Jengo la Water Front, Dar es Salaam.
Mambo kama matumizi ya kadi ya manjano mipakani pamoja na kodi ya kichwa, ambayo yalikuwa kero kubwa aliyamaliza. Ni lazima wizara na taasisi za Serikali ziwe sehemu ya kuwawezesha wananchi kufanya shughuli zao kwa amani, ili mchakato wa kuelekea Shirikisho la EAC uwe wenye tija.
Raia Mwema: Unadhani tangu kurejeshwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki hadi sasa, jumuiya hiyo imekidhi matarajio ya wananchi wa nchi husika?
Gambo: Nafikiri ni mapema sana kujua kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki imekidhi matarajio au la. Ila kwa kuwa wananchi hawashirikishwi kwa kiasi kikubwa kwenye michakato ya EAC, ni rahisi sana kusema kuwa EAC haikidhi matarajio.
Mfano, mchakato wa ushuru wa forodha ulioanza mwaka 2005 unaohusisha Soko la Pamoja, majadiliano yalikwishakusainiwa na utekelezaji umeanza. Majadiliano kuhusu kuwa na sarafu ya  pamoja yameanza na ilitakiwa Desemba, mwaka huu tumalize mambo ya sarafu ya pamoja, isipokuwa marais wetu bado hawajasaini Itifaki ya Sarafu ya Pamoja na inatarajiwa kwenye kikao kijacho cha marais wa EAC, huenda wakasini itifaki hiyo.
Na ratiba ilikuwa inaonyesha mwakani, mwaka 2013 tuwe kwenye Shirikisho la Afrika Mashariki. Utaona kama kuna uharaka fulani hapa. Kwa uharaka huu, huwezi kamwe kukidhi matarajio ya watu.
Raia Mwema: Nchi za EAC zinasuasua katika utekelezaji wa mipango ya pamoja. Mambo gani unadhani yafanyike ili kuondokana na hali hiyo?
Gambo: Kwa maoni yangu, namna pekee kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kutekeleza mipango ya pamoja kwa urahisi ni kuwa na Shirikisho la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kila nchi kufanya mipango yake kipekee pekee nadhani inaongeza changamoto zaidi ndani ya Jumuiya.
Katika hili nitakupa mfano, angalia ile barabara ya Afrika Mashariki ya Namanga. Kipande cha kutoka Namanga kwenda Kenya kiko sawa sana na kwa ubora wa hali ya juu, lakini kutoka Namanga kuja Arusha kiwango chake kinatia shaka mno. Hii ni changamoto kubwa kwa nchi yetu ya Tanzania. Ni mradi mmoja unaohusika na barabara ya Namanga, Kenya na Namanga Tanzania. Swali la kujiuliza ni kwa nini Namanga-Kenya kuwe bora zaidi kuliko Namanga-Tanzania?  Pengine mambo haya tungeyaangalia kwa pamoja yangekuwa sawa zaidi.
Raia Mwema: Nini tathmini yako kuhusu nafasi ya vijana kisiasa katika nchi za Afrika Mashariki?
Gambo: Kimsingi nafasi ya vijana ni finyu sana katika nchi za Afrika Mashariki. Na hii inasababishwa na kukosekana kwa chombo mahsusi cha kushughulika na masuala ya vijana pale Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa kifupi, hatuna Baraza la Vijana la Afrika Mashariki.
Nchi za Afrika Mashariki zimekubaliana kuwa na Baraza la Vijana la Afrika Mashariki hadi kufikia Desemba, mwaka huu.
Hapa kuna jambo linashangaza kidogo, katika nchi tano za Afrika Mashariki nchi za Rwanda, Uganda na Burundi tayari zina Baraza la Vijana la Taifa katika kila nchi. Kenya wameshakamilisha michakato yote na tayari wameshaunda bodi inayoshughulika na masuala ya vijana, wakati wowote wanakwenda kwenye uchaguzi wa viongozi wa Baraza la Vijana la Taifa la Kenya.
Hapa kwetu Tanzania mchakato wa kupata Baraza la Vijana la Taifa ulipata kasi mwaka 1994. Lakini cha ajabu hadi leo tunafanya kazi ya kujadili sera tu. Hii ni changamoto kubwa sana. Imefika wakati sasa tuache siasa kwenye mambo ya msingi. Ni muhimu tukapata chombo cha vijana hapa Tanzania na Afrika Mashariki. Chombo hiki muhimu kitawasaidia vijana kujadili masuala mbalimbali yanayohusu mustakabali wa taifa lao na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla.
Kwenye Baraza la Taifa la Vijana watu watajadili nje ya itikadi za vyama vyao vya siasa. Mwaka 2011, nilikutana na Rais Paul Kagame kule Ikulu ya Kigali, Rwanda. Rais Kagame alisema; “Unajua dunia ya leo ni dunia ya vijana ndiyo maana mimi ukienda ofisi karibu zote utakuta vijana wana madaraka makubwa na hiyo ni moja ya sababu ya  Rwanda kuendelea kwa kasi. Lakini lazima mkumbuke kuwa ujana ni namna akili yako inavyofanya kazi na si umri maana kuna vijana wengine wanafikiri kama wazee na wazee wengine wanafikiri zaidi ya vijana.”
Sasa kimsingi kukosekana kwa chombo hiki kuna nifanya nitafsiri kuwa nafasi ya vijana ni finyu sana katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Raia Mwema: Waliojitokeza kuwania nafasi hiyo wengi ni wenye umri wa zaidi ya miaka 65. Wewe ni mdogo kiumri kwao na hata kisiasa kwa baadhi ya washindani wako. Umejipanga vipi?
Gambo: Kama utakumbuka mwanzo kabisa wanaume tuliochukua fomu kwa ajili ya kuomba kupitishwa na chama chetu ili kugombea ubunge wa Afrika Mashariki tulikuwa 45. Tukachujwa na Kamati Kuu ya CCM tukabaki 18. April 3, 2011, tulipigiwa kura ya maoni na wabunge wa CCM na kubaki tisa, ambao tutakwenda kuomba ridhaa ya wabunge wote, bungeni Dodoma April 17, 2011.

1 comment:

  1. Inawezekana Gambo ni mtu makini hapendi uzembe. Hata hivyo namshauri kuwa na busara na asiogope kuchukuwa hatua zinazostahili kwa watumishi wazembe badala ya kuwatukana.

    ReplyDelete