BM BARBERSHOP KINONDONI

Wednesday, August 15, 2012

MAREHEMU ABUU SEMHANDO-NGUZO AMBAYO HAITASAHAULIKA TWANGA PEPETA


Mkurugenzi wa ASET mama Asha Baraka anasema, Semhando ni mwanamuziki ambaye amechangia mafanikio ya bendi hiyo kwa asilimia kubwa kupita kiasi kutokana na kujitoa muhanga na ndiyo maana amekaa kwa muda mrefu tangu ajiunge na Twanga Pepeta mwaka 1998 akitokea bendi ya Diamond Sound. “Abuu aliitumikia Twanga kama mali yake binafsi! Kifo cha Semhando kilinitia simanzi mimi binafsi na wapenzi wote wa Twanga Pepeta ndani na Nje ya Nchi. “Kwangu Semhando alikuwa ni chachu ya mafanikio ya albamu zote 10 ambazo tumezitoa kutokana na kushiriki katika kuandaa muziki na kusimamia nidhamu ya bendi jambo ambalo limezidi kutupaisha katika mafanikio kwa kweli ni majonzi makubwa kumpoteza kutokana na kuwa kiungo katika kila jambo lililohusu Twanga Pepeta,” amsema Asha na kuongeza: “Sidhani kama tutapata mtu mwenye uwezo aliokuwa nao mwanamuziki huyo kutokana na kipaji cha kuongoza alichokuwa nacho, kwa kweli tutamkumbuka sana kutokana na pengo alilotuachia kwetu ASET na medani nzima ya muziki nchini.” Kifo chake pengine kwa wanafamilia kilimgusa sana binti yake Sharifa ambaye siku ambayo alikuwa anatakiwa kufungishwa ndoa na baba yake ndiyo mauti yalipomkuta na kufanya sherehe hizo kugeuka msiba. Tutaendelea kumkumbuka Marehemu Abuu Ally Semhando sisi familia ya Baraka.
MKURUGENZI WA ASET ASHA BARAKA AKITOA HISTORIA YA MAREHEMU ABUU SEMHANDO
 WASIFU WA MAREHEMU ABUU ALLY SEMHANDO “LOKASSA” KWA MUJIBU WA ASHA BARAKA
 Abuu Ally Semhando maarufu ‘Lokassa’ au ‘Baba Diana’ ambaye alikuwa mpiga drum na Meneja wa bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’. Abuu Semhando alizaliwa mwaka 1953 Kijiji cha Kibanda Wialaya ya Muheza Mkoani Tanga na kufariki siku ya Jumamosi 18 December 2010,
ENZI ZA ABUU SEMHANDO NDANI YA TWANGA PEPETA
Abuu Ally Semhando "Lokassa" alianza shughuli za muziki mwanzoni mwa miaka 1970 akiwa na Tanga International na baadaye kwenda kuasisi bendi ya Super Matimila na Orchestra Tomatoma kabla ya kutua Safari Sound Orchestra (OSS) na Vijana Jazz ‘ Pamba Motto’ ambapo alikuwa Katibu hali kadhalika akiwa mwasisi wa bendi ya Tanza Muzika.
ABUU SEMHANDO WA PILI KULIA WALIOKAA AKIWA NA VIJANA JAZZ PICHA KWA HISANI YA MZEE JOHN KITIME
Abuu Ally Semhando na Mzee Hamza Kalala ni miongoni mwa wanamuziki waanzilishi wa bendi ya Super Matimila na ndio waliomkaribisha FanFan na marehemu Dk. Remmy Ongala; Abuu alishiriki kupiga drums kwa kiwango kikubwa katika nyimbo nyingi ambazo ziliiletea mafaniko bendi hiyo. Akiwa katika bendi hiyo Kasaloo Kyanga alimpa jina la Locassa na anatajwa na Kyanga katika wimbo ‘Alimasi’ wa bendi ya Matimila. Licha ya kuwa mpiga drums, Abuu alikuwa ni mwanamuziki mwenye kipaji kikubwa cha uongozi wa bendi (Music Band Management) na kushiriki katika kuandaa muziki ili kuhakikisha bendi yoyote aliyopitia inapata mafanikio jambo ambalo lilimjengea umaarufu katika kila bendi aliyopitia.
ABUU SEMHANDO WA PILI KUTOKA KLUSHOTO WALIOSIMAMA ENZI ZA SUPER MATIMILA
Historia inaonyesha kuwa bendi alizowahi kupitia akiwa kiongozi baada ya kuondoka kwake ziliyumba na zingine kutokomea kabisa katika medani ya muziki wa dansi, siri ya mafanikio na kipaji hicho cha uongozi akiwa amekufa nayo. Lakini si Matimila pekee yake hata alipokuwa na Vijana Jazz ‘Sagha Rhumba’ ambako alikuwa Katibu chini ya Hemed Maneti alikuwa mmoja wanamuziki walioshiriki katika kuiletea mafanikio kwa miaka yote hiyo kabla ya kujiondoa, ambapo alikua muasisi wa ‘Vijana Day’. Abuu alishiriki kwa kiwango kikubwa kutengeneza nyimbo za Vijana Jazz akiwa na waimbaji kina Hemed Maneti, Saidi Hamis, Fred Benjamin, Cosmas Chidumule na Kida Waziri, huku wapiga vyombo wakiwa Kurwa Milonge, Hamza Kalala, Hassan Dalali, Aggrey Ndumbalo, Disfa Semhando (mdogo wake), Shabaan Yohana (Wanted) na wengine wengi.

MAREHEMU SULEIMANI MBWEMBWE NA MZEE HAMZA KALALA WALIFANYA KAZI NA SEMHANDO PIA
Akiwa na wanamuziki hao ambao ni baadhi tu ya kundi alilokuwa nalo, walishiriki kutengeneza nyimbo kali kama ‘Bujumbura’, ‘Mary Maria’, ‘Tambiko la Pambamoto’, ‘Mundinde’, ‘Ali Hassan Mwinyi Apewe Kura za Ndiyo’, ‘Wifi Zangu Wananinyanyasa’, ‘Penzi Haligawanyiki’ na nyingine nyingi nzuri kupindukia ambazo zilitikisa anga ya muziki huo chini ya Hemed Maneti (Kiongozi), Hamza Kalala (Kiongozi Msaidizi) na Abuu Semhando mwenyewe (Katibu). Katika kudhihirikisha uwezo aliokuwa nao alipojing’atua Vijana Jazz ndipo jinamizi na anguko la bendi hiyo lilipoanza kuinyemelea tangu hapo bendi hiyo haijafanya vyema katika medani ya muziki nchini.
 

Wakimzungumzia marehemu baadhi ya wanamuziki ambao aliwahi kufanya nao kazi ni John Kitime ambaye anasema, atamkumbuka mwanamuziki huyo kwa ucheshi wake kwa kuwa alimpokea mjini na kumtafutia malazi jijini mwaka 1989 wakati anajiunga na Vijana Jazz akitokea Tuncut Almasi ya Iringa.
MAREHEMU ABUU AKIWA KAZINI TWANGA PEPETA KUCHEKA NA UTANI ILIKUWA SEHEMU YA MAISHA YAKE
Aldof Mbinga ambaye alifanya kazi na Semhando mwanzoni mwa albamu ya kwanza ya Twanga Pepeta ya ‘Kisa Mpemba’ na ‘Jirani’ alisema Tasnia ya muziki wa dansi imepoteza jemedari ambaye alikuwa hayumbi katika misimamo yake jambo ambalo liliiletea mafanikio Vijana Jazz akiwa Katibu na ASET akishika wadhifa kama huo.
KIDA WAZIRI "STONE LADDY ALIFANYA KAZI NA SEMHANDO VIJANA JAZZ
Wengine waliomzungumzia marehemu ni Waziri Ally ambaye ni mwanamuziki wa bendi The Kilimanjaro ‘Wana Njenje’ akimtaja Semhando kama nguzo iliyokatika ghafla wakati watu wakihitaji huduma na ukongwe wake katika muziki huku Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Dansi Nchini (CHAMUDATA), Juma Ubao, akimlilia kutokana kuwa chama hicho na medani ya muziki ilikuwa ikihitaji mchango wake wakati Ally Choki anamtaja kama mtu aliyemsaidia kumpa uzoefu wa uongozi.
ABUU SEMHANDO WA KWANZA KUTOKA KUSHOTO KWENYE MOJA YA ZIARA ZA BENDI YA TWANGA PEPETA NJE YA NCHI
Nukuu pia ilishawahi kupata ushuhuda wa Marehemu Isihaka Kibene, ambaye alisema, Twanga Pepeta imepoteza mpiganaji na mtawala mahiri kutokana na kuwa kiungo katika kufanya majukumu ya kila siku ya bendi. “Huyu jamaa ni rafiki yangu sana ambaye niliwahi kufanya naye kazi kiwanda cha uchapaji cha Printpak miaka ya 1970, na hata alipoanza shughuli za muziki tuliendelea kuwa marafiki; namna ninavyomjua utendaji wake wa kazi medani ya muziki na Twanga wamepoteza kichwa muhimu sana, kwa kuwa alikuwa anafanya shughuli za watu wengine hata kama siyo idara yake ili mradi mambo yaende sawa,” anasema Kibene ambaye ni rais wa bendi ya Walemavu ya ‘Tunaweza’.
Huyu ndiye Abuu Semhando ambaye ameacha mke na watoto 10 na kaburi lake lipo kijiji cha Kibanda Wilaya ya Muheza alipozaliwa. 
JAMES KIBOSHO MRITHI WA ABUU SEMHANDO NDANI YA TWANGA PEPETA

ANGALIA MATUKIO YA KUMBUKUMBU ZA KIFI CHA MAREHEMU ABUU ALLY SEMHANDO TAREHE 18/12/2010 

MWENYEKITI WA ASET BARAKA MSIILWA MWENYE SHATI LA DRAFT ALIFIKA ENEO LA TUKIO KUJIRIDHISHA... HAKUAMINI
GARI LILILOSABABISHA MAUTI YA ABUU SEMHANDO
PIKIPIKI ILIYOKUWA IKIENDESHWA NA MAREHEMU SEMHANDO BAADA YA AJALI
LUIZA MUTU ALISHINDWA KUJIZUIA SIKU HIYO

 


KINAMAMA WALIMLILIA SEMHANDO

VILIO VILITAWALA KILA KONA



DUA KWA SEMHANDO
CHARLES BABA HAKUWA NYUMA KUHAKIKISHA KAKA YAKE ANAPUMZIKA KWA AMANI

MZEE KITIME PIA ALIFANYA KAZI NA SEMHANDO VIJANA JAZZ



DUA KWA MAREHEMU
SAID MDOE WA SCREEN MASTERS ALIKUWEPO PIA MBUNGE IDDI AZAN
WAOMBOLEZAJI
 
REY KIGOSI NA MAREHEMU STEVEN KANUMBA PIA WALISHIRIKI MSIBA WA SEMHANDO KWA ASILIMIA MIA MOJA
MOJA KATI YA MABANGO YA KUMUENZI ABUU SEMHANDO MWAKA 2011
 
RIP ABUU ALLY SEMHANDO LOKASSA (Baba Diana, Baba Sharifa, Baba Zaituni, Baba Mwanahamisi nk)

No comments:

Post a Comment