HAYA NDIYO MAELEZO BINAFSI YA MHE. ZITTO ZUBERI KABWE DHIDI YA TUHUMA ZA RUSHWA HUSUSAN KUELEKEA KATIKA KUPITISHA BAJETI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI
Ndugu
Waandishi,
Nalazimika
kukutana nanyi kutoa maelezo juu ya tuhuma zenye shinikizo la kisiasa
zinazoelekezwa kwangu binafsi kwamba hata mimi nimeshiriki katika vitendo vya
rushwa, kwa nafasi yangu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya
Umma. Taarifa hizo, kama kawaida ya uzushi mwingine wowote zimesambazwa
kimkakati na kwa kasi kubwa kiasi cha kuukanganya umma.
Nafahamu
nabeba dhamana kubwa ya uongozi, taswira yangu ya uongozi daima imeakisi njozi
na matumaini ya wananchi wa Kigoma Kaskazini, wananchi wanyonge na vijana kote
nchini bila kujali itikadi zao za kisiasa, jinsia zao, makabila yao na rika
zao. Hivyo, nawajibika kupitia kwenu kuwatoa hofu juu ya hisia potofu
zinazopandikizwa kwao na wale wasiopenda kuona baadhi yetu tukiwaunganisha na
kuwasemea watanzania wasio na sauti, dhidi ya vitendo vya hujuma na vyenye
dhamira ovu kwa taifa.
Mkakati huo wa kuniunganisha na baadhi ya Waheshimiwa
Wabunge wanaotuhumiwa kwa kupokea Rushwa unatekelezwa kwa njia zifuatazo:
Kumekuwa
na kauli za watendaji wa serikali ambao wamekuwa wakizieneza na hususan kutoa
taswira kwamba baadhi ya kauli zangu zinatokana na ushawishi wa rushwa;
Kuna taarifa ambazo zimeandikwa tena katika kurasa za
mbele za baadhi ya vyombo vya habari zikidai ’’Zitto kitanzini’’ ama ’’Zitto
sawa na popo nundu’’ zikiashiria kwamba na mimi ni mla rushwa; na Waandishi wa
habari na jamii kwa ujumla wamefikia kuaminishwa habari hizi kiasi cha wengine
kuuliza kwa nini Mhe. Zitto Kabwe hakutajwa katika orodha iliyotolewa na
Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani.
Ndugu
Waandishi, Naomba kutoa ufafanuzi wa hicho kinachoelezwa kwamba nina ushiriki
katika masuala ya rushwa hususan kwenye masuala yanayohusu sekta ya Nishati na
Madini:-Mara baada ya bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Usambazaji wa Umeme
Tanzania (TANESCO) chini ya Uenyekiti wake Meja Jenerali Mstaafu Robert Mboma
kutangaza kwamba imemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Nd.
William Mhando ili kupisha uchunguzi wa baadhi ya vitendo/mwenendo wake, Kamati
ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ambayo mimi ni Mwenyekiti wake
ilimuandikia Mhe. Spika kumuomba aridhie ili Kamati iweze kuwaita Bodi ya
TANESCO, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG) na pia Mamlaka
ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kujiridhisha na tuhuma zote zinazotajwa
zinafanyiwa uchunguzi wa kina na hatua kuchukuliwa;
Kamati ya POAC ninayoiongoza ilimuomba Mhe. Spika
kuwaita wahusika tajwa kwa kuwa zilikuwapo tetesi kuwa kusimamishwa kazi kwa
Mkurugenzi huyo siku chache kabla ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kulikuwa
na lengo la kufunika ’madudu’ makubwa zaidi kwa kulichagiza Bunge na tukio hilo
dogo, mkakati ambao naona umefanikiwa sana. Isitoshe, Kamati kutaka
kujiridhisha na hatua za Bodi ni sehemu ya msingi ya utekelezaji wa majukumu ya
Kamati yaliyowekwa kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge na pia Shirika la
TANESCO ni moja kati ya mashirika ambayo yanawajibika kwetu kwa hesabu zake na
pia ufanisi wake kwa ujumla. Tumefanya hivyo pia katika mashirika mengine, hili
la TANESCO sio tukio la kipekee;
Kitendo hiki cha halali na kwa mujibu wa Kanuni
kilichofanywa na Kamati yangu kimetafsiriwa kwa makusudi na baadhi ya watu
kwamba ni ishara ya kuwa sisi au zaidi kwamba mimi nina maslahi binafsi na
TANESCO na hususan Mkurugenzi wake Injinia Mhando, ndio maana tumetaka maelezo
ya Bodi. Ukweli kwamba Kamati ya POAC tumewaita pia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Mahesabu (CAG) na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kwa jambo hilo
hilo umefichwa kwa makusudi!
Baada ya tukio hilo, nikiwa hapa Dodoma, mwandishi wa
habari wa gazeti moja alinifuata akiniambia kuwa wamekutana na Mhe. Waziri
Mhongo na Katibu Mkuu wake, Nd. Eliachim Maswi hapa hapa Bungeni na wamewaambia
kuwa mimi nimepewa rushwa. Hakutaja nimepewa rushwa na nani, kiasi gani na wala
kwa lengo gani!
Nimejaribu kumtafuta kwa simu Mhe. Waziri Mhongo na
Katibu Mkuu wake ili wanipe ufafanuzi juu ya mimi na Kamati ya POAC kuhusishwa
na tuhuma hizi bila mafanikio, hali ambayo inaniondolea mashaka juu ya ushiriki
wao katika kueneza au kuthibitisha uvumi huo. Najaribu sana kujizuia kutokuwa
na mashaka na ushiriki wao huo ikizingatiwa uzito na taswira ya nafasi zao
katika jamii, lakini wameshindwa kunidhihirishia tofauti.
Sasa naomba kutoa ufafanuzi rasmi kuhusu mlolongo wa
matukio hayo tajwa ambayo yanatumiwa na baadhi ya wanasiasa kuonesha kwamba eti
nimehusika na vitendo vya rushwa.
Binafsi sijawahi kuwa na mawasiliano ya aina yeyote na
uongozi wa TANESCO kushawishiwa juu ya hatua ambazo POAC ndio imezichukua za
kutaka kujiridhisha juu ya utaratibu uliotumika. Ieleweke wazi kabisa kuwa,
hakuna wakati wowote, popote ambapo mimi binafsi au Kamati yetu imekataa
Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO kuchunguzwa kwa tuhuma zozote. Ambacho tumesisitiza
wakati wote ni ufuatwaji wa taratibu, kanuni na sheria, hili nitalisimamia iwe
masika au kiangazi; Ni kwa sababu hiyo, na kwa kujiamini kabisa nimeunga mkono
suala la tuhuma za rushwa zinazotajwa zichunguzwe na Kamati ya Haki, Maadili na
Madaraka ya Bunge kwa kina; Nimekwenda mbali zaidi kukiomba chama changu
CHADEMA kifanye pia uchunguzi na tathmini yake kwa kina kujiridhisha na tuhuma
hizo; Natumia fursa hii pia kuomba vyombo vya Dola vichunguze tuhuma hizo kwa
nafasi yake ili kuweza kupata ukweli; Ninaahidi kushiriki kikamilifu iwapo
nitatakiwa katika uchunguzi wowote utakaofanywa na niko tayari kuwajibika iwapo
nitakutwa na hatia yeyote.
Napenda niwatoe hofu wananchi wa jimbo la Kigoma
Kaskazini walionituma kuja kuwawakilisha hapa Bungeni na Watanzania wote kwa
ujumla kwamba:-Mimi Zitto Zuberi Kabwe sina bei, sijawahi kuwa nayo na
sitarajii kuwa nayo huko mbeleni. Daima nimesimamia kidete maadili ya uongozi
bora katika maisha yangu yote ya siasa, na nawaahidi sitarudi nyuma katika
mapambano dhidi ya rushwa katika nchi hii pamoja na mikakati ya aina hii ya
kunidhoofisha na kunivunja moyo;
Nafarijika
na salam mbali mbali zinazotolewa kunifariji na kusisitiza kuwa nisilegeze
kamba katika mapambano haya, nimepokea ujumbe mwingi kwa simu, sms, tweeter na
hata facebook na niko pamoja nanyi Watanzania wenzangu kamwe sitarudi nyuma
hadi kieleweke. Naamini katika nchi yetu tunazo rasilimali za kutosha
mahitaji/haja ya kila mmoja wetu lakini si ‘tamaa/ulafi’ wa baadhi ya
watanzania wenzetu;
Napenda kuweka rekodi sawa kwa Watanzania kwamba
nimekuwa Mbunge hiki ni kipindi cha pili, Mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) huu ni takriban mwaka wa saba sasa, Kamati
yangu inasimamia mashirika 259 ya Umma na si TANESCO peke yake. Mchango wa
Kamati hii katika Bunge na kwa ustawi wa Mashirika ya Umma ni bayana na
haujawahi kutiliwa shaka. Kamati yetu imeokoa upotevu mkubwa wa mali za umma na
kuokoa fedha za umma kutokana na umakini wake. Tumefanya hivyo CHC hivi
karibuni, Kiwira na kwenye mashirika mengine mengi. Kote huko uadilifu na
uzalendo wa Kamati hii haujawahi kuhojiwa. Inatuwia vigumu kuona kuwa
tunahojiwa katika suala hili la TANESCO. Hapa pana kitendawili.
Zipo
hoja pandikizi za kutaka Kamati ya POAC ivunjwe na haswa zikinilenga mimi
binafsi. Nafahamu kiu ya wasioitakia mema nchi yetu kuiona POAC ikivunjwa au
sura zikibadilishwa kwa kuwa Kamati hii imekuwa mwiba kwa mikakati yao ya
kifisadi. Kwa maoni yangu, Kamati ya POAC isihusishwe na tuhuma hizi kwa
vyovyote vile. Niko tayari nihukumiwe mimi kama mimi na sio kuhusisha wajumbe
wengine ambao hawatajwi mahala popote katika tuhuma hizi mbaya sana katika
historia ya Bunge letu. Nitakuwa tayari kunusuru Kamati ya POAC na maslahi ya
taifa letu kwa kujiuzulu Uenyekiti iwapo itathibitika pasipo shaka kuwa
nimehongwa. Kamati ya POAC ni muhimu zaidi kuliko mimi. Nafahamu pia kuwa kuna
wanasiasa hasa wa Upinzani ambao wanautaka sana Uenyekiti wa POAC na wanafanya
kila njia kutaka kuidhoofisha. Lakini hawajui kuwa anaepanga wajumbe wa Kamati
ni Spika wa Bunge.
Msishangae pia kuja baadae kubaini kwamba baadhi ya wanasiasa
wenye midomo mikubwa ya kutuhumu wenzao wao ndio vinara wa kupokea rushwa.
Ni lazima tufike mahali kama viongozi kwamba utaratibu
unapokiukwa na yeyote yule, au uongo unapotolewa hadharani tuseme bila kuogopa.
Hili ndio jukumu letu kama wabunge na viongozi. Kusimamia ufuatiliaji wa
utaratibu ni jukumu letu kama Kamati ya POAC na ndio sababu ya msingi ya
kuanzishwa kwa mamlaka kama CAG na PPRA. Haiwezekani, tuwe na set ya kanuni kwa
kundi fulani na nyingine kwa makundi mengine, au kuhukumu ufuataji wa taratibu
kwa kuangalia sura ya mtu usoni.
Mwisho
Kumejengeka tabia hivi sasa ya kuwamaliza wanasiasa wenye kudai uwajibikaji na
uzalendo. Kumeanzishwa kiwanda kwenye medani ya siasa cha kuzalisha majungu na
fitna zenye lengo la kuwachonganisha wanasiasa wa aina hiyo na wananchi kwa
kutumia vyombo vya habari na nguvu ya fedha. Naamini mbinu hizi chafu, kama
nyingine nyingi zilizojaribiwa kwangu huko nyuma nazo zitashindwa.
Naamini
katika kweli na kweli daima huniweka huru. Naamini kuwa mwale mdogo wa mwanga
wa mshumaa hufukuza kiza. Kwa imani hiyo, sitasalimu amri mbele ya dhamira zao
ovu hata nitakapobaki peke yangu katika mapambano hayo ya kulinda na kutetea
rasilimali za taifa zinufaishe watanzania wote.
Daima
nitaongozwa na busara ya Hayati Shabaan Robert isemayo, ‘Msema kweli huchukiwa
na marafiki zake, nitakapofikwa na ajali hiyo, sitaona wivu juu ya wale wawezao
kudumu na marafiki zao siku zote, siwezi kuikana kweli kwa kuchelea upweke wa
kitambo, nikajitenga na furaha ya kweli itakayotokea pale uwongo
utakapojitenga”.
Ahsanteni sana.
No comments:
Post a Comment