Watu
10 wamekufa papo hapo na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa akiwemo Mbunge wa viti
maalum Mkoa wa Mbeya, Mheshimiwa Mary Mwanjelwa baada ya lori la
mafuta kufeli breki wakati likitelemka mlima wa Iwambi Mji wa Mbalizi na
kuyagonga magari matatu ambapo kati ya hayo magari mawili yaliteketea kwa moto
. Imeelezwa
kuwa ndani ya gari la Mbunge huyo kulikuwepo na watu wawili dereva wa gari hilo
aliyejeruhiwa miguuni na kichwani huku mwanamke mmoja anayesadikiwa
kuwa ni Katibu wa Mbunge huyo ambaye inadaiwa ameteketea kwa moto
na kubaki mifupa na majivu.
Ajali
hiyo ilitokea jana majira ya saa nane za mchana katika eneo la Mteremko
wa Iwambia mbapo Lori hilo la mafuta likiwa na namba T81 4BTC na tela lenye
namba T815 BT linadaiwa kufeli breki na kuyagonga magari matatu likiwemo gari
la Mbunge huyo. Mkuu
wa mkoa wa Mbeya, Abass Kandoro, akizungumza na waandishi kwenye eneo la tukio
alisema ajali hiyo imesababishwa na magari manne ambapo kati yao matatu
yameteketea kwa moto papo hapo likiwemo gari la Mbunge Toyota Hilux.
Alisema,
gari lingine lililoteketea moto ni gari ndogo ya abiria Toyota Hiace
yenye namba T587 AHT ambalo lilikuwa na watu kumi ambao kati yao wapo
waliofariki na kujeruhiwana lori lenyewe la mafuta limeteketea kwa moto. Akizungumzia
tukio hilo kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani alisema baadhi
ya majeruhi wa ajali hiyo ni Mbunge Mary Mwanjelwa ambaye anaendelea kupatiwa
matibabu katika hospitali ya Teule ya Ifisi baada ya kuumia kwenye kiuno na
dereva wake ambaye ameumia miguu na kupata majeraha kichwani.
Majeruhi
wengine wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali Teule ya Ifisi na
wengine hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya na kwamba hali ya Mbunge inaendelea
vizuri. Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo ambao walisema kuwa Lori hilo la
mafuta lilikuwa likishusha mlima huo wa Iwambi, huku mbele yake kukiwa na Lori
lingine la mizigo mbapo dereva wa gari hiyo alifanikiwa kulipisha Lori hilo na
ndipo lilipoyagonga magari hayo mawili ambayo mbali na kupinduka kandokando ya
barabara pia yaliteketea kwa moto.
“Lori
la mafuta lilikuwa katika mwendokasi na ndipo lilipoligonga lory lingine la
mizigo na kisha kwenda kuyagonga magari madogo mawili na kusababisha
ajali hiyo kutokea,”alisema Alisi Mwakisapi.
Alisema,
Mbunge wa viti maalumu aliokolewa na bodaboda iliyokuwa karibu na eneo hilo kwa
kile alichokidai kuwa mara baada ya kufanikiwa kutoka ndani ya gari hilo dereva
huyo alimuona na kumchukua kwenye bodaboda na kumuwahisha hospitali. “Katika
gari la Mheshimiwa Mwanjelwa alikuwemo dereva na mwanamke mmoja ambaye anadaiwa
kuteketea kwa moto na kubakia majivu,”alisema
Hata hivyo, miili ya
marehemu tisa imehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Mbeya na
hospitali Teule ya Ifisi majina yao hayajatambuliwa na kwamba mwili wa
mwanamke mmoja ambaye alikuwa kwenye gari ya Mbunge uliteketea kwa
moto kabisa.
No comments:
Post a Comment