BM BARBERSHOP KINONDONI

Wednesday, August 15, 2012

JAMES KIBOSHO AKILI KUWA ALLY CHOKY NDIYE ALIYEMLETA TWANGA PEPETA




Mkali wa drum anayeing'arisha Twanga Pepeta alimshangaza sana Ally Choki kwa uwezo wake mwanafunzi huyu wa Petit Makambo na Hamisi Magendela na Baadaye kukomazwa na marehemu Abuu Ally Semhando.
James Michael Kibosho anasimulia historia yake kwenye Muziki kama ifuatavyo:
"NILIANZA kuchezo shoo katika kumbi mbalimbali za starehe na kwenye shughuli ikiwemo maharusi kabla ya kupiga 'drums' ambayo ndiyo ilikuwa ndoto yangu kubwa maishani mwangu".
Hivi ndivyo alivyoanza kujieleza mpiga vyombo huyo tegemeo wa bendi ya muziki wa dansi ya African Stars 'Twanga Pepeta', James Michael almaarufu 'Kibosho', jina la ukoo wao.

Mwanamuziki huyu ambaye kwa sasa anabeba jahazi katika upande wa kucharaza mabati hayo, ambayo yanakuwa ni muongozo kwenye upigaji wa vyombo, anasema anajisikia faraja kufikia hatua hiyo baada ya safari ndefu yenye vikwazo vingi. Nyota huyu ambaye ni mtoto wa tano katika ya watoto watano wa Mzee Michael Kibosho, anasema baada ya kumaliza elimu ya msingi 2001, katika shule ya msingi Umoja iliyopo Mabibo, Dar es Salaam, Manispaa ya Kinondoni, na baadaye kuingia rasmi kwenye miziki. Anasema mwaka 2002 alianza kujifunza kupiga 'drums' katika bendi ya Lolita. Kutokana na kiu ya kupenda fani hiyo aliweza kujua kwa haraka sana na kuanza kupiga katika bendi zilizokuwa zikipiga muziki kwenye kumbi kwa ujira wa sh 1500 hadi 2000 kwa siku. "Kupiga drums katika bendi hizo nilipata ujuzi wa kutosha na kufanikiwa kujiunga katika bendi ya Maliki Star iliyokuwa ikiongozwa na Petit Makambo, ambaye alinipa mafunzo zaidi ya kutumia chombo hicho ambacho sasa napata riziki. Kwa kweli alinipa siri kubwa ambayo naitumia na kuwa tofauti na wapiga 'drums'  wengine na hadi leo namheshimu sana,"
Kibosho anasema baada ya kipindi kifupi, alikwenda Jijini Tanga kuanzisha bendi ya Super Sound, chini ya Makambo. Mapema 2003 wakaja Dar es Salaam kurekodi nyimbo kadhaa ambazo zilikuwa zimekamilika baada ya kukaa kambini Jijini Tanga kwa muda wa miezi sita. James anabainisha kuwa baada ya kumaliza kurekodi nyimbo mbalimbali, walirejea Jijini Tanga. Kibosho alisikia kuwa kuna bendi mpya inayoitwa Extra Bongo ikiwa chini ya 'Mzee wa Farasi', Alli Choki, ndipo akapata ushawishi wa kwenda Dar es Salaam kujaribu bahati yake.
"Ilikuwa kawaida yangu kujaribu kila eneo nililohisi kuwa na mafanikio japo ilikuwa kawaida yangu kununua kanda za kaseti na kusikiliza na kuzifanyia mazoezi kitu ambacho kiliniwezesha kujua mapigo ya nyimbo mbalimbali tofauti," anaweka wazi Kibosho.

Mwanamuzki huyu anasema aliweza kununua kaseti ya albamu ya Extra Bongo ya 3X3 kwa lengo la kupata uzoefu kabla ya kwenda Dar es Salaam kujaribu bahati yake.
Baada ya kufanya mazoezi ya kutosha na kujiridhisha kuwa amefikia kiwango cha kutosha, alinyanyua mguu nakwenda Dar es Salaam na kuomba nafasi ya kujaribiwa kupiga kifaa hicho. "Nilikutana na Mkurugenzi wa bendi Ally Choki, baada ya kuzungumza naye alinijaribu kwenye kupiga drums kwa hakika nilifanya maajabu 'wonders', kila mmoja alikubali uwezo wangu baada ya kupiga kibao cha 3X3," alisema J Kibosho.
Baada ya miezi mitatu aliitwa na uongozi wa bendi hiyo na kutambulishwa rasmi kupigia bendi ya Extra Bongo. Nilijisikia faraja kuwemo katika kikosi kazi cha bendi hiyo nikiamini kuwa ulikuwa mwanzo wa kuonekana kuelekea kwenye mafanikio kupitia tasnia hiyo," anasema.
Mwanamuziki huyo aliyezaliwa Desemba 17, 1987 Jijini Dar es Salaam anasema baada ya kuingia katika bendi hiyo alifanikiwa kupiga nyimbo kadhaa ikiwemo ya Double Double iliyofanya vizuri katika maeneo mbalimbali na baada ya siku chache kundi hilo lilivunjika na kujiunga Double Extra iliyokuwa chini ya Mwinjuma Muuni na Alli Choki 'Mzee wa Farasi' na kwenda Chalinze kukaa kwa miezi miwili kabla ya kutoa albamu ya kwanza iliyopewa jina la Chungeni Ndoa.
Mwaka 2004 bendi hiyo ilivunjika na yeye kujiunga na bendi ya Double M Sound akiwa chini ya Muumini 'Kocha wa Dunia', na wakafanikiwa kutoa albamu ya Titanic iliyokuwa na nyimbo saba na kufanikiwa kupiga nyimbo sita ikiwemo Ukewenza, Titanic, Ndoa ya Ufukara, Mapenzi Siyo Mtaji, Air Omani ambayo haikufanya vizuri katika soko la muziki.
"Unajua kutokana na matatizo madogo bendi ilivunjika nikajiunga na Mchinga Sound 'G8' ambayo nilidumu nayo kwa wiki moja tu ndipo nikapata nafasi ya kujiunga African Stars 'Twanga Pepeta' na kupokelewa tena na Ally Choki Mzee Wa Farasi baada ya kufaulu kupiga vyema kibao cha Safari 2005," anasema.
Baada ya kufika katika bendi hiyo alipata ujuzi zaidi kutoka kwa Abuu Semhando 'Baba Diana', ambaye kwa sasa ni marehemu, ambapo anamkumbuka kwa ujuzi aliomwachia.
"Tangu 2006 nilipotua nimeweza kushiriki kupiga albamu zote na 2008 aliniachia nyimbo tano kati ya saba. "Kwa kweli Mwenyezi Mungu ailaze roho ya baba yangu Abuu Semhando mahali pema peponi, hakika bado namkumbuka kutokana na mchango wake kwangu kwa jinsi alivyokuwa akinishauri na kunipa muongozo ambao unanipa mwelekeo mzuri katika fani hii," anasema Kibosho ambaye ni mdogo wa mpiga 'drums' wa bendi ya Extra bongo, Martini Kibosho.
Kibosho anavutiwa zaidi na mpiga 'drums' Peter Col wa Werrason Ngiama ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na malengo yake ni kuanzisha bendi yake mwenyewe.

HUYU NDIYE JAMES MICHAEL KIBOSHO

No comments:

Post a Comment