Rodrick Minja, Dodoma
RIPOTI ya Bunge kuhusu tuhuma za wabunge wa Kamati ya Nishati na
Madini waliotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa, inatarajia kuwasilishwa
bunge wiki Ijayo. Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Job Ndugai aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Spika wa Bunge
Anne Makinda atatoa utaratibu wa namna ya kuwasilisha ripoti hiyo ndani ya
ukumbi wa bunge.
Hata hivyo, Mheshimiwa Naibu Spika Job Ndugai alisema kuwa kwa mujibu
wa Kanuni za bunge toleo la 2007, vifungu 114(17), na 119 (1) hadi (6) kwa
pamoja vinampa madaraka spika kuhusu utaratibu wa kufuata katika uwasilishaji
wa taarifa bungeni. “Ambapo, yaweza kuwa spika akatoa uamuzi ama kamati
kuwasilisha taarifa hiyo bungeni au vinginevyo lakini spika atatoa taarifa ya
kukamilika kwa uchunguzi huo bungeni wakati wa mkutano wa tisa wa bunge
unaotarajia kuanza oktoba 30 mwaka huu,”. Katika mkutano wa nane wa bunge
lililopita, Spika wa bunge Anne Makinda aliunda kamati ya kuchunguza tuhuma za
wabunge wa Kamati ya Nishati na Madini kuhusu kujihusisha na vitendo vya
rushwa. Makinda alifikia uamuzi huo kufuatia tuhuma zilizokuwa zimezagaa karibu
nchi nzima kuwa wabunge hao wamekuwa wakijihusisha na rushwa lakini wakiwa
bungeni Mbunge wa Nkasi Ali Keissy Mohamed ndiye aliyeanzisha chokochoko hizo
kabla ya wabunge wengine kuidandia ajenda hiyo.
Kamati iliyoundwa na spika ilikuwa chini ya Mbunge wa Mlalo Hassan
Ngwilizi ambaye alisaidiwa na wajumbe Said Said Arfi (Mpanda Kati), John
Chiligati (Manyoni Mashariki),Godbless Blandes (Karagwe) pamoja na Mbunge wea
Viti Maalumu Ridhiki Juma.
Kwa mujibu wa Ndugai, Kamati hiyo ilimaliza kazi yake na
kuiwasilisha kwa spika tangu Septemba 20 mwaka huu ambapo ndiyo siku
ilipokabidhiwa kwa spika. Kwa upande
mwingine Naibu spika alikemea vitendo vya baadhi ya watu na vyombo vya habari
kuendelea kuandika na kuchapisha juu ya kilichomo ndani ya ripoti hiyo kwa
maelezo kuwa ni kosa.
“Kitendo cha kuchambua na kuchapisha maudhui ya taarifa hiyo katika
vyombo vya habari ni kinyume cha sheria na kinaingilia uhuru, haki na madaraka
ya Bunge kwa mujibu wa kifungu cha 31 (1) (g) cha sheria ya haki, kinga na
madaraka ya bunge sura 296,” Ndugai alifafanua kuwa kifungu hicho kinakataa mtu
yeyote kuchambua taarifa ya kamati kabla ya taarifa hiyo kuwasilishwa bungeni.
Naibu Spika alieleza kuwa ikibainika kuwa taarifa imechapishwa
wahusika wanaweza kulipa faini isiyozidi Sh 500,000 au kifungo kisichozidi
miaka mitatu au vyote kwa pamoja.
No comments:
Post a Comment