Hivi karibuni Waziri wa Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi Prof.
Anna Tibaijuka na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira)
Dkt. Terezya Huvisa walitoa tamko kwamba nyumba zote zilizojengwa kando
kando ya fukwe za bahari na mito zitabomolewa, bila wamiliki kulipwa
fidia kutokana na kukiuka Sheria za Ardhi na Mazingira za mwaka 1992,
1995 na 2004. Kauli hiyo ilitokana na ukweli kwamba imekuwa ni jambo la
kawaida kwa watu wenye nguvu ya fedha kuharibu mazingira kwa makusudi
pasipo kujali athari ambazo zinaweza kutokea sasa na baadae kwa wakazi
wa maeneo husika, jamii inayowazunguka na taifa kwa ujumla!
Kwa watu wengi, kauli ya mawaziri hao ilionekana kama ni hatua muhimu
sana katika kulinda mazingira ya fukwe zetu na jamii nzima hasa
kutokana na umuhimu wa kulinda mazingira katika wakati huu wa athari za
mabadiliko ya tabianchi. Lakini baadhi yetu tuliona kama ni mwendelezo
wa kauli za Serikali ambazo utekelezaji wake ama huwa ni wa mashaka au
ukitekelezwa basi utekelezaji wake hutawaliwa na upendeleo wa hali ya
juu kwa watu wenye fedha na nafasi kubwa serikalini (vigogo). Moja kati
ya nyumba iliyotakiwa kubomolewa imejengwa kwenye viwanja namba
2019-2020 Kawe Beach, katika fukwe za Bahari ya Hindi. Viwanja ambavyo
vilipatikana kwa ushirikiano wa Mchungaji Lwakatare na tapeli maarufu wa
Ardhi jijini Dar es salaam, anayejulikana kwa jina la Frank Mushi.
Ikumbukwe kwamba katikati ya mwezi Julai, 2012 wananchi waliojenga
nyumba katika maeneo yanayosemekana ni tengefu ya Jangwani Beach, Mto
Ndumbwi na Mto Mbezi walivunjiwa nyumba katika operesheni iliyoendeshwa
na Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC). Operesheni ambayo ilihusisha
takriban nyumba 15 na kuta ( fences) 8. Katika nyumba hizo, mojawapo
iliyotakiwa kuvunjwa ni ya Mchungaji Getruda Lwakatare. Lakini kwa
sababu ambazo wahusika, akiwemo yeye mwenyewe na serikali, wanazifahamu,
nyumba yake haikuguswa! Wakati wananchi wanaofahamu ukweli wa mambo,
wakiwa bado wanahoji chinichini juu ya upendeleo wa kitabaka ulio wazi,
hivi karibuni wameshuhudia kupitia njia mbalimbali za upashanaji habari,
ikiripotiwa kuwa Mchungaji Lwakatare (Mchungaji wa Kanisa la Assemblies
of God na Mbunge wa Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ) amehamia
kwenye nyumba yake mpya.
Nyumba ambayo ilipaswa kuwa imebomolewa kwa sababu imejengwa kwenye
viwanja ambavyo ni kinyume cha sheria kujenga katika maeneo hayo.
Kuvunja sheria kwa uwazi namna hii, huku wengine wakichukuliwa hatua kwa
kuvunja sheria hiyo hiyo, si tu ni ’double standards’, bali kunaweza
kutafsiriwa ni kuitia serikali mfukoni. Kitu kibaya zaidi ni kwamba
kiongozi huyo alishataarifiwa tangu mapema juu ya ubatili wa kujenga
katika eneo hilo, kupitia kwa huyo Frank Mushi kabla hata ujenzi wa
nyumba hiyo haujaanza. Ikumbukwe pia kuwa viwanja hivyo vilipatikana na
ujenzi huo kuwezekana baada ya eneo la bahari na mto kujazwa kifusi na
mawe! Kwa kutambua kuwa kuendelea na ujenzi katika eneo hilo ni kuvunja
sheria za nchi zinazohusu utunzaji wa mazingira kwa manufaa ya jamii
nzima, Mchungaji Lwakatare aliendelea kwa kujiificha nyuma ya mgongo wa
huyo Mushi, akijifanya hahusiki kabisa na kilichokuwa kikiendelea katika
eneo husika.
Uthibitisho wa ubatili wa kujenga katika viwanja husika: 1) Tarehe
4/1/2011 Wizara ya Ardhi kupitia barua yenye Kum. Namba LD/297571/18
waliandika barua kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni
kuhusiana na uvamizi wa kiwanja nana 2019 na 2020 Mbezi Kawe. Barua
husika pamoja na mambo mengine ilibainisha kwamba wizara imefanya
ukaguzi katika viwanja tajwa, baada ya kupata malalamiko juu ya
uharibifu wa mazingira unaoendelea katika eneo hilo. Na kwamba ukaguzi
walioufanya umeonesha kuwa ujenzi unaofanyika katika eneo husika
hauruhusiwi na unakiuka Tangazo la Serikali (GN) No. 76 ya mwaka 1992.
Kupitia barua hiyo, wizara ilimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri kuchukua
hatua za kubomoa/kuondoa uendelezaji batili uliokuwa ukifanyika katika
viwanja Na 2019 na 2020 Mbezi Kawe. Barua hiyo ilisainiwa na Bwana
Sadoth K. Kyaruzi, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara. 2) Uthibitisho
mwingine ni barua ya tarehe 30/9/2011 kutoka NEMC kwenda kwa Bwana Frank
Mushi. Barua husika, ilitoa maelekezo kwa Mushi kuvirudisha katika hali
yake ya kawaida, viwanja namba 2019-2020 kwa mujibu wa vifungu 55(2)
(a) (e), (3) na 151 (1) ,(2) (a), (b), (3) ,(4) (b) na (f) vya Sheria ya
Mazingira, sura 191 ya mwaka 2004. Barua husika inabainisha kwamba timu
ya wataalam toka Baraza la Mazingira (NEMC), Wizara ya Maji, Wizara ya
Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam na Manispaa ya Kinondoni
ilitembelea eneo husika kufuatia malalamiko kutoka kwa viongozi na
wakazi wa Kawe Beach. Timu hiyo ilibaini kwamba eneo la Mto Ndumbwi,
pamoja na bahari lilikuwa linajazwa mawe na vifusi hali iliyosababisha
kupatikana kwa viwanja na 2019 na 2020. Ambapo ndani ya viwanja hivyo
lilikuwa linajengwa jumba kubwa kinyume kabisa na vifungu 55(2)(a) ,
55(2) (b) , 55(2)(d) na 55(2)(e) vya Sheria ya Mazingira. Ilibainika pia
kuwa mikoko ilikatwa kinyume na s.63(1) ya Sheria ya Mazingira. Kwa
mujibu wa nyaraka nilizonazo, yafuatayo yalijitokeza i) Timu ya wataalam
ilibaini kwamba, tayari Wizara ya Maliasili na Utalii ilishatoa zuio la
ujenzi katika eneo husika. ii) Manispaa ya Kinondoni, mara kadhaa
iliweka zuio la uendelezaji na kutoa amri kwa ’mmiliki’ wa eneo husika
kubomoa, lakini mmiliki huyo alipuuza amri hiyo na kuendelea na ujenzi!
iii) Ilitolewa amri ya Mahakama, tarehe 5/4/2011 kumtaka Bwana Mushi
asiendelee na ujenzi. Amri hiyo ilipuuzwa na ujenzi ukaendelea. Baraza
la Mazingira lilimwagiza tena, Bwana Mushi:-
2) Kuvunja majengo yote yaliyoko kwenye viwanja vyenye mgogoro.
3) Ndani ya siku saba, tokea amri husika kutolewa (amri ilitolewa
30/9/2011) awe ametoa mawe na vifusi vyote vilivyoharibu mkondo wa maji
na bahari na kuurudisha mto na bahari katika hali yake ya kawaida.
4) Ndani ya siku 30 chini ya usimamizi wa Wizara ya Maliasili na
Utalii kuhakikisha kwamba mikoko yote iliyokatwa imerudishwa katika hali
iliyokuwa awali. Kwa gharama za Bwana Mushi. Licha ya amri zote hizo,
mazuio yote hayo, matamko ya mawaziri yaliyotawaliwa na mbwembwe nyingi,
ujenzi uliendelea, nyumba imekamilika. Sasa inatumika. Wakati kigogo
huyo amehamia kwenye nyumba yake kwa matangazo na mbwembwe, Mto Ndumbwi,
bahari na mazingira kwa ujumla yameharibiwa vibaya! Bila kusahau kuwa
wananchi wengine wamebomolewa nyumba zao kwa kutumia sheria hizo hizo.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira, Sura 191 ya mwaka 2004, Fungu 57(1)
hairuhusiwi kufanya shughuli zozote za kudumu za kibinadamu ndani ya
mita 60 ambazo kwa asili yake zinaweza kuhatarisha au kuathiri vibaya
ulinzi na utunzaji wa mazingira, utunzaji wa bahari, kingo za mto, bwawa
au mwambao wa asili wa ziwa. Halikadhalika, Sheria ya Ardhi Na. 4 ya
mwaka 1999 ( Sura 113) Fungu 7 (1) (d) inabainisha kwamba eneo lolote
lililo ndani ya mita 60 kutoka kingo ya mto na bahari linatakiwa
kutangazwa kama ardhi hatari au kuhifadhiwa. Na pale inapotokea kuwa
masharti ya sheria moja yanapingana na masharti ya Sheria ya Mazingira,
kuhusu mambo yanayohusu usimamizi wa mazingira, Sheria ya Mazingira
ndiyo hutumika, kwa mujibu wa Fungu 232 la sheria ya mazingira sura
Kutokana na hali hii serikali inatakiwa kujinasua katika mwendelezo wa
tafsiri wanayoipata wananchi kuwa imetekwa na kuwekwa mfukoni na watu
wachache wenye uwezo.
Maana wanaona kuwa huu ni mwendelezo wa serikali kuwa na kigugumizi
pale sheria zinapovunjwa na vigogo serikalini au watu wenye fedha
wanaoshirikiana na baadhi ya viongozi wa serikali na chama tawala
kufanya ufisadi. Wameona mambo ya namna hii mara kadhaa, ikiwemo
serikali kushindwa kuwachukulia hatua waliohusika na kashfa kubwa za
ufisadi kama ’akina’ Kagoda na wenzake (EPA), Richmond na kashfa
nyingine nyingi. Kwamba sasa inazidi kuonekana dhahiri kuwa kuna watu
wako juu ya sheria za nchi, huku wanyonge wakishughulikiwa.
Halima Mdee (MB)
Waziri Kivuli, Wizara ya Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi
No comments:
Post a Comment