ALEX MGONGOLWA |
Kamati ya Sheria, Maadili
na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilikutana
jana (Septemba 10 mwaka huu) ili kupitia na kutoa uamuzi/ushauri kwa masuala
mbalimbali yaliyowasilishwa mbele yake.
Wajumbe sita kati ya saba
waliopo walihudhuria kikao hicho chini ya Mwenyekiti Alex Mgongolwa. Wajumbe
hao ni Hussein Mwamba, Imani Madega, Ismail Aden Rage, Llyod Nchunga na Omari
Gumbo.
USAJILI/PINGAMIZI DHIDI YA
WACHEZAJI
Kwa mujibu wa Ibara ya
18(3) ya Kanuni za Hadhi na Uhamisho wa Wachezaji wa Kimataifa za FIFA, Yanga
ilifuata taratibu zote katika kumsajili Mbuyu Twite, hivyo ni mchezaji wake
halali. Hata hivyo, kwa vile Yanga imekiri kuwa mchezaji huyo alichukua dola
32,000 za Simba na kukiri kuzirejesha, kwa msingi wa kanuni ya Fair Play,
Kamati imeipa Yanga siku 21 iwe imelipa fedha hizo Simba.
Kwa mujibu wa Ibara ya
44(3) ya Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za TFF, Yanga ilifuata taratibu zote
katika kumsajili Kelvin Yondani, hivyo ni mchezaji wake halali. Kwa vile Simba
imesema mchezaji huyo vilevile alisaini mkataba na klabu yao, imetakiwa kupitia
mamlaka nyingine kuthibitisha hilo, na baada ya uthibitisho iwasilishe
malalamiko yake kwenye Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, au
mamlaka zozote za kisheria kwa mujibu wa madai/lalamiko husika.
Mchezaji Musa Hassan Mgosi
ameombewa usajili Ruvu JKT kutoka DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Congo (DRC), na Ayoub Hassan Isiko ameombewa usajili Mtibwa Sugar kutoka Bull
FC ya Uganda. Wachezaji hao hawaruhusiwi kuchezea timu hizo mpaka Hati zao za
Uhamisho wa Kimataifa (ITC) zitakapokuwa zimepatikana.
4. TOTO DHIDI YA KAGERA SUGAR KUMSAINI ENYINNA DARLINTON ARIWODO
Toto Africans ilipinga
usajili wa Enyinna Darlinton kwa timu ya Kagera Sugar kwa vile bado ina mkataba
wa mchezaji huyo ambao unamalizika mwakani.
Kwa upande wake Kagera
Sugar ilisema imemsaini mchezaji huyo kwa vile Toto Africans imeshindwa kumlipa
mshahara ambapo kuna makubaliano rasmi kati ya Ariwodo kuwa klabu hiyo
ikishindwa kumlipa mshahara anaruhusiwa kuondoka.
Uamuzi wa Kamati ni kuwa
Ariwodo ni mchezaji halali wa Kagera Sugar kwa vile Toto Africans ilishindwa
kutimiza masharti ya mkataba.
Redondo ameidhinishwa
kuchezea Simba kwa kuzingatia mchezo wa haki na uungwana (Fair Play) baada ya
klabu hiyo na ile ya Azam kufikia makubaliano kuhusu mchezaji huyo.
Yanga ilikiri kutolipa ada
ya uhamisho ya sh. milioni 5 kama walivyokubaliana na Kagera Sugar. Awali
waliipa Kagera Sugar hundi iliyogonga mwamba benki (bounced cheque). Shauri
hilo lilimalizwa kwa Yanga imetakiwa kulipa fedha hizo ndani ya siku 21 kuanzia
Septemba 10 mwaka huu.
7.
SUPER FALCON DHIDI YA
EDWARD CHRISTOPHER KUSAINI SIMBA
Simba imepewa siku 21
kuanzia Septemba 10 mwaka huu iwe imeilipa Super Falcon fedha za matunzo
(compensation) kwa vile ndiyo iliyomlea mchezaji Edward Christopher
aliyesajiliwa katika klabu hiyo.
8.
TOTO AFRICANS DHIDI YA
MOHAMED SOUD KUSAJILIWA COASTAL UNION
Toto Africans iliweka
pingamizi kwa maelezo kuwa bado ina mkataba na mchezaji huyo. Hivyo kwa msingi
wa Fair Play, mchezaji huyo ameidhinishwa Coastal Union baada ya makubaliono
kati ya klabu.
9.
ROLLINGSTONE DHIDI YA KIGI
MAKASSY KUSAJILIWA SIMBA
Simba imetakiwa kuilipa
Rollingstone gharama za matunzo ilizoingia wakati ikiwa na mchezaji huyo kwa
kuzingatia kanuni za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
10.
SUPER FALCON DHIDI YA
SULTAN JUMA SHIJA KUSAJILIWA COASTAL UNION
Uamuzi wa Kamati ni kuwa
Shija atachezea Coastal Union, na kwa vile yuko chini ya umri wa miaka 23,
Coastal Union itailipa Super Falcon fidia ya fedha ilizotumia kumhudumia
mchezaji huyo.
11.
AFRICAN LYON DHIDI YA RAZAK
KHALFAN KUSAINI COASTAL
Lyon imesema bado ina
mkataba na mchezaji huyo. Kamati imebaini kuwa mkataba wa mchezaji huyo na Lyon
umemalizika, hivyo ni mchezaji halali wa Coastal Union.
12.
FLAMINGO DHIDI YA KELVIN
FRIDAY KUSAJILIWA AZAM
Friday ruksa kucheza Azam,
lakini klabu hiyo imepewa siku 21 kuanzia Septemba 10 mwaka huu kuilipa
Flamingo gharama za kuvunja mkataba.
13.
SUPER FALCON DHIDI YA
ROBERT JOSEPH MKHOTYA KUSAINI AFRICAN LYON
Lyon imeagizwa kuilipa
Super Falcon sh. milioni moja ikiwa ni fidia ya kuvunja mkataba wa mchezaji
huyo ambaye imemsajili. Fedha hizo zitalipwa kwa awamu nne kutokana na makato
ya mlango yatakayofanywa na TFF. Falcon itapokea malipo hayo kupitia TFF.
14. OLJORO JKT DHIDI YA OTHMAN HASSAN KUSAJILIWA COASTAL
Kwa mujibu wa rekodi za
TFF, mkataba wa mchezaji huyo na Oljoro JKT unamalizika mwakani. Hivyo, Othman
Hassan ni mchezaji halali wa Oljoro JKT kwa vile bado ana mkataba na klabu
hiyo.
15.
YANGA DHIDI YA SIMBA KUACHA
WACHEZAJI WANNE
Kamati imetupa pingamizi
hizo kwa vile hakuna malalamiko yoyote kutoka kwa wachezaji juu ya kuvunjiwa
mikataba yao. Wachezaji hao walioachwa na Simba ni Dan Mrwanda, Haruna Shamte,
Kanu Mbiavanga na Lino Masombo.
Ikiwa wachezaji hao
watakuwa na malalamiko kuhusu kuvunjiwa mikataba suala hilo litafikishwa katika
Kamati kwa ajili ya kusikilizwa na kutolewa uamuzi.
SUALA LA UGOMBEA WA MICHAEL
WAMBURA KATIKA FAM
Michael Wambura aliomba
uongozi katika Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara (FAM) katika uchaguzi
uliofanyika Novemba mwaka jana. Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliondoa jina lake
kwa kukosa sifa ya kugombea nafasi hiyo.
Wambura hakuridhika na
uamuzi huo akapeleka shauri lake Kamati ya Nidhamu ya TFF. Kamati hiyo katika
uamuzi wake ilisema haina mamlaka ya kushughulikia shauri hilo. Baadaye Wambura
alikata rufani katika Kamati ya Rufani ya TFF ambayo ilimpa haki ya kugombea.
Kutokana na mkanganyiko huo
wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuwa na uamuzi wa mwisho katika masuala ya
uchaguzi ya wanachama wa TFF, na uamuzi wa Kamati ya Rufani kuhusu uchaguzi wa
mwanachama wa TFF, Sekretarieti ya TFF iliomba mwongozo wa kisheria kwa Kamati
ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji.
Kwa vile Kamati hizo mbili
(Uchaguzi na Rufani) haziko katika mtiririko wa moja kwa moja wa utoaji
maamuzi, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji iliishauri
Sekretarieti ya TFF kuliandikia Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA) ili kupata muongozo juu ya suala hilo.
Katika muongozo wake, FIFA
ilitoa maoni kuwa kwa mujibu wa Katiba ya TFF chombo cha mwisho cha rufani
katika masuala ya uchaguzi kwa wanachama wa TFF ni Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
Hata hivyo, FIFA ilishauri kuwa si vizuri chombo kimoja kikawa msimamizi wa
uchaguzi, na chenyewe tena ndiyo kiwe cha mwisho katika uamuzi kwenye uchaguzi
husika.
Hivyo, Kamati ya Sheria,
Maadili na Hadhi za Wachezaji imetoa mapendekezo mawili kwenda Kamati ya
Utendaji kwa ajili ya marekebisho ya Katiba ili kiwepo chombo kingine cha
rufani pale mgombea anapopinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
Mapendekezo hayo ni; Iundwe
Kamati ambayo itakuwa inasikiliza rufani zote zinazotokana na uamuzi uliofanywa
na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, hivyo Kamati ya Uchaguzi ya TFF isiwe chombo cha
mwisho cha uamuzi kwa rufani zinazotokana na uchaguzi wa wanachama wa TFF.
AU. Rufani zote zinazotokana na uchaguzi wa wanachama wa TFF
zisikilizwe na Kamati ya Rufani ya TFF. Kwa maana hiyo Kamati ya Rufani ya TFF
ndiyo kiwe chombo cha mwisho kwa wasiokubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi
ya TFF kuwasilisha malalamiko yao.
Alex Mgongolwa
Mwenyekiti
Kamati ya Sheria, Maadili
na Hadhi za Wachezaji
No comments:
Post a Comment