BAO la penalti dakika ya 81 lililofungwa na kiungo
Kiggi Makassy, jioni hii limeipa Simba ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mathare
United ya Kenya katika mchezo wa kirafiki wa kujiandaa na mechi ya Ngao ya
Jamii kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha.
Hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao
na kipindi cha pili, Simba SC inayofundishwa na Mserbia, Milovan Cirkovick
ilipata bao la kuongoza dakika ya 53, mfungaji mshambuliaji kutoka Ghana,
Daniel Akuffo aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Amir
Maftah. Mathare walisawazisha bao hilo dakika ya 68,
mfungaji Daniel Mwaura aliyeipasua ngome ya Simba SC, iliyokuwa ikiogozwa na
Paschal Ochieng na Juma Nyosso. Beki wa Mathare alimuangusha kwenye eneo la hatari,
Uhuru Suleiman dakika ya 80 na ushei na refa akaamuru ipigwe penalti,
iliyopachikwa kimiani kiufundi kwa guu la kushoto la Kiggi Makassy.
Simba ilicheza vizuri mechi hiyo, leo hii Haruna
Moshi ‘Boban’ akirudishwa katika nafasi ya kiungo baada ya kupatikana kwa
washambuliaji halisi. Alicheza kwa utulivu, akigawa vizuri mipira na hata
kuwapokonya mipira viungo wa timu pinzani.
Dakika za mwishoni ilishuhudiwa Boban akipitia mpira
kwa nguvu miguuni mwa mshambuliaji wa Mathare, baada ya Maftah kupitwa, kuashiria
kwamba kijana amebadilika si Yule wa kukaba kwa macho.
Feliz Sunzu na Akuffo walikuwa wanapishana vizuri
pale mbele na waliitia misukosuko ngome ya Mathare- zaidi ni kwamba wawili hawa
wanahitaji muda zaidi wa kucheza pamoja ili kutengeneza safu kali ya
ushambuliaji ya Simba SC.
Juma Kaseja na Mrisho Ngassa hawakushiriki kabisa
mechi ya leo kwa sababu walikuwa wagonjwa na Keita alimpisha Nyosso baada ya
kuumia.
Simba itamenyana na Azam katika mechi ya Ngao ya
Jamii ya kuashiria kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,
Septemba 8, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment