Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete leo, Alhamisi, Septemba 20, 2012, ameweka Jiwe la Msingi
la ujenzi wa Daraja la Kigamboni, Dar es Salaam kwa kuwaonya watu ambao
amewaeleza kuwa wanavyo viwanda vya kutunga uongo kuacha tabia hiyo na
kuelekeza nguvu kwenye maendeleo.
Aidha, Rais Kikwete amewahakikishia wakazi wote wa
Kigamboni ambao wanaondolewa katika maeneo yao kwa ajili ya kupisha ujenzi wa
daraja hilo na ujenzi wa Mji Mpya wa Kigamboni kuwa watalipwa stahili na haki
zao zote.
Daraja hilo la Kigamboni ambalo wazo la kujengwa kwake
lilibuniwa kwa mara ya kwanza zaidi ya miaka 30, tokea mwaka 1978, wakati wa
uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, linajengwa kwa gharama ya Sh.
bilioni 214.6 na litakuwa tayari katika muda wa miezi 36 ijayo, ingawa muda huo
unaweza kupungua na kubakia miezi 30.
Daraja hilo ambalo litakuwa na urefu wa mita 680
linagharimiwa kwa pamoja na Serikali na Shirika la Hifadhi ya Jamii la NSSF
ambalo litachangia kiasi cha asilimia 60 na Serikali asilimia 40. Daraja hilo ambalo litakuwa na jumla ya barabara za
kupitisha magari sita kwa wakati mmoja linajengwa na makampuni mawili ya China
ambayo ni China Railway Construction Engineering Group na China Railway Major
Bridge Engineering Company na mhandisi msimamizi wa ujenzi huo ni Kampuni ya
Misri.
Daraja hilo litapunguza adha ya usafiri kati ya
Kigamboni na Dar es Salaam ambao kwa sasa unategemea vivuko, ama boti ndogo,
mitumbwi ama wenye magari kulazimika kufanya mzungumo wa kilomita 52. Kwa
uamuzi wa sasa, wavuka kwa miguu ambao watakuwa na njia maalum kwenye daraja
hilo pamoja na waendesha baiskeli watavuka bure bila malipo yoyote.
Akizungumza kwenye sherehe hiyo, Rais Kikwete amesema
kuwa Serikali haiwezi kudhulumu wananchi wake na hivyo watu wote ambao
wanastahili fidia kutokana na ujenzi wa daraja hilo na mji mpya wa Kigamboni
watalipwa haki na stahiki zao.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake
haitaruhusu mtu yoyote kuzuia ama kuchelewesha miradi ya maendeleo ambayo
inalenga kunufaisha watu wengi.Rais Kikwete pia amewaonya watu ambao wamelifanya
suala la kutunga na kusema uongo kama sehemu ya utamaduni wao. “Watu wana
viwanda vya kuzalisha uongo. Wanashinda wanasambaza uongo kwenye mitandao, kila
mahali. Wamepata hata kusema kuwa mimi nimemuuzia George Bush eneo la Kigamboni.
Bush aje kufanya nini Kigamboni?”
Rais pia amesema kuwa wapo watu ambao hawapendi
maendeleo ya nchi. “Wanatamani kila siku tushindwe kuwaletea wananchi maendeleo.
Lakini watakufa kwa kihoro kwa sababu hatutashindwa. Kila tulilosema
tutalifanya, litafanyika”.
Amesema kuwa thamani kubwa ya vyama vya siasa ni
maendeleo ya wananchi. “Lakini wapo wenzetu ambao wanaudhika wakiona maendeleo. Wanapenda
hata daraja hili lisijengwe. Leo hawatalala usingizi. Kazi ya vyama vya siasa
ni kuweka maslahi yetu sote mbele.”
Imetolewa
na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar
es Salaam.
20
Septemba, 2012
No comments:
Post a Comment