Zacharia Hans Pop Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Simba
KLABU ya Simba imesema itamfikisha
mahakamani mchezaji Mbuyu Twite wa klabu ya APR kwa kosa la kuwatapeli na
kukubali kusajiliwa na Yanga.Akizungumza mjini Dar es Salaam leo, mwenyekiti wa
kamati ya usajili ya Simba, Zakaria Hanspope alisema, Twite alishapokea fedha
za Simba na kukubali kuingia nayo mkataba, hivyo hawezi kwenda kinyume. Hanspope
alisema kilichofanywa na Yanga kumshawishi mchezaji huyo arejeshe fedha za
Simba na kupokea fedha zao ni cha kihuni na hawawezi kukivumilia.
Alisema kama ni kurejesha fedha zao,
anayepaswa kufanya hivyo ni Twite mwenyewe na si klabu ya Yanga. Hanspope
alisema wao waliingia mkataba na Twite kupitia klabu yake ya APR na Shirikisho
la Soka la Rwanda, hivyo walipaswa kuomba hati ya uhamisho kutoka Rwanda na si
Congo. "Haya mambo lazima ufike wakati yafikie mwisho. Haiwezekani klabu
imesikia kwamba mchezaji amesajiliwa na klabu fulani na yenyewe inamfuata
kuzungumza naye,"alisema.
Hanspope alisema bado wanaamini
kwamba Twite ni mchezaji wao na kama itatokea vinginevyo, watapambana hadi haki
yao ipatikane.Naye mjumbe wa kamati ya utendaji ya Yanga, Abdalla Bin Kleb
alijigamba kuwa, hawana mjadala wowote na Simba kuhusu Twite kwa vile wamefuata
taratibu zote katika kumsajili. Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Rwanda leo,
Bin Kleb alisema anaashukuru kwamba amekamilisha vyema kazi aliyotumwa na
viongozi wenzake na kwamba Twite sasa ni mali ya Yanga.
No comments:
Post a Comment