Na:
Florence Majani,MWANANCHI
KWA
wakazi wa Dar es Salaam, mawingu yanapotanda angani na kutengeneza giza ambalo
huashiria mvua, kwao huwa ni jambo la kawaida na pengine ni ahueni kwa karaha
za joto kali. Lakini kwa wakazi wa mkoa wa Rukwa hasa Sumbawanga, dalili ya
mvua inayoambatana na radi ni tishio la umauti kwani mara nyingi radi hizi si
za kawaida au za asili bali ni za kichawi na hutengenezwa na wanadamu kwa
madhumuni ya kuua.
Mkoa
wa Rukwa hususani wilaya ya Sumbawanga, ni eneo linalosifika kwa imani za
kishirikina nchini. Lakini katika masuala ya utaalamu wa radi, yapo maeneo na
watu maalum ambao wana uwezo wa kutengeneza radi. Ukiwa unatokea wilaya ya
Sumbawanga kuelekea wilaya ya Nkasi, ndipo vilipo vijiji maarufu kwa kutengeneza
radi hizo.
Baadhi
ya vijiji hivyo ni Sintale na Chipu, ambako ndiko walipo wataalamu wenye uwezo
na nguvu za ziada za kutengeneza radi. Kwa nini radi zinatengenezwa? Radi hizi
zinatengenezwa kwa ajili ya kuua au kuwajeruhi maadui. Kwa mfano, kama yupo
aliyekudhulumu, aliyekuibia mke au mume, aliyekugonga na gari bila kukulipia
gharama za matibabu au anayekutusi na kukukebehi. Vijiji vya Sintale, Chipu na
Kalundi, vimepakana, kinaanza kijiji cha Kalundi kisha Sintale na cha mwisho ni
Chipu. Vijiji hivyo viko duni kimaendeleo na ukubwa.
Hata
hivyo huku ndipo walipo watalaamu na mafundi wa kuunda radi. Nilipokuwa mkoani
humo hivi karibuni na mwenyeji wangu, tulielekezwa na wenyeji wa Kalundi kwa
mganga wa kwanza nayeitwa Mashaka ambaye anaaminiwa kwa kuunda radi. Baada ya
kufika kwa Mashaka, tunamkuta akiwa na wateja kadhaa. Ninamweleza shida yangu
na kumtonya kuwa ni shida ya kipekee kidogo. Namweleza kuwa nahitaji kununua
radi kwani nina adui yangu aliyenidhulumu fedha nyingi. Mashaka anajibu kuwa
yeye si mtaalamu wa radi bali anatibu maradhi tu.
Anasema:
“Lakini yupo mtaalamu wa radi, anaitwa mzee Chimwaga, anaishi kijiji cha
Sintale. Ngoja nimpigie simu sasa hivi,” Mganga huyu anazungumza kwenye simu
kwa lugha ya kifipa, na baada ya dakika chache anakata simu na kutugeukia na
kusema: “Yupo- nendeni- kutoka hapa kwenda Sintale kwa Honda ni dakika 20,
mkimuuliza yeyote, atawapeleka kwa mzee huyo,” Kwa kuhofia muda, hatukwenda kwa
mganga Mzee Chimwaga, na badala yake tunakwenda eneo jingine na kuuliza iwapo
kuna mganga mwingine mwenye utaalamu wa radi. Mzee mmoja anatuelekeza kuwa yupo
mganga anayeitwa Ntoro, mwenyeji wa hapo hapo Kalundi ambaye naye ni mtaalamu
wa radi.
Tunaelekezwa
kwa mganga Ntoro, tunapofika tunamkuta akiwa na wake zake wawili na watoto
wasiopungua wanane. Anatukaribisha na tunamweleza shida yetu. Mganga Ntoro
anasema, yeye hutengeneza radi lakini kwa wakati ule alikuwa kaishiwa vifaa,
hivyo aliamua kumpigia simu mganga mwenzake mwenyeji wa kijiji cha Sintale
ambaye ana ujuzi huo pia.
Anashika
simu, na kumpigia mganga huyo tuliyebaini kuwa anaitwa Maisha, huku
akimsisitizia afike haraka azungumze na wateja. Wakati tukimsubiri Mganga
Maisha afike, tulianza kumdodosa Mganga Ntoro kuhusu utaalamu huo wa kuunda
radi. Ntoro anasema, kwa kawaida huduma ya radi huuzwa, au hutozwa gharama kwa
bei ya kuanzia Sh40,000 hadi 30,000 tu na hiyo ni kulingana na umbali wa eneo
alipo mtu anayetakiwa kuuwawa na aina ya radi.
“Kwa
mfano watu wanaotoka Zambia au Kongo tunawachaji fedha nyingi zaidi kwa sababu
ya umbali, lakini kwa maeneo ya karibu bei ni nafuu kidogo,” anasema Ntoro.
Radi hutengenezwaje? Ntoro anasema, kwa kabila la kifipa, utaalam wa kuunda
radi huitwa ‘Namasata’. Radi hutengenezwa kichawi, lakini mtu yeyote anaweza kufundishwa
na kuweza kuitengeneza, ili mradi afuate masharti. Anasema zipo radi za aina
tatu, ya kwanza ni ya maji, ya pili ni ya pembe, na ya tatu ni ya gome la mti.
Zote hizo hutengenezwa kulingana na umbali na ubora wake.
“Radi
ya pembe ni ya hatari zaidi, huchoma na kuweza kutekeza watu na mali, na huenda
umbali mrefu tofauti na radi ya gome la miti,” anasema Huku tukiendelea
kumdadisi, mganga Ntoro anasema, radi ya maji hutengenezwa kwa kuchukua sahani
mpya, bakuli mpya au chupa ya udongo. Kisha mtaalamu huweka dawa ndani ya chupa
au bakuli na kuisemea maneno fulani.
“Ukishanuiza,
unaviweka vifaa hivyo ndani, kesho asubuhi utakuta maji ndani ya chupa au kama
uliweka bakuli basi utaona maji ndani ya bakuli,” anasema na kuongeza, “Baada
ya hapo unachukua vifaa vile na kuanza kunuiza adhabu unayotaka impate mbaya
wako, kwa kumtaja jina. Kama huna jina basi uwe na nyayo zake, nguo au kitu
chake chochote kile.”
Anasema
baada ya kunuiza, unachukua bakuli au chupa ikiwa juu ya sahani na kuyarusha
maji yale juu, kwa nguvu za kichawi, maji yale hupotea lakini kama kutakuwa na
kasoro yeyote, maji yale humrudia aliyeyarusha. Endapo mtaalamu atairusha radi
ile kwa mtu asiye na makosa, basi maji yatarudi chini na kama kweli mtu yule
amefanya kosa, basi maji hayatarudi na yatakwenda angani na kuanza kutengeneza
wingu jeusi linaloambatana na ngurumo.
“Maji
yakisharushwa juu, baada ya saa moja tu, utaanza kuona angani kiwingu cheusi na
kizito sana, mvua inaweza kunyesha kidogo na kisha ngurumo za kutisha … basi
hapo ujue kazi tayari na mbaya wako kashamalizwa,” anasema na kuongeza: “Kama
unairusha radi kwa mtu asiye na makosa kabisa, au ukakosea masharti radi
inaweza kukurudia na kukuunguza wewe.
Mtu
akiniudhi mimi huwa nazirusha tu,” Radi ya pembe hutengenezwaje? Wakati
tukiendelea kumsubiri mganga Maisha, kutoka Chipu, Mganga Ntoro anaendelea
kutupa utaalamu huo bila kujua kuwa alikuwa akichunguzwa. Sasa anasimulia namna
ya kutengeneza radi ya pembe. Anasema, radi hii hutengenezwa kwa pembe ya mbuzi
au kondoo, ambayo kwa kawaida huwa na uwazi katikati.
‘Tunachukua
pembe, tunaweka dawa ndani yake, (yaani kwenye uwazi) tunafunga hirizi
kuizunguka pembe, pamoja na shanga, kisha tunanuiza maneno kadhaa ya kichawi,
na kisha tunairusha kuelekea alipo mlengwa,” anasema Radi hii ni kama kimondo,
inaporushwa, hupaa angani na hufuka moshi katika upande wa mbele wa pembe wenye
uwazi kama zifanyavyo ndege za kushambulia(rocket). Mganga Ntoro anasema, radi
hii huweza kupaa umbali mrefu na huweza kuharibu mali, mifugo na binadamu
ambaye anawindwa.
Kuhusu
namna ya kutengenez radi ya gome la mti, Ntoro anasema hiyo ina masharti makali
ambayo si rahisi kuzitoa siri zake kwa kila mtu. Hata hivyo, baada ya muda
mfupi, mganga Maisha anapiga simu na kusema kuwa ameshindwa kufika kwa sababu
ametingwa na shughuli za mazishi na kutaka twende siku inayofuata asubuhi na
mapema.
Mkazi
mwingine wa kijiji hicho, David Ntare anasema mauaji ya radi ni jambo la muda
mrefu mahali hapo kwani wanaotumia uchawi wa radi wamekuwa wakijigamba mitaani
kwa uweza wao huo. “Tangu nazaliwa nasikia vifo vya radi na nina uhakika si
radi za kawaida kwa sababu, wanaokufa mara nyingi huwa na uhasama na mtu, kama
kumuibia mke,mume, kuiba au kutukana,” anasema Ntare.
Ntare
analihusisha tukio la kuungua kwa benki ya NMB, wilayani Nkasi, tarafa ya
Namanyere lililotokea miaka ya nyuma na uchawi wa radi. “Ile benki iliunguzwa
na radi na mzee mmoja mkulima wa kijiji cha Kizi baada ya aliibiwa hela nyingi
katika akaunti yake, akaona alipe kisasi kwa njia ile. Ile benki iliungua wa
radi, hakuna asiyejua,” anasema Inadaiwa kuwa wenyeji wa hapa aghalabu huviona
vitu hivi na hujua madhumuni yake na mara nyingi vifo vya aina hii hutokea
wilayani Sumbawanga. Anasema, kwa kawaida mtu aliyeungua kwa radi huwa kama
aliyeungua kwa umeme.
“Huungua
na kuwa weusi kama mkaa, na wakati mwingine radi hukataa kumuua mtu akiwa
ndani, bali humrusha nje na kumchoma huko ili isiwadhuru watu wengine,”
anasema. Mwalimu wa shule ya msingi Chalantala, Abeid Kisanga, anasema siku
moja akiwafundisha wanafunzi wa darasa la tatu somo la sayansi kuhusu radi ,
mwanafunzi wa kiume alinyoosha kidole na kusema ‘mimi najua kutengeneza radi,
baba kanifundisha,”
Anjelo
Singo, Afisa wa Polisi tarafa ya Namanyere anasema suala la ushirikina wilaya
ya Sumbawanga na Nkasi ni kubwa na yamekuwapo matukio kadhaa ya vifo
vinavyodaiwa kusababishwa na imani hizo. “Ingawa serikali haiamini uchawi,
lakini matukio ya radi yanayotokea hapa mengi ni ya kishirikina, au matukio ya
watu kuuwawa na kukatwa sehemu za siri vilevile ni ya kishirikina,” anasema
Anasema ni ukweli usiopingika kuwa uchawi umesheheni katika maeneo haya na
wakazi wake wameshaathirika kisaiolojia kuhusu hilo.
Mkuu
wa mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya anasema ameshawahi kusikia taarifa
za kuwepo kwa wataalamu wa kuunda radi lakini akasema hata hivyo hana uhakika
nazo. “Unajua jiografia ya mkoa wa Rukwa imekaa katika nyanda za juu, ni rahisi
radi kulipuka maeneo haya. Hata hivyo hili suala ni la kiimani zaidi,” anasema
pamoja na mambo mengi yanayosemwa kuhusu mkoa huo, kwa sasa maendeleo
yanakwenda kwa kasi na anaamini miaka michache ijayo, imani za ushirikina
zitapungua kama sio kwisha kabisa.
No comments:
Post a Comment