BM BARBERSHOP KINONDONI

Wednesday, August 29, 2012

ASKOFU PASCHAL KIKOTI WA JIMBO LA MPANDA AFARIKI DUNIA

Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Mpanda Paschal Williamu Kikoti (55) amefariki dunia usiku wa kuamkia jana 28/08/2012 kwa ugonjwa wa shinikizo la damu katika hospitali ya Bugando Mjini Mwanza.
 
Makamu wa Askofu wa Jimbo la Mpanda Padre Patrick Kasomo ametoa taarifa hiyo katika kanisa kuu la Jimbo la Mpanda muda mfupi baada ya kifo hicho kwa mamia ya wamumini waliokuwa wamekusanyika hapo majira ya nne usiku. Aliwaeleza waumini hao kuwa Askofu Kikoti alipatwa na ugonjwa wa shinikizo la damu siku ya jumapili Agosti 27 mwaka majira ya saa moja asubuhi wakati akioga na kuanguka ghafla akiwa bafuni akioga kisha kupoteza fahamu. Baada ya kupatwa na tukio hilo alikuja kugunduliwa baada ya Mapadri na Masister walipokuwa wametoka kwenye ibada ya misa ya kwanza majira ya saa mbili na nusu asubuhi huku akiwa kapoteza fahamu.
Makamu wa  Askofu Jimbo Katoriki Mpanda Padre Patrick Kasomo
Baraza la Maasikofu lilitafuta usafiri wa ndege siku hiyohiyo na kumchukua jimboni Mpanda na kumsafirisha hadi hospitali ya rufaa ya Bugando Mkoani Mwanza kwa ajili ya kupatiwa matibabu hadi hapo jana majira ya saa 2:30 alipofariku dunia. Baada ya makamu wa Askofu Padre Kasomo kutoa taarifa hiyo waumini wa kanisa hilo waliangua vilio na baadhi yao kupoteza fahamu.
Mmoja wa Waumini wa Kanisa Katoriki Jimbo la Mpanda alipoteza fahamu baada ya kupata taarifa ya kifo cha Askofu wao Paschal Kikoti iliyotolewa na Makamu wa Askofu wa Jimbo la Mpanda Padri Patrick Kasomo
WASIFU WA ASKOFU PASCHAL KIKOTI
Marehemu Askofu Paschal Kikoti alizaliwa Mkoani Iringa katika Parokia ya Nyabula mkoani Iringa mwaka 1957 na kupewa daraja la upadre tarehe 29/6/1988 huko mkoani Iringa. Alipewa daraja la uaskofu 14/01/2001 na kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo jipya la Mpanda. Padre Kasomo ameeleza kuwa Askofu Kikoti mwili wake utawasili siku ya Alhamisi ukitokea Mwanza kwa njia ya usafiri wa ndege na anategemewa kuzikwa siku ya Jumamosi ya wiki hii ndani ya kanisa kuu la Mpanda. 
Waumini wa Kanisa Katoriki Jimbo la Mpanda wakimlilia Askofu wao Paschal Kikoti mara baada ya kutangaziwa na makamu wa Askofu wa Jimbo la Mpanda Padri Patrick Kasomo kuwa Askofu Paschal Kikoti amefariki
 
Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi

No comments:

Post a Comment