Watu zaidi ya 18 wamepoteza maisha
na wengine 22 kujeruhiwa katika ajali iliyolihusisha lori aina ya Fuso. Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alithibitisha jana kutokea kwa
ajali hiyo ikihusisha gari hilo namba T407 KST lililokuwa likitoka kijiji cha
Ntalamila Wilayani Nkasi katika barabara ya Ntuchi – Sumbawanga. Hata
hivyo, hakutoa maelezo zaidi kwa madai kuwa alikuwa safarini kwenda eneo la
tukio na kuahidi kutoa taarifa rasmi baadaye.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka eneo la tukio, wengi wa abiria waliokuwa wakisafiri kwa gari hilo waliokuwa familia za wafugaji huku likiwa limesheheni magunia ya mahindi, kuku na zana za kilimo, yakiwamo majembe ya mkono na plau. Akizungumza na waandishi wa habari katika hospitali ya mkoa, Mganga Mkuu wa Hospitali, Dkt. Gasper Nduasinde, alisema hadi jana taarifa alizokuwa nazo ni watu 15 kufa papo hapo huku wengine 35 wakijeruhiwa, lakini akasema hadi jana hakuna maiti aliyekuwa ametambuliwa, “Hayo ndiyo ninayoweza kusema sasa, kwani tuko katika heka heka ya kuendelea kuhesabu majeruhi hospitalini, ili kupata idadi kamili, lakini taarifa nilizonazo watu 15 wamekufa na idadi hii inaweza kuongezeka wakati wowote kwani wengi wa majeruhi hali zao ni mbaya,” alisema.
Vyanzo vingine vya habari vilidai kuwa zaidi ya watu 18 walipoteza maisha katika ajali hiyo huku sita miongoni mwao, wakifa papo hapo. Mwandishi wa habari hizi alishuhudia wengi wa majeruhi wakiwa wamechunika ngozi kichwani huku wengine wamevunjika viungo. Mji wa Sumbawanga na viunga vyake uligubikwa na simanzi na majonzi makubwa huku wengi wakiangua vilio na baadhi kusubiri kutambua wapendwa wao. Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Idd Kimanta ambaye alikuwa eneo la tukio muda mfupi baada ya ajali hiyo kutokea, alimwambia mwandishi kwa njia ya simu kuwa ajali hiyo ilitokea jana saa 2.30 asubuhi. Alisema Fuso lilikuwa na zaidi ya abiria 50 na mizigo mingi yakiwamo pia masanduku ya soda na abiria sita wakiwamo watoto watatu walikufa papo hapo lakini mwingine mwanamke alikufa akiwa njiani katika gari la Mkuu wa Wilaya akikimbizwa hospitali ya mkoa kwa matibabu huku majeruhi 30 wakisafirishwa kwa basi dogo. Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya, dereva wa gari hilo ambaye ni mmiliki wa gari hilo, George Kawiti, mkazi wa kijiji cha Ntuchi, Nkasi alitoroka baada ya ajali hiyo.
Mmoja wa wafanyakazi wa basi la
"Bismark", basi ambalo liliahirisha safari zake ili kutoa msaada kwa
majeruhi, amelalamikia kitendo cha Polisi kuchukua muda mrefu kufika katika
eneo la ajali ili kutoa msaada kwa majeruhi. Amesema walipiga simu tangu ajali
ilipotokea saa mbili asubuhi lakini msaada wa kwanza wa Polisi ulipatikana saa
sita mchana. Anahoji, "iko wapi Serikali?"Majeruhi wameshukuru
ubinadamu na jitihada za basi la "Bismark" lililotoa msaada
uliohitajika.
No comments:
Post a Comment