BM BARBERSHOP KINONDONI

Thursday, September 6, 2012

MWELELEKEO MPYA WA USAFIRI WA UMMA JIJINI DAR ES SALAAM JE MABASI YAENDAYO HARAKA KUWA MKOMBOZI WA KWELI KWENYE SEKTA HII MUHIMU??


SCENE NO. 1 – Historia ya Jiji la Dar Es Salaam
KUANZA KWA MJI WA DAR ES SALAAM
Maumbile ya ardhi ya eneo la jiji la Dar es salaam yamegwanyika katika sura kuu nne.Upande wa mashariki kuna ufuko wa bahari unaoinuka hadi m.50 juu ya usawa wa bahari ukifuatiwa na uwanda wa chini wa pwani wenye mwinuko mdogo wa m.50-100 juu ya usawa wa bahari.Magahribi mwa ukanda huu,kuna vilima vya Pugu ,vyenye miinuko kati ya m.100 na m.350 juu ya usawa wa bahari na vimekatishwa na mabonde ya mito yenye miteremko mikali inayoelekeza maji yake kwenye bahari ya Hindi.Baadhi ya mito hiyo ni mto Msimbazi huingia baharini kupitia kwenye ghuba yenye tingatinga za mimea aina ya mikoko.
MANDHARI YA BARABARA YA OCEAN ROAD
Hali ya hewa ya Dar es salaam ni ya joto kama ilivyo kawaida kwa maeneo ya pwani ya tropiki ambapo wastani wa kiwango cha unyevu katika hewa ni wa juu asilimia 96 nyakati za asubuhi na asilimia 67 nyakati za alasiri. Wastani wa mvua kwa mwaka ni milimita 1,000. Chimbuko la Jiji la Dar es salaam ni uamuzi uliofanywa na Sultani Majid bin Said wa Zanzibar mwaka 1862,na kujenga makao yake mapya pamoja na bandari katika Pwani ya Tanganyika. Lengo la uamuzi huo ilikuwa ni kuimarisha njia za biashara 'Carravan' zilizofunguliwa kuelekea kwenye maeneo ya Afrika Mashariki na ambazo zilijulikana kama 'Caravan Routes'. Ujenzi wa makao ya Sultani pamoja na bandari ulianza rasmi mwaka 1865 katika eneo la kijiji kidogo kilichojulikana kwa jina la Mzizima.Ujenzi huo ulikamilika mwaka 1866 na Sultani Majid bin Said kuhamia Dar es salaam mwaka huo.

Mara baada ya kuanzishwa, mji wa Dar es salaam ulipanuka na uchumi wake kukua kwa kasi kubwa ingawaje ni kwa kipindi kifupi tu hadi Sultani Majid bin Said alipokufa mwaka 1870. Kifo cha Sultani huyo kilisababisha kudidimia kwa maendeleo ya mji wa Dar es salaam. Hali hiyo ilianza tena kubadilika mwaka 1884 kufuatia kuanzishwa kwa koloni la Wajerumani la Afrika ya Mashariki.

UKUMBI WA KARIMJEE DAR ES SALAAM
Mwaka 1891 serikali ya kikoloni ya Kijerumani iliamua kuhamisha makao makuu ya utawala wao katika Afrika Mashariki Bagamoyo na kuyaweka Dar es salaam. Hata baada ya Wajerumani kushindwa na Waingereza katika vita kuu ya kwanza ya dunia mwaka 1916,mji wa Dar es salaam uliendelea kuwa makao makuu ya utawala wa koloni la Waingereza nchini Tanganyika,hadi Tanganyika ilipopata uhuru wake mwaka 1961. Dar es salaam iliendelea kuwa makao makuu ya Tanganyika huru na hatimaye kuwa makao makuu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi mwaka 1972 wakati serikali ilipoamua kuhamishia makao yake makuu mjini Dodoma.
MNARA WA KUONGOZEA MELI ENEO LA KIVUKONI
Mji wa Dar es salaam ulitangazwa kuwa mji wenye serikali yake ya mtaa mwaka 1920. Hadhi ya mji wa Dar es salaam ilipandishwa kuwa manispaa mwaka 1949 na baadaye kutunukiwa hadhi ya Jiji la Malkia wa himaya ya Uingereza, wakati Tanganyika ilipopata uhuru mwaka 1961. Kwa kipindi hicho,Jiji la Dar es salaam lilikuwa likiongozwa na halmashauri ya Jiji la Dar es salaam hadi mwaka 1972 wakati ambapo serikali ilivunja serikali zote za mitaa nchini ili kutekeleza mfumo wa madaraka mikoani.Mamlaka za miji nchini Tanzania zilirejeshewa madaraka mwaka 1978.

Mwaka 1857 mji wa Dar es salaam ulikuwa na watu 3,000 tu.Idadi hiyo iliongezeka hadi kufikia watu 128,742 mwaka 1957,watu 272,821 mwaka wa 1967.Idadi ya wakazi wa Dar es salaam kwa mujibu wa sensa,ilikuwa 843,000 mwaka 1978 na kuongezeka hadi kufikia watu 1,360,850 mwaka 1988.
BAADHI YA MIZUNGUUKO KATIKAKATI YA JIJI LA DAR ES SALAAM
Idadi ya watu kwa sasa Jijini Dar es salaam inakadiriwa kufikia zaidi ya 3,000,000 kukiwa na mamlaka za manispaa katika wilaya za Ilala, Kinondoni na Temeke. Ongezeko hili la watu ndani ya Jiji la Dar es salaam na manispaa zake linazua changamoto katika uwekezaji zaidi kwenye miundo mbinu ya huduma za kijamii katika sekta za afya, elimu, mazingira na usafirishaji. Mawakala wa huduma za forodha ni sehemu ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na huduma zao zinaendelea kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii Jijini Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla.
JIJI LA DAR ES SALAAM KWA JUU
Mkoa wa Dar es Salaam ulianzishwa kutoka Mkoa wa Pwani ukiwa na Wilaya 3 za Ilala, Kinondoni na Temeke. Kipindi hicho Serikali kuu ilihodhi madaraka. (Madaraka Mkoani) Mfumo wa Serikali za Mitaa ulirejeshwa tena mwaka 1982-1984. Hata hivyo Mamlaka za Serikali za Mitaa za Mkoa wa Dar es Salaam zilizopo sasa zilianzishwa mwaka 2000 baada ya kuvunjwa iliyokua Tume ya Jiji iliyokuwepo tangu 1996 hadi 1999. Hadi sasa mwaka 2012 Mkoa wa Dar e s Salaam una Wilaya 3 za kiutawala Ilala, Kinondoni na Temeke ambazo pia ni Halmashauri za Manispaa, pia ipo Halmashauri ya Jiji na Majimbo 8 ya uchaguzi Tarafa 10, Kata 90 na Mitaa 448.

HISTORIA YA MKOA WA DAR ES SALAAM
JENGO LA HALMASHAURI YA JIJI LA DAR ES SALAAM
Jiji la Dar es Salaam lipo kati ya latitudo nyuzi 6 hadi 7 na longitudo kati 39.45 kwa upande wa Mashariki na nyuzi 39 kwa upande wa magharibi, Kusini mwa ikweta na upande wa magharibi, Kusini na Kaskazini. Jiji linapakana na Mkoa wa Pwani upande wa Mashariki linapaka na Bahari ya Hindi. Jiji la Dar es Salaam lina eneo la ukubwa wa kilomita za Mraba zipatazo 1,800; kati ya hizo, kilomita za mraba 1,350 ni eneo la nchi kavu ikijumuisha visiwa vinane vilivyopo katika eneo la bahari ya Hindi. Jiji hupata joto la wastani wa kati ya nyuzi 25 hadi 33 na mvua katika misimu miwili ya vuli ambayo ni miezi ya Oktoba – Desemba na Masika ambayo huanza miezi ya Machi – Mei.
MNARA WA ASKARI KUTOKA ANGANI (ASKARI MONUMENT)
Kabla ya uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 Mkoa wa Dar es Salaam haukuwepo, kilichokuwepo ni mji wa Dar es Salaam. Mkoa ulianzishwa mwaka 1974 wakati wa madaraka mikoani. Jina la Dar es salaam lilitokana na majilio ya wageni wa Kiarabu, waliotokea pande za Persia. Waliita (Bandari Ur Salama) Kwa lugha ya Kiswahili Bandari ya Salama. Kihistoria, Jiji hili limekaliwa na kutawaliwa na wageni wa aina mbalimbali. Dar es Salaam ilipata hadhi ya mji mdogo mwaka 1920 na mwaka 1949 ilipata hadhi ya kuwa Manispaa.

Miaka ya Sitini Mkoa wa Dar es Salaam uligawanywa kwenye Maeneo Makuu matatu ya Kinondoni, Temeke na Ilala ikiwa chini ya Wilaya ya Mzizima. Magawnyo huu uliwezesha wakazi wa maeneo hayo matatu kuwa na shughuli tofauti za kiuzalishaji mali kulingana na maeneo wanayotoka.

HISTORIA YA MANISPAA YA KINONDONI
JENGO LA HALMASHAURI YA MANISPAA YA KINONDONI
Mwaka 1961 Kinondoni ilikuwa sehemu ya wilaya ya Mzizima na kupata hadhi ya kuwa Manispaa tarehe 25/01/2000. Kabla ya uhuru wa Tanganyika 1961 hakukuwepo na Wilaya ya Kinondoni bali ilikuwa sehemu ya wilaya ya Mzizima. Baada ya Uhuru Wilaya ya Kinondoni ilianzishwa mnamo tarehe 1/7/1974 sambamba na kuanzishwa kwa Mkoa wa Dar es Salaam wenye Wilaya 3 za Kinondoni, Ilala na Temeke. Asili ya Kinondoni ilitokana na mkulima wa mazao ya mboga na jamii ya mizizi aliyeitwa KILONDONI. Kinondoni imepitia kwenye hatua hizi kama ifuatavyo; Mwaka 1982 kanda, Mwaka 1999 ilikuwa tume ya Manispaa ya Kinondoni na tarehe 25/1/2000 ilipata hadhi ya kuwa Manispaa ya Kinondoni.

Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ina ukubwa wa kilomita za mraba 531. Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imepakana na Wilaya ya Bagamoyo upande wa Kaskazini, upande wa Kaskazini Mashariki inapakana na Bahari ya Hindi, upande wa Kusini inapakana na Manispaa ya Ilala, upande wa Kusini Magharibi inapakana na Wilaya ya Kisarawe na upande wa Magharibi inapakana na Wilaya ya Kibaha.

HISTORIA YA MANISPAA YA TEMEKE
JENGO LA HALMASHAURI YA MANISPAA YA TEMEKE
Kabla ya Uhuru mwaka 1961 Wilaya ya Temeke ilikuwa katika mkoa wa Pwani. Miaka ya 1980 ilihamishiwa mkoa wa Dar Es Salaam.  Watu wa Temeke kabla ya Uhuru wengi wao walikuwa wazawa kwa maana ya Wazaramo, Wandengereko, Wakwere na Wamakonde wachache. Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ilianzishwa rasmi tarehe 1/2/2000. Asili ya Wakazi wa Temeke niwacheza bao na Ngoma za asili, mchezo wa bao ulikuwa ukichezwa kwenye maeneo maarufu kule Temeke hususan Mwembeyanga, Mwembemkamba na African Temeke.


Ngoma kama Vile Tokomile, Mkwaju Ngoma, Mganda, Gombesugu, Mchunje, Mchape, Mtondoo, Buti, Msewe Inayotambulika kama ngoma ya Mangariba zilichezwa sana eneo hili lililokuwa mkoa wa Pwani hapo awali. Vikundi maarufu wakati huo kwenye suala la ngoma moja wapo ni kikundi cha NGASUMO kilichokuwa kikipiga ngoma ya Tokomile maeneo ya Tandika sokoni.  Aidha Mangariba maarufu walikuwa LUMALIZA aliyeishi kati ya mtaa wa Ruvuma na Madenge na wengine ni SINDE, NZASA na SUBA taarifa hii nikwamujibu wa Mzee Shaaban Mzee Marufui sana eneo la Temeke Wailes.

Halimashauri ya Manispaa ya Temeke ni kubwa kieneo kuliko Manispaa zote ikiwa na eneo la kilomita za mraba 656; ipo upande wa kusini wa Mkoa wa Dar es Salaam ambapo kwa upande wa mashariki inapakana na Bahari ya Hindi, kusini inapakana na Wilaya ya Mkuranga – Mkoa wa Pwani na upande wa kaskazini na magharibi inapakana na Manispaa ya Ilala.

HISTORIA YA MANISPAA YA ILALA
JENGO LA HALMASHAURI YA MANISPAA YA ILALA
 Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ipo kati ya Latitudo 6 na 7 kusini mwa Ikweta na kati ya Longitudo 39 na 40 Mashariki. halmashauri ya Manispaa ya Ilala ina eneo la kilomita za mraba 210 ambapo zaidi ya asilimia 75% ya eneo hilo la Manispaa ya Ilala ni eneo la mji.  

Manispaa ya Ilala imepakana na Manispaa za Kinondoni na Temeke kwa upande wa Kaskazini na Kusini, Mkoa wa Pwani kwa upande wa Magharibi na Bahari ya Hindi katika ukanda wa Pwani wenye urefu Kilomita 10 kwa upande wa Mashariki. Idadi ya Watu Kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002, Manispaa ya Ilala ilikuwa na wakazi 637,573 wakiwemo Wanaume 321,903 sawa na asilimi 50.5% na Wanawake 315,670 sawa asillimi 49.5. Ongezeko la watu ni asilimia 4.6 kwa mwaka, Hivyo inakadiriwa kuwa idadi ya watu imefikia 795,024 mwaka 2007. 

BANDARI YA DAR ES SALAAM INAUWEZO MKUBWA
Manispaa ya Ilala ina jumla ya Kaya 187,581. Wastani wa ukubwa wa Kaya ni watu 4.3.
Wilaya ya Ilala inamezwa sana na Jiji kwakuwa pale ndiyo sehemu ambayo waliishi watu wenye asili ya Weupe. Maeneo ya Halmashauri ya Ilala yalijigawa kwa mabaka ya weupe kama ifuavyo:

Eneo la Kariakoo (Gerezani) waliishi waarabu wengi hadi maeneo ya karibu na Ilala Boma kuanzia pale Shauri Moyo. Eneo la Sokoni Kariakoo, Rumumba lilikuwa na Wapagazi wengi waliokuwa wanabeba mizigo inayotoka Bandarini wakati huo kwa kuja na Majahazi kutoka Zanzibar, Tanga, Shelisheli, Bagamoyo na Mashariki ya Mbali.

IDADI YA WATU
Mwaka 1948 mji wa Dar es Salaam ulikuwa na watu wapatao 69,227. Idadi ya watu imekuwa ikiongezeka kwa asilimia 4.3 (sensa ya 2002), hivyo sensa ya 2002 idadi ya watu ilifikia 2,497,000. Hadi sasa mwaka 2012 Jiji la Dar es Salaam linakadiriwa kuwa na watu 3,118,132 mabadiliko ya kisensa yanatarajiwa baada ya Sensa hii ya mwaka 2012.
KANISA LA MTAKATIFU JOSEPH KIOO CHA JIJI
UTAWALA
Kabla ya ukoloni walitawala Machifu na wazee wa mila. Walipokuja wakoloni walijitahidi kupambana na utawala huo na baada ya uhuru  utawala wa machifu uliondolewa, wakoloni walifanya kazi na Serikali za Mitaa ambazo zilivunjwa baadae.
MUONEKANO WA BANDARI YA DAR ES SALAAM,
MIUNDOMBINU
Mwaka 1961 ukubwa wa eneo la Dar es Salaam wakati huo ilikuwa kilometa za mraba 635 na sasa Jiji la Dar es Salaam lina eneo la kilometa za mraba 1,397. Kuhusu utoaji hati za umiliki wa ardhi iuikua unafanyika makao makuu ya Wizara pekee, kwa sasa kuna kanda zimeanzishwa ambapo hati hutolewa huko. Usafiri wa umma umekua kutoka treni na mabasi hadi ndege, meli/boti kwa sasa.
BUSTANI YA MNARA WA ASKARI INAVYOONEKANA SASA
MIUNDOMBINU YA DAR ES SALAAM WAKATI WA MVUA
FUATANA NAMI KESHO KWENYE UJUE USAFITRI WA UMMA ULIKOANZIA JIJINI DAR ES SALAAM!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!

KESHO - SCENE NO. 2 – Historia ya Usafiri wa Umma Jiji la Dar Es Salaam

No comments:

Post a Comment