MAPEMA wiki hii, Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) kwa kushirikiana na Kamati ya Ligi kwa pamoja walitangaza kuahirisha
baadhi ya mechi za Ligi Kuu ya Bara ili kutoa nafasi kwa kituo cha luninga cha
SuperSport cha Afrika Kusini kuweza kuonyesha live baadhi ya mechi hizo.
SuperSport kupitia kampeni yake maalum iitwayo
SUPER WEEK, itaonyesha mechi hizo katika kile kinachoelezwa kuwa ni kuitangaza
Ligi Kuu ya Bara duniani kote. Mechi zilizoahirishwa ni mchezo namba 127,
ulipangwa kuzikutanisha Azam FC na African Lyon ambao ulipangwa kuchezwa jana
kwenye Uwanja wa Chamazi, mechi hii sasa itachezwa leo Alhamisi 11 Aprili
kwenye uwanja huo na itaonyeshwa live.
Mchezo mwingine ni ule namba 156 wa 10 Aprili,
mwaka huu kati ya Yanga na JKT Oljoro ambao sasa utachezwa Jumamosi ya 13
Aprili, mwaka huu ili kuipa nafasi SuperSport kuonyesha live mechi hiyo. Pia
mchezo namba 155 kati ya Azam na Simba sasa utachezwa 14 Aprili badala ya 13
Aprili mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kama ilivyo kwa Yanga.
Ikumbukwe hii ni zaidi ya mara mbili ndani ya
kipindi cha misimu miwili, kituo hiki kinafanya hivi BURE huku kikilazimisha
kupangua ratiba ya ligi kuu na kuziathiri baadhi ya timu.
TFF, KAMATI YA
LIGI WAVUNJA KANUNI YA LIGI NAMBA 9
Kutokana na
Yanga kuwa klabu ya kwanza kulalamikia jambo hili, mambo mengi yameweza kuibuka
na kubwa zaidi ni TFF na Kamati ya Ligi kuvunja kanuni namba 9 ya Ligi Kuu ya
Bara msimu wa 2012/13 inayoelezea mazingira ya kuahirishwa kwa mchezo.
Kanuni ya 9 ya
ligi inasema, Mchezo unaweza kuahirishwa kutokana na sababu yoyote kati ya
zifuatazo:-
(a) Endapo timu ya Taifa ina mchezo.
(b) Endapo timu inashiriki katika mashindano
ya Kimataifa na ina muda usiozidi siku sita kufikia mchezo wa Kimataifa;
(c) Sababu yoyote ya dharura au/ na yenye
msingi itakayokubaliwa na TFF.
(d) Matukio yasiyotarajiwa wala kusababishwa na
timu husika.
(e) Mchezo wowote ulioahirishwa chini ya
kipengele 9 (a),(b) na (c) utapangwa tena katika tarehe itakayoamuliwa na TFF
isipokuwa kama utaahirishwa chini ya kipengele 9 (d) utachezwa siku inayofuata
iwapo ratiba inaruhusu.
(f) Iwapo mchezo ulishaanza na kuvunjika kwa
sababu ya matukio ya dharura yasiotarajiwa wala kusababishwa na timu husika,
utapangwa kurudiwa kwa muda uliosalia, mabao yaliyofungwa katika mchezo huo,
Kadhalika kadi walizoonyeshwa wachezaji katika mchezo uliovunjika zitaendelea
kuhesabika.
(g) Taarifa ya maombi ya kuahirisha mchezo ni
lazima itolewe kwa maandishi si chini ya siku 14 kabla ya siku ya mchezo,
isipokuwa kwa sababu zilizo nje ya uwezo wa binadamu.
UKIUKWAJI WA
KANUNI ULIOFANYWA NA TFF, KAMATI YA LIGI
KUHUSU KANUNI YA 9.
Kama kanuni
inavyosema kwamba mchezo unaweza kuahirishwa kutokana na sababu yoyote kati ya
zifuatazo:-
(a)
Endapo timu ya Taifa ina mchezo.
UKWELI NI KWAMBA HAKUNA MCHEZO WOWOTE WA
TIMU YA TAIFA.
(b)
Endapo timu inashiriki katika mashindano ya Kimataifa na ina muda usiozidi siku
sita kufikia mchezo wa Kimataifa; AZAM PEKEE NDIYO INAYOSHIRIKI MICHUANO YA
KIMATAIFA NA HAIKUWA NA MCHEZO WIKI HII AMBAO UNGEILAZIMU KUPANGUA RATIBA.
(c)
Sababu yoyote ya dharura au/ na yenye msingi itakayokubaliwa na TFF.
LABDA HII YA
SUPERSPORT INGEWEZA KUWA SABABU YA MSINGI YA KUAHIRISHWA KWA MECHI HIZO, ENDAPO
MAKUBALIANO YANGEFIKIWA KATI YA KAMATI YA LIGI, KLABU NA TFF YENYEWE. UKWELI NI
KWAMBA, KLABU HAZIKUAFIKIANA NDIYO MAANA BAADHI VILABU KAMAYANGA NA
AFRICAN LYON VIMEJITOKEZA KUPINGA WAZI WAZI HAYO MABADILIKO.
(d)
Matukio yasiyotarajiwa wala kusababishwa na timu husika.
HAKUNA
MATATIZO YASIYOTARAJIWA AMBAYO YAMEJITOKEZA WALA KUSABABISHWA NA KLABU HUSIKA.
HAPA YAWEZA KUWA HALI YA HEWA YAANI MVUA KUBWA AU JAMBO LA KITAIFA LINALOWEZA
KUZUIA MIKUSANYIKO.
(e)
Mchezo wowote ulioahirishwa chini ya kipengele 9 (a),(b) na (c) utapangwa tena
katika tarehe itakayoamuliwa na TFF isipokuwa kama utaahirishwa chini ya
kipengele 9 (d) utachezwa siku inayofuata iwapo ratiba inaruhusu.
HAKUNA KITU
KAMA HICHO KINACHOENDANA NA UAHIRISHWAJI HUU WA SASA.
(f)
Iwapo mchezo ulishaanza na kuvunjika kwa sababu ya matukio ya dharura
yasiotarajiwa wala kusababishwa na timu husika, utapangwa kurudiwa kwa muda
uliosalia, magoli yaliyofungwa katika mchezo huo, Kadhalika kadi walizoonyeshwa
wachezaji katika mchezo uliovunjika zitaendelea kuhesabika.
HAKUNA KITU
KAMA HICHO KINACHOENDANA NA UAHIRISHWAJI HUU WA SASA
(g)
Taarifa ya maombi ya kuahirisha mchezo ni lazima itolewe kwa maandishi si chini
ya siku 14 kabla ya siku ya mchezo, isipokuwa kwa sababu zilizo nje ya uwezo wa
binadamu.
HAPA NDIPO
KWENYE UTATA, KWANI TFF KUPITIA MKURUGENZI WAKE WA MASHINDANO, SAAD KAWEMBA
ILITOA TAARIFA KWA NJIA YA BARUA PEPE KWENDA KWA WAJUMBE WA KAMATI YA LIGI KUHUSU KUAHIRISHWA KWA MECHI HIZO IJUMAA
ILIYOPITA YA 5 APRILI, 2013 SAA 9:50 ALASIRI. MUDA HUU HAUPO NDANI YA SIKU 14
KABLA YA SIKU YA MCHEZO. HAPA ILIPASWA TFF KUZITAARIFU KLABU JUU YA JAMBO HILI
SI CHINI YA 27 MACHI MWAKA HUU.
Jumapili ya 7
Aprili, mwaka huu, saa 1:32 usiku mtendaji mkuu wa kamati ya ligi bwana Silas
Mwakibinga alivitumia vilabu taarifa kwa njia ya barua pepe akivisihi
vizingatie mabadiliko ya ratiba kutokana na Super Week ambapo Super Sport
wataonesha michezo iliyotajwa na Bwana Saad Kawemba. Cha kushangaza kwanini
Bwana Mwakibinga hakuitisha kikao cha viongozi wa vilabu na kujadiliana juu ya
hayo mabadiliko ya ratiba ikiwa ni pamoja na kuvijulisha ujio mpya wa Super
Sport ?
Mbaya zaidi
klabu hizo, nyingine zikawa zinaomba nazo safari hii mechi zao zionyeshwe live
huku wakijua fika kwa kuonyesha live mechi hizo, SuperSport inajiingizia kiasi
kikubwa cha fedha. Kuonyeshwa live kwa mechi hizo, si sababu iliyo nje ya uwezo
wa binadamu.
KUTOKANA NA
KUTAMBUA HILO, NDIYO MAANA YANGA KUPITIA KATIBU MKUU WAKE, LAWRENCE MWALUSAKO
JUMATATU YA WIKI HII AMBAYO ILIKUWA 8 APRILI SAA 3:54 ASUBUHI ILIJIBU E-MAIL YA
KAWEMBA KWA KUSEMA HAIWEZI KUCHEZA JUMAMOSI BADALA YA JANA KWA KUWA TAYARI
WALISHAFANYA MAANDALIZI YA MCHEZO WA JUMATANO.
Pamoja na
Yanga kuwa na haki ya kukataa mechi yao kuahirishwa, bado TFF na Kamati ya Ligi
waliendelea kung’ang’ania mabadiliko hayo ili tu kuifurahisha SuperSport na
wengine WANAONUFAIKA na maonyesho ya mechi hizo live.
TFF, KAMATI YA
LIGI LAO MOJA
Kwa mchakato
huu wa kuipa nafasi SuperSport kuonyesha live mechi zake, inaonekana wazi
kwamba TFF na Kamati ya Ligi wapo pamoja na hawazipi klabu uhuru wa kuamua
mambo yake.
Kwa mfano
Yanga imekataa kucheza mechi yake wikiendi badala ya jana, lakini imelazimishwa
kucheza siku hiyo huku Kamati ya Ligi ikiwa kimya isiseme lolote kwa kuitetea
Yanga au kuweka mambo sawa kidemokrasia.
Inaonekana
wazi Kamati ya Ligi ipo kwa kuinufaisha na kuisimamia TFF kufanya jambo lake
lolote kwa klabu za ligi kuu bila yenyewe kuhoji hali yoyote ile. Yawezekana
Kamati ya Ligi ndiyo kama isiyoweza kuamua jambo lake lolote ndani ya TFF
tofauti na kamati nyingine.
Ili mechi ionyeshwe live, ni lazima klabu
husika, TFF na Kamati ya Ligi wote wakubaliane kufanya hivyo. Kwa hili la SUPER
WEEK mambo hayakuwa hivyo inavyotakiwa.
MSIMAMO WETU
Bado tunaendelea kupambana kuhakikisha kanuni
zinafuatwa katika kila jambo linalotokea nchini kwani FAIR PLAY ndicho kitu
pekee kinachoweza kutuletea maendeleo katika soka.
Kauli kuwa SUPER WEEK inafanyika ili
kuitangaza ligi yetu, inapaswa kuachwa na kuitaka SuperSport kulipia matangazo
hayo iwe kwa moja kwa moja au kwa udhamini kama inavyofanya Kenya na kwingineko
Afrika ambako kuna ligi dhaifu kuliko ya Tanzania Bara.
Tunachokifanya ni kujaribu kuziamsha klabu
kufahamu haki zao na kuweza kunufaika nazo, kwani kwa kufanya hivyo timu
zinaweza kupata fedha nzuri za maandalizi na kufanya ushiriki wake katika ligi
kuwa wenye mafanikio na kutoa ushindani kwa klabu zenye hali nzuri kifedha.
SOURCE NI SHAFFII DAUDA
No comments:
Post a Comment