MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo
inatarajia kutoa hukumu ya Kesi ya Uhujumu Uchumi na Kuisababishia Serikali hasara
ya Euro 2 milioni, inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania, nchini Italia
Profesa Costa Mahalu na Ofisa Utawala wa ubalozi huo, Grace Martin. Profesa
Mahalu na Martin wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwamo ya uhujumu uchumi na
kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60, katika mchakato wa ununuzi
wa jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Italia. Hukumu ya kesi hiyo iliyokuwa
ikinguruma mahakamani hapo kwa miaka kadhaa sasa, inatarajiwa kusomwa leo na
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ilvin Mugeta ambaye amekuwa akiisikiliza.
Awali, hukumu hiyo ilipangwa kusomwa
Julai 11, mwaka huu lakini iliahirishwa kutokana na Hakimu Mugeta kukabiliwa na
majukumu mengine. Kesi hiyo iliahirishwa na Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana na
kupanga kuwa hukumu hiyo itasomwa leo.
Kiongozi wa jopo la mawakili wa
washtakiwa hao, Mabere Nyaucho Marando alisema jana kwamba anaamini kesi hiyo
ambayo imechukua muda mrefu, leo inafikia mwisho kwa Mahakama kutoa hukumu. Hata
hivyo, hakutaka kuizungumzia kwa undani
hukumu ya leo badala yake alisema kuwa wanachosubiri ni kuona itakavyokuwa, ila wako
tayari kwa matokeo yoyote. “Sisi tunasubiri kuona hukumu ya Mahakama, kwani imekuwa ikisubiriwa sana. Kama akiachiwa tutafurahi na tutakunywa wine (mvinyo) usio na kilevi
kama akifungwa basi tutapiga magoti kumwombea,” alisema Marando kwa utani huku
akicheka. Alisisitiza kuwa uamuzi wa mwisho ni wa Mahakama na kwamba mambo
mengine yatafuata baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo. Kwa upande wake, Wakili
wa Serikali, Shadrack Kimaro alisema katika makosa kama hayo yanayowakabili washtakiwa hao, ikiwa watapatikana na hatia adhabu yake inaweza kuwa kifungo kisichozidi miaka 15 jela.
Alisema kwa mujibu wa Kifungu cha 60 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi,

Kifungu kidogo cha pili, Mahakama inaweza kutoa amri nyingine ikiwamo mshtakiwa kulipa fidia. Hukumu ya kesi hiyo leo inasubiriwa kwa shauku si tu na Profesa Mahalu na wenzake ambao wangependa kujua hatima yao, bali pia na umma wote wa Watanzania ambao umekuwa
ukiifuatilia kwa muda wote. Wakati wa utetezi, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ambaye ununuzi wa jengo hilo ulifanyika wakati wa uongozi wake, alipanda kizimbani na kumtetea Profesa Mahalu na mwenzake, akidai kuwa mchakato wa ununuzi wa jengo hilo ulifuata sheria. Mkapa katika ushahidi wake wa utetezi licha ya kudai kuwa mchakato huo
ulifuata taratibu na kwamba ni yeye aliyebariki, pia alimmwagia sifa kedekede Profesa Mahalu akidai kuwa ni kiongozi mwadilifu na mwaminifu katika historia yake ya utumishi wa
umma. Akiongozwa na mmoja wa mawakili wanaomtetea Mahalu na mwenzake, Alex Mgongolwa, Mkapa alieleza mchakato wote wa ununuzi wa jengo hilo na malipo yake kwa kuwa lilinunuliwa kwa maagizo ya Serikali yake.
Upande wa mashtaka ulidai kuwapo kwa
uhujumu uchumi kutokana na kuwapo kwa mikataba miwili wakati wa ununuzi wa
jengo hilo, Mkapa alidai kuwa aliifahamu mikataba yote hiyo na malipo kufanyika
kupitia akaunti mbili tofauti. Alieleza kushangazwa kwake kusikia kuwa aliyekuwa
Katibu Mkuu Kiongozi wakati huo, Martin Lumbanga katika ushahidi wake alidai
kuwa hakujua mchakato wa ununuzi wa jengo hilo, akisema hajui ni kwa nini Lumbanga
alisema hivyo. Mbali na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
ambayo wakati wa ununuzi wa jengo hilo, Rais Jakaya Kikwete ndiye aliyekuwa
waziri wake. Mkapa alisema wizara nyingine zilizohusika ni Ujenzi na ile ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Alidai kuwa wizara zote hizo zilituma wataalamu wake kwenda kufanya tathmini ya
thamani ya jengo hilo kabla ya ununuzi wake. Alisema taarifa iliyotolewa na
Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo, Kikwete bungeni juu ya ununuzi wa jengo hilo
ni sahihi. Pamoja na mambo mengine, taarifa hiyo inaeleza kuwa jengo hilo lilinunuliwa
kwa Sh.2.9 bilioni na kwamba hati za umiliki wake zilishawasilishwa wizarani na
kupelekwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). “Maneno hayo ni sahihi. Hayo ndiyo ninayoyajua
mimi,” alisema Mkapa na kuongeza kwamba hajawahi kupata malalamiko kutoka
Italia kuhusu ukiukwaji wa sheria wakati wa mchakato wa ununuzi wa jengo hilo
wala kwa mmiliki akidai kuwa alilipwa pungufu ya makubaliano.
Akijibu swali la Wakili Alex Mgongolwa
kama alishapata malalamiko yoyote kutoka kwa CAG kuhusu ununuzi wa jingo hilo,
alijibu kuwa hajawahi kupokea malalamiko hayo. Akijibu swali la Wakili wa Serikali,
Ponsiano Lukosi kama aliwahi kuuliza ni kwa nini mwenye jingo alitaka alipwe
kupitia mikataba miwili, Mkapa alijibu kuwa hakuuliza kwa kuwa alichokuwa
anahitaji ni kupata jengo. Akijibu swali kwamba kama lengo la mwenye jengo kutaka
kulipwa kwa mikataba miwili lilikuwa ni kukwepa kodi ya Serikali ya nchi yake,
Mkapa alijibu: “Hilo ni tatizo lake na nchi yake, mimi nilikuwa nataka nyumba
na nimepata nyumba, nasema Alhamdulillah.”
Pia Mkapa alisema anamshangaa wakili
wa Serikali kudai kuwa pesa hizo kulipwa kwa awamu mbili kunaonyesha kwamba
Profesa Mahalu alikuwa na lengo za kuzichukua na kuzitumia kwa masilahi yake...
“Mimi nitashangaa sana kusikia hivyo na hasa nitakushangaa wewe maana Profesa
(Mahalu) mimi namwamini.” Utetezi wa Profesa Mahalu Katika utetezi wake, Profesa
Mahalu alikana mashtaka hayo na kudai kuwa alipofika katika ubalozi huo alikuta
ofisi hizo zikiwa na hali mbaya hali iliyosababisha kutoa fedha zake za mfukoni
na kununua samani zenye hadhi ya ofisi ya ubalozi. Alisema aliyekuwa Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Kikwete pia alifika katika ofisi za
ubalozi huo na kushuhudia hali hiyo mbaya na kwamba aliunga mkono hoja yake
kwamba ofisi hiyo ni mbovu na akashauri ipatikane ofisi yenye hadhi ya ubalozi.
Alisema mwanzoni mwa Juni, 2001 Katibu Mkuu wa Wizara hiyo alimpigia simu akimpongeza
kwamba maombi ya wizara yao katika bajeti ya kutaka kila ofisi ya ubalozi
inunue jengo lake itapitishwa na Bunge. Alidai kuwa Katibu Mkuu alimtaka yeye
na maofisa wengine wa ubalozi kuanza kutafuta majengo.
Alisema baada ya hapo aliwaagiza
maofisa wake kwenda kutafuta majengo ndani na nje ya Jiji la Rome kwa ajili ya
kulinunua.Martin katika utetezi wake alidai kuwa, Balozi Mahalu hakuisababishia
Serikali hasara ya Euro 2 milioni, bali alileta faida kwa taifa kwa kuwa na
jengo zuri na kwamba anahitaji kupewa shukrani. Akiongozwa na Wakili
Marando kujitetea dhidi ya tuhuma zinazomkabili, Grace alidai: “Mheshimiwa kwa ufahamu wangu, Balozi Mahalu mashtaka yote sita yanayomkabili hakuyatenda, aliwasilisha mikataba miwili kama taarifa iliyofanyika kihalali.” Pia Martin alihoji sababu ya upande wa Jamhuri
kutomleta mmiliki wa jengo hilo la ubalozi kukana risiti hiyo au Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea kuulizwa juu ya ununuzi wa jengo hilo akidai walikwenda nchini humo kufanya uchunguzi. Chanzo: Mwananchi.

No comments:
Post a Comment