BM BARBERSHOP KINONDONI

Tuesday, August 21, 2012

SALEH KUPAZA "SACCOS" MPISHI WA TWANGA PEPETA

SALEHE IDDI KUPAZA MWANATANGA "SACCOSS AU MASTER FILLING"
HUYU NDIYE KUPAZA
Saleh Iddi Kupaza “SACCOS” alizaliwa miaka kadhaa iliyopita Kijiji cha Manzi Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga. Jina hili la SACCOS alipewa na Mdogo wake Charles Mbwana Gabriel (Chazbaba) ambaye sasa ni Kiongozi kwenye Bendi ya Mashujaa yenye maskani yake jijini Dar es Salaam.

KUPAZA NA FASHA KAZINI
SAFARI YA KUPAZA KWENYE MUZIKI.
Mtu aliyemuingiza Kupaza kwenye Miziki ni Shimanga Kalala Asosa mwaka 1992-1993. Kupaza amekiri kumkumbuka na kumheshimu sana Mzee Assossa kwa mchango wake mkubwa alioutoa kwenye safari yake kimuziki. Baada ya kuwa na Mzee Assossa kwa mwaka huo mmoja hatimaye Kupaza alianza Safari yake kwa vipindi tofauti hadi leo kama ifuatavyo:
Mwaka 1994 alijiunga na DBR Sound ya Jijini Dar es Salaam iliyokuwa inapiga miziki yake kwenye Hotel ya Embassy Jijini Dar es Salaam. Kupaza alidumu na Bendi hii kwa mwaka mmoja.
Mwanzoni mwaka ya 1995 Kupaza alijiunga na Bendi ya Bandari Tanga na kudumu huko hadi mwaka 1995. Baadaye alichukuliwa na Less Wanyika ya Nairobi Kenya kwenye Ziara Maalum (Special Tour) chini ya Taasisi ya Povert Africa na kudumu huko hadi mwaka 2000 alipoamua kuanzisha kundi lake mwenyewe lililojulikana kwa jina la 9-GROUP lililokuwa na maskani yake Mjini Arusha na kupiga kwenye Hotel ya Mount Meru.  Mwaka 2000 Bendi yake hiyo ilikuja Dar es Salaam kwa ziara maalum ambayo walikuwa kwenye maandalizi ya kwenda Botswana kufanya Kazi huko. Walipokuwa Dar es Salaam Mkurugenzi wa ASET mama Asha Baraka aliwaalika kushiriki kwenye Bonanza la Twanga Pepeta Viwanja vya Mnazimmoja mwishoni mwa mwaka 2001. Baada ya Onyesho la Mnazimmoja Mama Asha alivutiwa na Uimbaji wangu na hatimaye kunikaribisha kwenye Bendi yake ya Twanga Pepeta mwaka 2001 rasmi.
Nilipoingia Twanga pepeta Mwaka 2001 nilifika na kuwakuta wenzangu wakiwa kwenye maandalizi ya Albam ya UKUBWA JIWE. Hapo nikakutana na Rogart Hegga, Ally Choky, Banza Stone, Luiza Mbuttu, Jesca Chalres na Marehemu Abuu Semhando. Katika albam jiyo nilitunga wimbo wa Engineer Saudia. Nyimbo ambazo nimetunga nikiwa na Bendi ya Twanga Pepeta ni pamoja na: Engineer Saudia – Albam ya Ukubwa Jiwe, Msinijadili na Mama Iffe –Albamu ya Safari 2005, Mapenzi na Pesa – Albamu ya Password, Mungu wa Maajabu-Albamu ya Mtaa wa Kwanza, Sitaki tena – Albamu ya Mwana Dar es Salaam na Mapenzi Hayana Kiapo – Albamu ya Dunia Daraja. Nasasa nakuja na wimbo Maumivu ya Wajane kwenye albamu ya Twanga Pepeta 2012.
TWANGA PEPETA SUGU
Nimetoa Mchango mkubwa kwenye Bendi ya Twanga Pepeta Kiutunzi kwakuwa asilimia kubwa huwa wanamuziki wanakuja na maneno bila melody mimi ndiye huumiza kichwa na kuingiza melody. Albamu ya Mtu Pesa ambayo ni Utunzi wa Banza wakati inaletwa na Banza Marehemu Abuu Semhando alisema kuwa ujumbe ni mzuri ila Melody aliyoleta Banza niya KIBAMBINO na KITOT siya KITWANGA. Semhando alimuambia Banza anikabidhi mashairi yake ili niyakarabati nikafanya hivyo. Muulize Banza juu ya hili atakueleza ukweli. Katika Wimbo wa Mtu Pesa Kipande change nilimpatia Igge Muyaba ili kumkuza Kimziki kwakuwa ndiyo kwanza alikuwa anaingia kwenye gemu. Kipande nilichompatia ni kile kinachosema; “Mtu na Pesa Zake yeye Pichoue Ngongo, Mutu na Pesa zake yeyee Frdedy Elima anaweza akahamisha miti milima na Mabonde, na vilevile ajue kwamba kifo hakipewi rushwa hawezi ishi milele Ras D wangu, hawezi ishi milelee baba Diana eeeh “
MRS. WEST KUPAZA
MCHANGO WA KUPAZA NDANI YA TWANGA PEPETA
Nilipokuja Twanga nilijifanya kama sijui kitu lengo langu ilikuwa kujua tabia na uwezo wa kila mmoja ndani ya Twanga Pepeta. Pia sikutaka kujinadi kwa kupiga kelele nilitaka watu wanitambue kutokana na uwezo wangu na si mbwembwe na kelele zangu. WADAU wengi wa muziki wanajiuliza ni kwa nini mwaka 2008 bendi ya African Stars ‘Wana Twanga Pepeta ‘ ambayo ina kawaida ya kutoa na kuzindua albamu mpya kila mwaka haikutoa wala kuzindua albamu katika mwaka huo.
Mengi yamekuwa yakizungumzwa huku wapenzi wengi wakidhani kuwa huenda Twanga Pepeta ilipoteza muelekeo ama wanamuziki wake waliishiwa uwezo wa kutunga nyimbo mpya. Ukweli hasa ni kwamba uongozi wa Kampuni ya African Stars Entertainment (ASET) chini ya Mkurugenzi wake mwanamama wa Shoka Asha Baraka na wanamuziki wa bendi hiyo walikuwa na kiu kubwa ya kuzindua albamu katika mwaka huo wa 2008. Lakini kiu hiyo ya uongozi wa ASET na wanamuziki wa Twanga Pepeta ilizimwa na mwanamuziki na mwimbaji mwenye uwezo wa kipekee  Saleh Iddi Kupaza  maarufu kama ‘Mwana Tanga’ SACCOS.
KUPAZA KATIKA MAISHA YA KITAA
Wakati wanamuziki hao wakiungana na Asha Baraka kutaka kutoa albamu Kupaza ambaye sasa ndiye kiongozi wa bendi hiyo akishirikiana na Luiza Mbutu alipinga wazo hilo la kutoa albamu katika mwaka huo. Ni kwa nini mwanamuziki huyo ambaye kipaji chake kiliibuliwa na mwimbaji mkongwe Shimanga Kalala Assossa mwenye uwezo wa kipekee alipinga kuzindua albamu?. Kupaza anaeleza.
“Niliamua kupinga tusitoe albamu kutokana na ukweli kuwa mwaka 2008 bendi zilizokuwa zinatamba ni FM Academia na Akudo Impact. Ilikuwa unapokwenda kwenye maonyesho ya bendi hizo unakutana na watu nyomi (wamejaa) na huku kwetu lazima tuseme ukweli kulikuwa kunaonekana wazi kuwa kumetetereka,” anasema Kupaza.  Mawazo na akili za wapenzi wa muziki kwa wakati ule yalikuwa huko. Na mimi nachojua ili uweze kufanikiwa kwanza lazima umkubali mwenzako anapofanya vizuri na wewe uiiangalia kasoro yako. Sasa mimi sikuona kama ni jambo la busara kukurupuka kutoa tu albamu na kuzindua. Tulikuwa tunataka kujimaliza wenyewe,”
TWANGA PEPETA ILEEEEE!!!!
Kwa nini walikuwa wanajimaliza wenyewe , mwanamuziki huo anasema “Kwa kuwa akili za wapenzi wa muziki kwa kipindi kile zilikuwa katika bendi hizo mbili, nilihofia kuwa kama tungefanya uzinduzi, basi kulikuwa na uwezekano wa uzinduzi kuhudhuriwa na watu wachache".“Hofu yangu ilikuwa zaidi kwa vyombo vya habari kwani kama tungepigia viti basi waandishi wangepiga picha na kutoa gazetini picha zikionyesha viti vikiwa vitupu na kutoa picha za zamani na za wakati huo na kicha cha habari kuuubwa, Ona Twanga ya zamani na ya sasa, kwisha kabisa” anasema Kupaza. “Kwa hiyo uongozi walivyoitisha kikao na kutuambia tutunge nyimbo za kujaza albamu ili tufanye uzinduzi haraka nilisimama na kuwaambia viongozi akiwemo Mkurugenzi kuwa Twanga hatuwezi kutoa albamu kwa mwaka huu. Kama mmezoea kupata pesa za uzinduzi kila mwaka andikeni maumivu. Hakuna uzinduzi mwaka huu. Unajua uongozi ulishtuka lakini walipokuja juu niliwafafanulia kwa nini nakataa. Niliwaeleza kama wanategemea pesa za uzinduzi, tutakapomaliza uzinduzi bendi itakuwa imekufa. Na kama itakuwepo ina maana haitosimama. Niliwaambia kuwa lazima ifike mahali tuukubali ukweli kuwa FM na Akudo wako juu. Kwa hiyo badala ya kung’ang’ania kutoa albamu ili tuonekane na sisi tumo, ni vyema tukaa chini na kujipanga upya namna ya kukabiliana na changamoto hiyo. Baadhi ya wanamuziki wenzangu walinielewa na kuniunga mkono hali ambayo iliufanya hata uongozi wa ASET kulazimika kukubaliana na maamuzi hayo ingawa ilikuwa kwa shingo upande. Kupaza anasema kuwa kwa kuwa uongozi ulikubali kwa shingo upande hali ilikuwa mbaya kwa wanamuziki kwani kila walipokuwa wanaeleza shida zao uongozi haukuwa tayari kutoa pesa.
MIRAJI SHAKASHIA NA KUPAZA WANATANGA
“Ilikuwa kila unapokwenda kuomba kitu unajibiwa pesa hakuna, hamjatoa albamu albamu mnadhani pesa tutatoa wapi. Lakini kwa kuwa tulikuwa tunajua tunachokifanya, hatukupaniki kwani tulijua itafika wakati uongozi utatuelewa na watatupongeza. Kwa hiyo tulielekeza nguvu zetu katika kufanya kazi anasema Kupaza. Wahenga walisema penye nia pana njia na palipo na ukweli siku zote uongo hujitenga, mwaka 2009 Twanga ilianza kuachia nyimbo moja baada ya nyingine na hatimaye kuzindua albamu ya Mwana Dar es Salaam. Pale uongozi ndipo walipoelewa kwani katika uzinduzi wetu pale Diamond Jubilee walijaa watu wengi sana. Naamini kama tungefanya hivyo mwaka 2008 watu wasingejaa vile” anasema Kupaza. Kupaza anasema kuwa albamu ya Mwana Dar es Salaam ilianza kuwafanya wapenzi wa muziki ambao walianza kuchoshwa na mambo ya Akudo na FM hasa baada ya kugundua kuwa huko hakuna jipya, walianza kuigeuzia macho tena Twanga Pepeta.
KUPAZA NA LUIZA MBUTU VIONGOZI WA BENDI
Lakini wahenga walisema mgaagaa na upwa hali wali mkavu na mchawi siku zote mpe mwana akulelee, baada ya Kupaza kuonekana adui mwaka 2008 kutokana na kushinikiza kutotoa albamu, uongozi wa Twanga umefurahishwa na shinikizo hilo ambalo limekuwa na faida kubwa na kuamua kumpa Kupaza uongozi wa bendi sambamba na mwanamama Luiza Mbutu.
MASWALI YA MWISHO KWA KUPAZA

MWANAMUZIKI GANI UNAMKUBALI NJE YA AFRICA-Jibu la Kupaza ni Papaa Wemba na Africando wa West Africa. 

NI MWANAMUZIKI GANI MKONGWE ANAYEKUKUNA- Jibu la Kupaza ni Mzee Shabani Dede.  

NI MWANAMUZIKI GANI WA KIZAZI CHA SASA ANAKUKUNA- Jibu la Kupaza ni Alfa Kabeza wa FM Accademia

UJUMBE WA JUMLA:
Nilisiliza kipindi cha Mikas cha Channel 5 kinachorushwa siku ya Jumatatu saa 3.30 Usiku na kurudiwa Jumanne Mchana saa saba. Nilimsikia ndugu yangu Ramadhan Masanja “Banza Stone” akijinadi kuwa Twanga Hakuna Mtunzi. Sasa nawaomba wapenzi wa Miziki wamuulize Banza Swali hili: Kwenye Albam ya MTU Pesa alitamka Neno Master Filling alimaanisha nini??? Pili muulizeni Mdogo wangu Charles Baba kwanini alitiita SACCOSS kwenye albamu ya Mwanadar es Salaam?.Pia ninaomba Banza alicord Verse zake zote alizoimba Twanga Pepeta nazile za nje ya Twanga Pepeta kama vile TOT, Bambino na Extra Bongo. Mkishasikiliza vipande hivyo mtanielewa. 

MWISHO KABISA-
Wanamuziki tupendane na tukubali uwezo wa waliotuzidi .

1 comment:

  1. Mjomba nakukubali sana na kazi yako haina mjadala. Wacha wabwabwanye wewe chapa mzigo tu mwanangu;

    ReplyDelete