BM BARBERSHOP KINONDONI

Monday, September 3, 2012

MATAMKO MBALIMBALI JUU YA KIFO CHA MWANGOSI


TAMKO LA CHAMA CHA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA MBEYA (MBPC) DHIDI YA JESHI LA POLISI NCHINI.

Chama cha waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya (MBPC)kimepokea kwa masikitiko taarifa ya mauaji ya Mwandishi na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari Mkoa wa Iringa, Daudi  Mwangosi yanayodaiwa kufanywa na Jeshi la Polisi Mkoani Iringa tarehe 2/9/2012. Kutokana na mauaji hayo na kutoridhishwa na nguvu kubwa kupita kiasi inayotumiwa na polisi dhidi ya raia, Waandishi wa habari Mkoa wa Mbeya wanaungana na waandishi wa habari nchini kusitisha kutoa taarifa za jeshi la polisi hadi hapo jeshi hilo litakapokubali kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa polisi waliohusika kufanya mauaji  hayo akiwemo, Kamanda wa polisi Mkoa wa Iringa  aliyeongoza operesheni hiyo.

Tamko hilo pia limeeleza wazi kuwa muda umefika kuwe na mkataba maalumu wa kazi  kati ya waandishi wa habari na jeshi la polisi na kwamba atakayekiuka hatua za kisheria dhidi ya majukumu ya kila chombo zichukuliwe hatua kali za uwajibishaji.
Ili kujenga dhana ya uwazi na uwajibikaji,Waandishi wa habari Mkoa wa Mbeya wanamtaka Waziri wa mambo ya ndani, Mkuu wa jeshi la polisi nchini (IGP) na Kamanda wa mkoa wa Iringa wajiuzulu nyadhifa zao kwa kuwa wameshindwa kusimamia vyema usalama wa raia na mali zao.

Pia Tamko hilo limebainisha mfumo wa uundwaji wa tume ya kuchunguza kifo hicho haupaswi kuongozwa na Jeshi la polisi kwa kuwa ndio waliohusika na mauaji hayo na kwamba tume huru itakayoundwa ipewe muda maalumu ili majibu yapatikane mapema na  kwa haraka na hatua za kisheria zichukuliwe kwa wahusika.

Waandishi wa habari Mkoa wa Mbeya, wanaamini kuwa Serikali na jeshi la polisi litachukua hatua stahiki kwa waliohusika na mauaji ya Mwandishi Daudi Mwangosi, na pia Polisi watajitathmini upya katika utendaji wa shughuli zake hasa katika udhibiti wa vurugu na uzuiaji wa maandamano.

………………………………..
Christopher Nyenyembe,
Mwenyekiti MBPC.

Nakala ;
1.Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama.
2.Inspekta wa Jeshi la Polisi(IGP).
3.Vyombo vyote vya Habari



Taarifa kwa vyombo vya habari, Septemba 03, 2012

Sikika imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi.  Kwa mujibu wa vyombo vya habari, marehemu Mwangosi alikuwa kazini akitimiza wajibu wake wa kutafuta habari. Tumestushwa zaidi baada ya kuona picha za mnato zikionyesha jinsi ambavyo mtu anayedaiwa kuwa ni mwandishi huyo akishambuliwa na idadi kubwa ya askari polisi na baadae kupoteza maisha.
Katika siku za karibuni, tumeshuhudia ongezeko la matumizi ya nguvu kupita kiasi yanayofanywa na jeshi la polisi, ambayo siyo tu yanasababisha uharibifu mkubwa wa mali za wananchi bali pia baadhi yao kupoteza maisha. Mfano, mwezi uliopita, tuliarifiwa kuwa kijana aliyeuawa mkoani Morogoro alikuwa akiuza magazeti na wala hakuhusika katika vurugu kwa namna yoyote. Vivyo hivyo, marehemu Mwangosi alikuwa akitimiza wajibu wake wa uandishi wa habari.
Uhai ni haki ya kikatiba ya kila Mtanzania. Hivyo, ni jukumu la polisi kulinda maisha na uhai wa wananchi wote bila kujali itikadi au kazi zao. Hakuna sheria inayohalalisha kujeruhi, kutesa wala kuua mwananchi yeyote kwa sababu tu ati amekataa kutii amri ya polisi. Sikika inasikitishwa zaidi na utamaduni unaozoeleka ndani ya jeshi la polisi kwamba matukio ya kujeruhi, kutesa au  vifo ni halali iwapo wanasiasa au wananchi hawakutii amri.
Kwa mtazamo wetu, amri ya serikali au polisi haitakiwi kuwa juu ya Katiba inayolinda haki ya  kuishi. Hivyo, kisingizio cha kukiuka amri ya polisi hakitakiwi kuwa sababu ya kujeruhi wala kuua binadamu yeyote. Hata kama polisi watatoa maelezo kukanusha kuwa picha ya mtu anayeteswa si mwandishi, je wanayo haki ya kumjeruhi, kumtesa au kumdhalilisha mtanzania yeyote kama inavyoonekana kwenye picha hizo?
Tangu matukio haya ya kujeruhi, kutesa na hata kuua wananchi yalipoanza, hakuna hatua za dhati zilizochukuliwa na serikali wala jeshi la polisi. Vitendo hivi vinavyofanywa na polisi siyo tu vinapunguza imani ya jeshi hilo kwa wananchi, bali pia vinakiuka wajibu wa msingi wa jeshi hilo ambao ni kulinda usalama wa raia.
Ni matumaini yetu kwamba waliohusika na kifo cha Daudi Mwangosi na watanzania wengine waliopoteza maisha katika mazingira ya aina hii, watachukuliwa hatua stahiki. Pia, maaskari wanaoonekana katika picha hizo wakimtesa na kumnyanyasa raia wafikishwe kwenye vyombo vya sheria ili iwe funzo kwa wengine.
Tunatoa pole nyingi kwa familia na ndugu wa marehemu Daudi Mwangosi pamoja na tasnia ya habari hapa nchini. Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi, Amen.

Bw. Irenei Kiria
Mkurugenzi Mtendaji, Sikika, S. L. P 12183 Dar es Salaam,
Simu: +255 222 666355/57, Nukushi: 2668015, Barua pepe: info@sikika.or.tz, Tovuti: www.sikika.or.tz


TAMKO LA CHAMA CHA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA DODOMA (CPC)

CHAMA cha waandishi wa habari mkoa wa Dodoma (CPC)wamelaani vurugu zilizotokea juzi mkoani Iringa na kusababisha kifo cha mwandishi wa habari wa kituo cha utangazaji cha Chanel Ten Daud Mwangosi. Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa chama hicho Habel Chidawali alipokuwa akitoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari mkoani hapa.

Chidawali amesema kuwa kamwe chama hicho hakikubaliani na nguvu kubwa iliyotumiwa na jeshi la polisi kwa ajili ya kumwaga damu ya mwandishi huyo ambaye hakuwa na hatia na kamwe jeshi la polisi haliwezi kujitetea kwa kudai kifo cha mwandishi huyo ni bahati mbaya. Amesema kuwa jeshi la polisi limekuwa likionyesha wazi wazi kuwa linatumia nguvu,ubabe na matumizi mabovu ya silaha za moto ambayo hayajaweza kusaidia siku zote na badala yake kinachoachwa ni maumivu na vilio kwa wananchi.

Katibu huyo amesema kama jeshi la polisi linatuliza ghasia hakuna siku hata moja haijatokea wakamuua kiongozi yoyote wa siasa ambao nivinara wa mikutano mbalimbali. Kwa upande wao wananchi mbalimbali mkoani hapa wamekemea nguvu kubwa inayotumika na Polisi katika vurugu mbalimbali zinazotokea. Wamesema tabia ya jeshi la polisi kutumia nguvu na silaha za moto ambazo zinasababisha vifo vya watu wasiokuwa na hatia.

Catheline Muhinte, amesema kuwa tukio lililofanywa na jeshi la polisi la kumuua mwandishi wa habari linaonyesha dhairi kuwa kwa sasa jeshi hilo linafanya kazi kwa kukiuka maadili ya malengo yao. Amesema katika mwonekano wa picha ambazo zinaonekana katika vyombo mbalimbali vya habari inaonyesha dhairi kuwa polisi walihusika moja kwa moja na kifo cha mwandishi huyo.

TAMKO LA JUKWAA LA WAHARIRI TANZANIA KUHUSU KUUAWA KWA DAUDI MWANGOSI

TAARIFA YA JUKWAA LA WAHARIRI (TEF) KWA VYOBO VYA HABARI
KUHUSU KUUAWA KWA MWANDISHI DAUDI MWANGOSI

UTANGULIZI:
1.      Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, mkoani Iringa, Daudi Mwangosi.

2.      Mwangosi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Iringa (IPC), aliuawa akiwa kazini jana, Septemba 2, 2012, wakati polisi walipokuwa wakiwadhibiti wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

3.      Tukio hili linaiingiza Tanzania katika historia mbaya ya ukiukwaji na ukandamizwaji wa uhuru wa habari, kwani ni kwa mara ya kwanza tunashuhudia mwandishi wa habari AKIUAWA WAKATI AKITEKELEZA MAJUKUMU YAKE YA KIHABARI.

4.      Taarifa za awali zinaonyesha kuwa Mwangosi kabla ya kufikwa na mauti saa 9.30 alasiri katika kijiji cha Nyololo, Mufindi, alizingirwa na kushambuliwa na polisi waliokuwa katika eneo la tukio. Na hata alipopiga kelele za kuomba msaada, hakusikilizwa na matokeo yake aliuawa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu.

5.      Kwa kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania, TEF tumechukua hatua za haraka za kuunda timu ya uchunguzi wa suala hilo, ambayo itakwenda mkoani Iringa mapema kadri itakavyowezekana, ili kubaini ukweli wa tukio hilo. Lengo la uchunguzi huo ni kuweka kumbukumbu sahihi (documentation) ya tukio hilo la aina yake katika historia ya nchi yetu.

6.      Matokeo ya uchunguzi huo pamoja na mwingine unaofanywa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), ndiyo yatakayotoa mwelekeo wa hatua ambazo TEF inachukua dhidi ya Jeshi la Polisi katika siku chache zijazo.

MTIZAMO NA MSIMAMO WA TEF
Kwa kuzingatia taarifa kutoka Iringa na zile za vyombo vya habari vya jana (Jumapili, Septemba 02, 2012) na leo (Jumatatu, Septemba 03, 2012), TEF ina mtizamo na msimamo kama ifuatavyo:

1.      Kwanza tunalaani vikali tukio la kupigwa, kisha kuuwawa kwa mwandishi Daudi Mwangosi ambalo limeigusa tasnia ya habari kwamba sasa pengine waandishi wa habari ni malengo “target ya polisi” wanapokuwa kwenye kazi zao.

2.       Ieleweke wazi kwamba matukio haya siyo yanaondoa imani ya waandishi wa habari kwa jeshi la polisi tu, bali yanaweza kuwa chanzo cha uhasama na ufa mkubwa ambao utawanyima wananchi nafasi ya kutumikiwa na pande mbili ambazo zinategemeana.

3.      Kwa matukio ya aina hii, tunadhani wakati mwafaka kwa uongozi wa Jeshi la Polisi nchini kuwajibika, kuazia kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa na uongozi wa Makao Mkuu, akiwamo Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Saidi Mwema.

4.      Tunasema hivi kwani kuna kila dalili kwamba polisi wanahusika kwa namna moja au nyingine na tukio au/na matukio yaliyosababisha kifo cha Mwangosi, kwani kitendo cha kumzingira tu na kumshambulia kinathibitisha kwamba hawakuwa na nia njema hata kidogo dhidi ya mwandishi huyu.

5.      Taarifa ambazo TEF tunazo, pia  zinadai kwamba kulikuwa na mpango wa polisi wa “kuwashughulikia waandishi wa habari watatu” (Mwangosi) akiwa mmojawapo na hilo lilionekana likitekelezwa kwa polisi kumshambulia mwandishi huyo, baadaye alipoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha.

6.      Hili linatiliwa nguvu na tukio jingine la polisi kumpiga na kumjeruhi  mwandishi mwingine, Godfrey Mushi ambaye ni mwakilishi wa gazeti la Nipashe mkoani Iringa. Mwandishi wa tatu ambaye hadi tunapoandika taarifa hiyo yumo katika mpango wa ‘kushughulikiwa na polisi’ ni Francis Godwin ambaye ni mwandishi wa habari wa kujitegemea.

7.      Vitendo vya aina hii havivumiliki na havipaswi kuachwa kuendelea kwani ni hatari kwa ustawi wa demokrasia na uhuru wa habari nchini. Hatuwezi kuendelea katika mazingira ambayo polisi wanageuka kuwa chombo cha mauaji ya raia badala ya kuwa walinzi wa raia.

8.      Kwa maana hiyo, mbali na uchunguzi ambao utafanywa na polisi, tunatoa wito kwa Serikali kuunda chombo huru, ambacho kitabaini ukweli, na matokeo yake yatangazwe kwa umma, huku wahusika wa aibu hiyo wakichukuliwa hatua za kisheria. Tunasema hivyo, tukifahamu kwamba tayari kuna jitihada za kuficha ukweli na kueneza propaganda za uongo kuhusu tukio zima.

9.      Mwenendo wa aina hii wa chombo cha dola kuamua kutumia silaha kuua na baadaye kupanga mbinu chafu za kuficha ukweli ni hatari kwa Taifa, na unaiweka demokraisia ya nchi yetu njia panda, huku tukielekea katika hatari ya Taifa kutumbukia katika uovu.
IMETOLEWA NA:
NEVILLE MEENA,
KATIBU MKUU – JUKWAA LA WAHARIRI TANZANIA (TEF)
SEPTEMBA 3, 2012

KIFO CHA MWANDISHI TANZANIA: POLISI WATAKIWA KUWAJIBIKA
Waandishi wataka uongozi wa jeshi la polisi Tanzania kuwajibika kuanzia kamanda wa polisi wa mkoa na uongozi wa makao makuu akiwamo -IGP, Saidi Mwema. Viongozi wa vyama vya siasa, wanaharakati, waandishi wa habari na wananchi wa kawaida jijini Dar es salaam,   wamezungumzia  tukio la kuuwawa kwa mwandishi mmoja wa habari Daudi Mwangosi katika vurugu zilizotokea jumapili mkoani Iringa zilizohusisha jeshi la polisi na wafuasi wa chama cha upinzani cha CHADEMA. Watu wengi waliohojiwa kuhusu kifo cha mwandishi huyo walidai kuwa mauaji hayo yametokana na polisi kutumia nguvu kupita kiasi, huku wakitaka tume huru iundwe ili kufanya uchunguzi wa kina wa chanzo kilichopelekea kifo cha mwandishi huyo.

Wakati huo huo jukwaa la wahariri kwa kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania, wameunda timu ya uchunguzi wa suala hilo  ambayo itakwenda mkoani Iringa ili kubaini ukweli wa tukio hilo. Lengo la uchunguzi huo ni kuweka kumbukumbu sahihi ya tukio hilo. Katika tamko lake Jumatatu, jukwaa hilo la wahariri limesema tukio la mauaji ya mwandishi wa habari linaiingiza Tanzania katika  historia mbaya ya ukiukwaji na ukandamizwaji wa uhuru wa habari, kwani ni kwa mara ya kwanza nchi inashuhudia mwandishi wa habari akiuwawa wakati akitekeleza majukumu ya kazi yake Naye kaimu katibu mkuu wa chama cha UDP, Isaac Cheyo ametaka jeshi la polisi kuacha kutumia nguvu kupita kiasi wakati wa kutuliza ghasia. Amawataka polisi kuacha kutumika jeshi hilo kama chombo cha kuweka mbele maslahi ya watawala badala ya umma wa watanzania.

Pia mwenyekiti wa chama cha siasa cha NLD Dk.Emmanuel Makaidi, ametaka kuwepo kwa chombo huru cha kuchunguza matukio yanayohusisha jeshi la polisi kuliko ilivyo hivi sasa, jeshi kuunda timu ya uchunguzi kujichunguza yenyewe. Daudi Mwangosi licha ya kuwa mwakilishi wa kituo cha televisheni cha channel Ten cha jijini Dar es salaam alikuwa mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoani Iringa. Waandishi wametaka uongozi wa jeshi la polisi nchini Tanzania kuwajibika kuanzia kamanda wa polisi wa mkoa na uongozi wa makao makuu, akiwamo Mkuu wa Jeshi la Polisi -IGP, Saidi Mwema. Mwandishi huyo wa habari anatarajiwa kuzikwa jumanne Tukuyu Mkoani Mbeya.






No comments:

Post a Comment