Mkuu wa
Wilaya Korogwe ndugu Mrisho Gambo amemwambia mwanasheria wa wilaya hiyo kuwa
ana degree ya chupi kufuatia majibu ya mwanasheria huyo dhidi ya kesi kati ya
wafanyabiashara na halmashauri. Mwanasheria huyo alishindwa kutoa maelezo ya
kina juu ya sakata hilo ndipo Mkuu huyo wa Wilaya akatoa kauli hiyo (KUMCHANA).
WASIFU WA BWANA MRISHO GAMBO
Bwana Mrisho Gambo Mkuu wa Wilaya ninayotokea
mimi alizaliwa Mei 22, mwaka 1982 katika Hospitali ya Ocean Road ya Dar es
Salaam. Alipata Elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Ilala Boma na kuhitimu
darasa la saba mwaka 1997 na kupata bahati ya kuchaguliwa kuendelea na masomo
ya sekondari kidato cha kwanza hadi cha nne, katika Shule ya Sekondari Kibaha
na kuhitimu kidato cha nne mwaka 2001. Mwaka 2002 nilichaguliwa kujiunga kidato
cha tano Shule ya Ufundi Tanga, maarufu kama Tanga Technical School na kumaliza
kidato cha sita mwaka 2004.
Mwaka 2005 alichaguliwa kujiunga na elimu ya juu,
katika Chuo cha Uhasibu Arusha, kusomea stashahada ya juu katika Sayansi ya
Kompyuta (computer science) na kuhitimu mwaka 2008. Mwaka 2009
niliajiriwa kwa nafasi ya mchambuzi wa mifumo ya kompyuta katika Halmashauri ya
Jiji la Arusha. Mwaka 2011, aliajiriwa kama msimamizi mwandamizi
wa mifumo ya kompyuta wa Chuo cha Kimataifa cha Nelson Mandela. Mwaka 2011 alijiuzulu
nafasi hiyo pale Chuo cha Nelson Mandela na kurudi Jiji la Arusha. Gambo alirudi
Arusha kwa kuwa hakuwa ameacha kazi, bali aliomba likizo bila malipo. Baadaye aliendelea na safari yake kielimu mwaka
2010 alipojiunga tena Chuo cha Uhasibu Arusha kwa ajili ya shahada ya uzamili (masters
degree) katika masuala ya uongozi na teknolojia ya habari na kuhitimu
mwaka 2011.
MASWALI HAYA ALIULIZWA NA GAZETI LA RAIA
MWEMA KAMA IFUATAVYO
Raia Mwema: Wewe ni
mtaalamu wa masuala ya kompyuta na kwa kiasi kikubwa umepata mafanikio kielimu.
Nini hasa kilikusukuma kuingia katika siasa katika umri wako huo mdogo?
Gambo: Kwanza mimi ni kada na
kiongozi mwaminifu kabisa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na masuala ya siasa
nilianza muda mrefu kidogo. Niliwahi kuwa kiongozi wa wanafunzi nilipokuwa
shule ya msingi pale Boma na katika hili, hata Mrisho Mpoto (msanii maarufu wa
muziki na maigizo) atakuwa shahidi japo yeye alinitangulia kwa mbali sana.
Pia pale Kibaha Sekondari nilikuwa Mbunge (Bunge
la Wanafunzi). Nakumbuka pale nilipata changamoto sana. Unajua Kibaha Sekondari
ni shule ya watoto wenye vipaji pekee kiakili, walimu walikuwa
hawafundishi sana, nikawaambia wenzangu sasa tupo kidato cha tatu mwishoni
lakini masomo ya nusu mwaka hatujamaliza nafikiri hii si sawa. Nataka tuwaite
walimu mmoja mmoja watueleze kwa nini hawatimizi wajibu wao ipasavyo. Wenzangu
waliogopa kweli lakini tulifanya. Wakati wa likizo nikaitwa kwenye kikao cha
nidhamu na kutishiwa kweli. Lakini nilibaki katika msimamo wangu kuhusu hatua
tulizo zichukua kama wanafunzi kwa sababu tulimsainisha mkataba kila mwalimu na
kukubaliana muda wa yeye kumaliza mada zake. Tangu kipindi hicho mahudhurio ya
walimu yalikuwa mazuri na mambo yalikwenda barabara. Nilipokuwa kidato cha tano pale Tanga Technical
School, niliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu katika Serikali ya Wanafunzi.
Mwaka 2006, nilikuwa mwenyekiti wa CCM tawi la Chuo cha Uhasibu Arusha. Kipindi
hicho cha uongozi wangu kwa kushirikiana na wenzangu wa vyuo mbalimbali vya
Arusha tulifanikiwa kushawishi vijana wenzetu wengi kujiunga na CCM. Mbunge wa Mvomero, Amos Makalla alitusaidia sana
katika mchakato huo. Kwa ufupi, harakati hizi za siasa nilianza kitambo kidogo.
Wakati wote kwa kweli nimekuwa nikisukumwa na dhamira yangu ya kupenda
kutumikia watu.
Raia Mwema: Unaelezeaje
uzoefu ulioupata ukiwa katika ushiriki wa siasa za CCM katika nafasi za uongozi
ngazi ya tawi kwa mfano na ngazi nyingine?
Gambo: Kimsingi, uzoefu wangu
kiuongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi ni mkubwa. Nina nafasi mbalimbali ndani
ya CCM na umoja wetu wa vijana katika chama chetu. Kwa upande wa Umoja wa
Vijana (UVCCM), mimi ni mjumbe wa Baraza Kuu la Vijana wa CCM ngazi ya Taifa,
kutokea mkoani Arusha.
Lakini pia ni mjumbe wa kamati ya utekelezaji ya
vijana wa CCM Mkoa wa Arusha, pia ni mjumbe wa Baraza Kuu la Vijana wa CCM Mkoa
wa Arusha na pia mjumbe wa Baraza Kuu la Vijana la Wilaya ya Arusha Mjini. Kwa upande wa Chama, mimi ni mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha na pia ni mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Arusha Mjini.
Kwa kweli wakati nagombea ujumbe wa Baraza Kuu la
CCM Taifa, niliahidi mambo makubwa mawili. Kwanza, ni kugawa kanuni za umoja wa
vijana wa CCM kwa Mwenyekiti, Katibu na Katibu Uhamasishaji kwa kata zote 101
wakati huo pamoja na viongozi wote wa wilaya na mkoa. Nilifanikiwa kugawa kanuni kama nilivyoahidi kwa
lengo kuu la kuwawezesha vijana wenzangu kuijua jumuiya yetu vizuri zaidi. Pili niliahidi kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa
vijana mbalimbali wa Mkoa wa Arusha. Hili nalo nilifanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Nilitoa semina hiyo kwa kata 37 za Wilaya ya Arumeru pamoja na kata 12 za
Wilaya ya Monduli. Michakato mingine inaendelea kukamilisha wilaya zilizobaki. Tuliahidi pia kuanzisha SACCOS ambayo aliyekuwa
Mbunge wa Arusha, Felix Mrema na Mbunge mwenzake, Elisa Mollel walituchangia
kiasi cha milioni moja kila mmoja. Lakini cha kushangaza hadi leo hazijulikani
zimeenda wapi. Binafsi nasubiri kikao kijacho cha vijana ili niweze kuuliza
vizuri. Kama kuna mtu kakaa nazo hizo fedha kwa manufaa yake binafsi lazima
arudishe na riba maana fedha hizo zilitolewa tangu mwaka 2009. Kwa ujumla
naamini kwa kiasi kikubwa nimekidhi matarajio ya ninaowaongoza.
Raia Mwema: Hivi
karibuni umetangaza nia ya kugombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki. Je,
nini hasa kilikusukuma hadi kutangaza nia hiyo?
Gambo: Kwa kweli nimesukumwa na
mambo mengi sana kufikia uamuzi huu. Kwanza nimefanya kazi na asasi za vijana
kwa zaidi ya miaka kumi. Nimepata fursa ya kuwakilisha vijana kwenye nchi
mbalimbali kwa masuala tofauti. Nakumbuka mwaka 2006 kupitia asasi iitwayo YUNA
niliwakilisha vijana wa Tanzania nchini Kenya, kwenye mkutano wa masuala ya
Afrika Mashariki na Kati, na malengo ya Millenia. Mwaka 2007 nilialikwa nchini
Zimbabwe kwenda kutoa mada kwenye mkutano wa masuala ya Amani na Migogoro
barani Afrika. Pia nimeshiriki kwenye majadiliano mbalimbali
yanayohusu masuala ya Afrika Mashariki. Nakumbuka wakati ule imeundwa Tume ya
Profesa Wangwe ya kuchukua maoni ya Watanzania kuhusu mchakato wa kuharakisha
kuwa na Shirikisho la Afrika Mashariki. Nilikutana kwenye kikao hicho na Mbunge Pindi
Chana, Mzee Joseph Butiku na Zitto Kabwe. Vijana maoni yetu yalikuwa wazi kuwa
hatupingi kuungana lakini kama nchi tunahitaji maandalizi ya kutosha ili watu
wetu waweze kunufaika na Shirikisho hilo. Tukasema nchi zilizoendelea mfano za
Ulaya, wao wametumia zaidi ya miaka kumi kukubaliana kuwa na sarafu ya
moja na bado hawakuweza kukubaliana nchi zote.Sasa kwa nini sisi tunataka kuchukua chini ya
miaka 15 kukamilisha hatua zote nne tena bila maandalizi? Yaani
tukamilishe ushuru wa forodha, soko la pamoja, sarafu moja na Shirikisho la
Afrika Mashariki kwa kipindi kifupi, kwa shinikizo la nani? Na haraka ya nini? Pia mwaka 2007, nilichaguliwa kuwa mwenyekiti wa
asasi ya vijana kwa nchi zote tano za Afrika Mashariki. Nchi za Tanzania,
Uganda Kenya, Rwanda na Burundi zote zilileta wawakilishi wao kwenye uchaguzi
uliofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa AICC Arusha. Nakumbuka
John Mnyika, Mbunge wa sasa wa Ubungo ndiye alikuwa mwandishi wa mkutano ule.
Tulimwomba afanye kazi hiyo kwa kuwa yeye alikuwa na uwezo na uzoefu mkubwa
kuandika ripoti za mikutano mikubwa.
Pia nimeshiriki kwenye mijadala mbalimbali ya
masuala ya Afrika Mashariki kwenye ushuru wa forodha na soko la pamoja katika
nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
Pamoja na hayo, niliwahi kuwa msaidizi wa Mbunge
wa Afrika Mashariki Dk. George Nangale. Nilifanya naye kazi kama mtafiti
msaidizi. Nilijifunza mengi sana kutoka kwa Dk. Nangale, wakati wote
alikuwa anapenda kufanya mambo ambayo mwishowe yanaleta matokeo chanya kwa
jamii. Nakumbuka namna alivyo kuwa anasukuma muswada wa “Transboundary and
Ecosystem”. Naambiwa sasa huo muswada uko kwenye hatua za
mwisho. Kwa ujumla utaona nimepata uzoefu wa kutosha kwenye mambo haya ya EAC. Lakini pia vijana ni zaidi ya asilimia 65 ya watu
wote wa Afrika, binafsi naamini kundi hili la vijana halijapata uwakilishi
mzuri. Wenzetu kule Rwanda wametenga nafasi moja kwa ajili ya vijana.
Nafikiri ni wazo jema kwa Tanzania Bara tukawa na nafasi moja kwa ajili ya
kundi la vijana. Pia kuna kitu wenzetu wazungu wanaita “succession
planning”. Nina amini kwamba tunapaswa tuanze kuwaunga mkono na
kuwainua viongozi vijana wenye uwezo ili kuanza kufanya hiyo Succession
Planning (maandalizi ya viongozi). Pamoja na hayo nataka kuwa sauti ya
wanyonge, sauti ya under – preveleged na si sauti ya wanasiasa pekee.
Kwa mantiki hiyo, nina amini kuwa nina kila sababu ya kuwania nafasi hiyo.
Raia Mwema: Waliojitokeza
kuwania nafasi ya ubunge wa Afrika Mashariki ni wengi mno, umejipanga kwa namna
gani kushiriki ili hatimaye ushinde?
Gambo: Jambo la kuvutia ni
kwamba, uchaguzi wa wabunge wa Afrika Mashariki wapiga kura wake ni wabunge
wetu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa imani yangu binafsi,
wabunge wetu hao ambao ni makini, huwezi kuwadanganya kwa njia yoyote kwani
wana uwezo mkubwa wa kupima uwezo, ari na dhamira ya kila mgombea kwa sababu
nao ni wazoefu katika masuala ya chaguzi zenye ushindani mkali na wengi ni wanataaluma
waliobobea katika masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Binafsi, naamini nina uwezo mkubwa wa kuwa mbunge
bora wa Afrika Mashariki bila kujali idadi ya wagombea wenzangu ni kubwa au
ndogo na msimamizi wangu katika mchakato huu ni Mwenyezi Mungu. Mungu hamwachi
mja wake.
Raia Mwema: Endapo
utafanikiwa kushinda ubunge wa Afrika Mashariki, nini vipaumbele vyako
kiutendaji kama mbunge?
Gambo: Jumuiya ya Afrika
Mashariki ni jumuiya yenye michakato mingi ya msingi. Pamoja
na mambo mengine, nitahakikisha vijana wa Tanzania na wananchi
kwa ujumla wanapata fursa ya kushiriki ipasavyo kwenye michakato
yote inayohusu Jumuiya hiyo ya Afrika Mashariki.
Kwa mfano ni Watanzania wachache sana ambao
wanajua kuwa katika ile hatua ya ushuru wa forodha ilitolewa miaka mitano kwa
nchi za Afrika Mashariki pamoja na Tanzania kupeleka bidhaa nchini Kenya bila
ushuru ili kutoa mwanya kwa nchi kama Tanzania kujipanga kutokana na tofauti
yake kiuchumi na Kenya.
Sasa wasli linalojitokeza ni je, Watanzania
wangapi walinufaika na fursa hiyo? Wabunge wetu wa wakati huo walifanya
juhudi za kutosha? Na je, Wizara ya Afrika Mashariki iliweka msukumo wa
kutosha?
Nakumbuka wenzetu wa Kenya walizindua mkakati wao
wa mawasiliano kwenye masuala ya EAC, mkakati huo waliuita “EAC Communication
Strategy”. Hapa kwetu sijawahi kusikia kitu kama hicho, inawezekana
kipo lakini bado binafsi sijasikia. Kwa hiyo, kipaumbele changu cha kwanza kitakuwa
ni kuhakikisha Watanzania wanapata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu mambo
yanavyokwenda pale EAC.
Binafsi nilifurahishwa na ziara ya mipakani ya
hivi karibuni ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
Nakumbuka alikwenda Namanga na Holili, kule alitatua changamoto nyingi ambazo
asingeweza kuzitatua akiwa kwenye kiti chake pale ofisini Jengo la Water Front,
Dar es Salaam.
Mambo kama matumizi ya kadi ya manjano mipakani
pamoja na kodi ya kichwa, ambayo yalikuwa kero kubwa aliyamaliza. Ni lazima
wizara na taasisi za Serikali ziwe sehemu ya kuwawezesha wananchi kufanya
shughuli zao kwa amani, ili mchakato wa kuelekea Shirikisho la EAC uwe wenye
tija.
Raia Mwema: Unadhani
tangu kurejeshwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki hadi sasa, jumuiya hiyo
imekidhi matarajio ya wananchi wa nchi husika?
Gambo: Nafikiri ni mapema sana
kujua kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki imekidhi matarajio au la. Ila kwa kuwa
wananchi hawashirikishwi kwa kiasi kikubwa kwenye michakato ya EAC, ni rahisi
sana kusema kuwa EAC haikidhi matarajio.
Mfano, mchakato wa ushuru wa forodha ulioanza
mwaka 2005 unaohusisha Soko la Pamoja, majadiliano yalikwishakusainiwa na
utekelezaji umeanza. Majadiliano kuhusu kuwa na sarafu ya pamoja yameanza
na ilitakiwa Desemba, mwaka huu tumalize mambo ya sarafu ya pamoja, isipokuwa
marais wetu bado hawajasaini Itifaki ya Sarafu ya Pamoja na inatarajiwa kwenye
kikao kijacho cha marais wa EAC, huenda wakasini itifaki hiyo.
Na ratiba ilikuwa inaonyesha mwakani, mwaka 2013
tuwe kwenye Shirikisho la Afrika Mashariki. Utaona kama kuna uharaka fulani
hapa. Kwa uharaka huu, huwezi kamwe kukidhi matarajio ya watu.
Raia Mwema: Nchi za EAC
zinasuasua katika utekelezaji wa mipango ya pamoja. Mambo gani unadhani
yafanyike ili kuondokana na hali hiyo?
Gambo: Kwa maoni yangu, namna
pekee kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kutekeleza mipango ya pamoja kwa
urahisi ni kuwa na Shirikisho la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kila nchi kufanya
mipango yake kipekee pekee nadhani inaongeza changamoto zaidi ndani ya Jumuiya.
Katika hili nitakupa mfano, angalia ile barabara
ya Afrika Mashariki ya Namanga. Kipande cha kutoka Namanga kwenda Kenya kiko
sawa sana na kwa ubora wa hali ya juu, lakini kutoka Namanga kuja Arusha
kiwango chake kinatia shaka mno. Hii ni changamoto kubwa kwa nchi yetu ya
Tanzania. Ni mradi mmoja unaohusika na barabara ya Namanga, Kenya na Namanga
Tanzania. Swali la kujiuliza ni kwa nini Namanga-Kenya kuwe bora zaidi kuliko
Namanga-Tanzania? Pengine mambo haya tungeyaangalia kwa pamoja yangekuwa
sawa zaidi.
Raia Mwema: Nini
tathmini yako kuhusu nafasi ya vijana kisiasa katika nchi za Afrika Mashariki?
Gambo: Kimsingi nafasi ya vijana
ni finyu sana katika nchi za Afrika Mashariki. Na hii inasababishwa na
kukosekana kwa chombo mahsusi cha kushughulika na masuala ya vijana pale
Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa kifupi, hatuna Baraza la Vijana la Afrika
Mashariki.
Nchi za Afrika Mashariki zimekubaliana kuwa na
Baraza la Vijana la Afrika Mashariki hadi kufikia Desemba, mwaka huu.
Hapa kuna jambo linashangaza kidogo, katika nchi
tano za Afrika Mashariki nchi za Rwanda, Uganda na Burundi tayari zina Baraza
la Vijana la Taifa katika kila nchi. Kenya wameshakamilisha michakato yote na
tayari wameshaunda bodi inayoshughulika na masuala ya vijana, wakati wowote
wanakwenda kwenye uchaguzi wa viongozi wa Baraza la Vijana la Taifa la
Kenya.
Hapa kwetu Tanzania mchakato wa kupata Baraza la
Vijana la Taifa ulipata kasi mwaka 1994. Lakini cha ajabu hadi leo tunafanya
kazi ya kujadili sera tu. Hii ni changamoto kubwa sana. Imefika wakati sasa
tuache siasa kwenye mambo ya msingi. Ni muhimu tukapata chombo cha vijana hapa
Tanzania na Afrika Mashariki. Chombo hiki muhimu kitawasaidia vijana kujadili
masuala mbalimbali yanayohusu mustakabali wa taifa lao na Jumuiya ya Afrika
Mashariki kwa ujumla.
Kwenye Baraza la Taifa la Vijana watu watajadili
nje ya itikadi za vyama vyao vya siasa. Mwaka 2011, nilikutana na Rais Paul
Kagame kule Ikulu ya Kigali, Rwanda. Rais Kagame alisema; “Unajua dunia ya leo
ni dunia ya vijana ndiyo maana mimi ukienda ofisi karibu zote utakuta vijana
wana madaraka makubwa na hiyo ni moja ya sababu ya Rwanda kuendelea kwa
kasi. Lakini lazima mkumbuke kuwa ujana ni namna akili yako inavyofanya kazi na
si umri maana kuna vijana wengine wanafikiri kama wazee na wazee wengine
wanafikiri zaidi ya vijana.”
Sasa kimsingi kukosekana kwa chombo hiki kuna
nifanya nitafsiri kuwa nafasi ya vijana ni finyu sana katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Raia Mwema: Waliojitokeza
kuwania nafasi hiyo wengi ni wenye umri wa zaidi ya miaka 65. Wewe ni mdogo
kiumri kwao na hata kisiasa kwa baadhi ya washindani wako. Umejipanga vipi?
Gambo: Kama utakumbuka mwanzo
kabisa wanaume tuliochukua fomu kwa ajili ya kuomba kupitishwa na chama chetu
ili kugombea ubunge wa Afrika Mashariki tulikuwa 45. Tukachujwa na Kamati Kuu
ya CCM tukabaki 18. April 3, 2011, tulipigiwa kura ya maoni na wabunge wa CCM
na kubaki tisa, ambao tutakwenda kuomba ridhaa ya wabunge wote, bungeni Dodoma
April 17, 2011.
Inawezekana Gambo ni mtu makini hapendi uzembe. Hata hivyo namshauri kuwa na busara na asiogope kuchukuwa hatua zinazostahili kwa watumishi wazembe badala ya kuwatukana.
ReplyDelete