Katika mazingira ya kutatanisha aliyekuwa
Mfanyabiasahara maarufu mjini Iringa Ndugu. Makosa ametangaza kujinyonga katika
tukio atakalolifanya hadharani. Kwanini anataka kulifanya tukio hili
hadharani? Hili ni swali ambalo kila mtu anaweza kujiuliza lakini jibu lake
anataka iwe hivyo kwa kuwa atajinyonga katika tukio ambalo mashuhuda
watalazimika kulipa kiingilio.
Kwanini anataka kufanya tukio hilo kwa
kiingilio? Kila mtu anaweza kujiuliza swali hili. Katika majibu yake MAKOSA
anasema amefikia uamuzi huo ili zikusanywe fedha zikazosaidia kuendesha familia
yake, watoto yatima na sehemu kuchonga madawati kwa shule zenye upungufu wa
madawati mjini Iringa. Alipoulizwa kama ana ufahamu wa sheria na kwamba
kujaribu au kufanya hivyo ni kosa la jinai, katika majibu yake anasema litakuwa
kosa la jinai mpaka pale atakapofanya hivyo na kwa kuwa atakufa hana cha kuhofia.
MAKOSA ni nani? Kwa wakazi wa mjini
Iringa MAKOSA ni mtu maarufu sana, alifahamika zaidi kwa biashara zake nyingi
alizoanza kuzifanya mwanzoni mwa miaka ya tisini baada ya kuacha shughuli yake
ya ubaharia. Wakati akifika mjini Iringa, MAKOSA akiwa na itikadi za rasta,
alikuwa hanywi pombe, mnyenyekevu na alijikita katika kuisaidia jamii ya watu
wa Iringa kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti. Miti ya aina mbalimbali
inayonekana mjini Iringa, sehemu yake kubwa ilipandwa na MAKOSA. Hata hivyo pamoja
na kuupendezesha mji kwa miti hiyo, historia ya MAKOSA katika uhifadhi wa
mazingira ni kama vile imesahaulika kwasababu hakuna anayemuenzi kwa kazi kubwa
aliyoifanya.
Pamoja na harakati hizo MAKOSA ndio
mtu wa kwanza mjini Iringa kuingiza magari aina ya Coaster zilizokuwa zikifanya
kazi ya kusafirisha abiria katika maeneo mbalimbali ya mjini Iringa. Pamoja na
biashara ya usafirishaji, MAKOSA alikuwa anaendesha biashara ya hoteli. Kabla
ya kuanza kuendeshwa na MAKOSA, hoteli hiyo ilikuwa ikijulikana kama Cats Hotel
(ipo jirani na Maktaba ya Mkoa wa Iringa) na akaibadilisha jina na kuiita
MAKOSA CATS Hotel. Katika hoteli hiyo bendi nyingi zimepiga muziki na kwa
mara ya mwisho, mwanamuziki Macay Fanta alikuwa akifanya shoo zake mpaka pale
MAKOSA aliposhindwa kuiendesha mwanzoni mwa miaka ya 2000. Mtandao wa biashara
za makosa haukuishia hapo, alikuwa pia akimiliki hospitali maarufu sana iliyopo
jirani kabisa na soko kuu la mjini Iringa, hii nayo iliitwa MAKOSA hospital.
Taarifa kutoka kwake mwenyewe biashara
zote hizo haziko tena mikononi mwake na ugumu wa maisha unazidi kumuandama.
Japokuwa hajasema hivyo, huenda kuteteleka kwa hayo yote ndio sababu ya MAKOSA
kutaka kujiua. Tafsiri ya jina la MAKOSA imeendelea kuwa siri yake na
amekataa kutoa maana ya kuacha majina yake halisi ya Ramadhani Mrisho na
kujiita MAKOSA.
Chanzo: Frankleonard blog
No comments:
Post a Comment