USAFIRI wa treni jijini Dar es
Salaam kutoka Ubungo Maziwa kuelekea katikati ya Jiji la Dar es Salaam
(Stesheni ya Treni) umeanza leo rasmi baada ya kuzinduliwa na Waziri wa
Uchukuzi Mheshimiwa Dr. Harrison Mwakyembe. Treni ya kwanza imeondoka Ubungo
majira ya saa 12:00 asubuhi kuelekea katikati ya jiji, ambapo kwa mujibu wa maofisa
wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) treni hiyo imetumia wastani wa dakika 30
kufika katikati ya jiji.
Treni
iliyoanza kazi leo ina injini mbili (vichwa vya treni) moja ikiwa imefungwa
nyuma na nyingine mbele huku ikiwa na mabehewa sita, yaani matano ya abiria wa
kawaida (watu wazima) na moja likiwa ni maalumu kwa ajili ya kubeba wanafunzi. Nauli kwa kila abiria mmoja ni sh. 400 kwa
tripu huku wanafunzi wakitakiwa kulipa sh. 100.
Waziri
wa Uchukuzi, Mheshimiwa Dk Harrison Mwakyembe amezindua usafiri huo leo kama
majaribio akiwa pamoja na viongozi waandamizi kutoka TRC, Mamlaka ya Usafiri wa
Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), TAZARA pamoja na Polisi Kitengo cha Reli. Treni
hiyo imezinduliwa sambamba na treni ya TAZARA ambayo itafanya kazi kama ya
Ubungo, lakini yenyewe ikianzia eneo la TAZARA kuelekea Mwakanga.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo
Waziri Mwakyembe alisema atahakikisha treni hiyo inaendelea kufanya kazi ili
kuwasaidia kiusafiri wananchi wa Dar es Salaam ambao wamekuwa wakisumbuliwa na
kero ya usafiri hasa kwa foleni, ambapo hutumia muda mrefu njiani wakati wa kuingia
na kutoka jijini. Dr. Mwakyembe alisema jumla ya mabehewa 14 pamoja na injini mbili
zimekarabatiwa na mafundi wazalendo nchini, ambayo ndiyo yatakayokuwa yakifanya
kazi ya kusafirisha abiria kuingia na kutoka jijini kila asubuhi na jioni. Kwa
sasa treni moja imeanza kwa majaribio lakini baada ya uzinduzi mkubwa treni
mbili zitafanya kazi, na zitakuwa zikipishana njiani moja ikirudi na nyingine
ikienda.
Akifafanua zaidi alisema kitendo
cha mafundi wazalendo kufanya ukarabati kwa mabehewa na injini kimeokoa kiasi
kikubwa cha fedha za umma kwani ukarabati wote umetumia sh. bilioni 2.1 tu, wakati
kama Serikali ingelazimika kukodi injini gharama ingekuwa kubwa zaidi kwani bei
ya kukodi injini moja ya treni ni sh. milioni moja kwa siku. Hata
hivyo Waziri Mwakyembe amewataka Watanzania hasa abiria kuwa wavumilivu kwa
upungufu utakaojitokeza kwa safari za mwanzo kwani bado wanaendelea kufanya
marekebisho kadhaa, lakini baada ya muda mambo yatakaa sawa. Mwanatanga alikuwa
mmoja wa wasafiri walioizindua treni hiyo leo.
Mmoja
wa viongozi waandamizi wa TRC, alisema treni hiyo itafanya kazi kila siku
isipokuwa kwa siku za jumapili na siku kuu na itakuwa ikianza safari zake saa
12:00 asubuhi hadi saa sita mchana na kupumzika hadi saa 9:00 jioni,
itakapoendelea tena na safari zake hadi majira ya saa nne usiku. Behewa moja la
treni linauwezo wa kuchukua abiria 66 wakiwa wamekaa likiwa na milango minne,
feni, taa, muziki/redio, pamoja na mikanda maalumu ya kujishikia kwa abiria
ambao watakuwa wamesimama.
Aidha
mabehewa yote yana madirisha ya kutosha kuingiza na kutoa hewa ya kutosha.
Treni ilioanza kazi leo, ikitokea Ubungo ilikuwa ikisimama vituo vya eneo la
Mwananchi (relini), Tabata Relini, Buguruni Miamani, Tazara, Kariakoo Gerezani
(Kamata), na mwisho Kituo Kikuu cha Treni kilichopo jirani na Kituo cha Polisi
Kati (Katikati ya Jiji).
No comments:
Post a Comment