BM BARBERSHOP KINONDONI

Monday, August 6, 2012

UJENZI WA BARABARA YA NJIA SITA KUANZIA KIMARA HADI MIKESE MOROGORO KUANZA PUNDE

Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Chato akiwa Kbaruani
WAKAZI wa Jiji la Dar es Salaam waishio kandokando ya barabara ya Morogoro wametakiwa kukaa chonjo kwani ujenzi wa barabara hiyo hadi Mkoani Morogoro utaanza hivi punde. Kufuatia upanuzi huo kuna baadhi ya mali zitakozo athirika yakiwemo Majengo mashamba na mali zote zisizohamishika. Bomoabomoa hiyo itapelekea ujenzi huo wa upanuzi (Uborshaji wa barabara kwa jumla ya kilometa 200 kutoka jijini Dar es Salaam nadi Mji unaokua kwa kasi Morogoro (Mji kasoro Bahari).

Waziri wa Ujenzi, Mh. Dk John Pombe Magufuli alisema hayo jana kwenye mahafali ya nne ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph, Kitivo cha Uhandisi na Teknolojia. Bila Kumung’unya au kung’ata maneno Mheshimiwa Magufuli alisema barabara hiyo inatarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami kwa njia sita (Three Lanes each side) kwa umbali wa kilometa 200 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro jambo ambalo limerudiwa kutamkwa na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje Bernard Membe leo 06/08/2012 Bungeni wakati akiwasilisha hotuba ya Wizara yake.

Waziri Magufuli amewatahadharisha waliojenga kwenye hifadhi ya barabara kuanza kuondoka ili kupisha upanuzi huo kabla hawajaondolewa kwa nguvu. Hifadhi ya Barabara ilikuwa ni mita 22.5 kutoka katikati ya barabara kwa pande zote kwa maana ya mita 45 kwa sheria ya zamani wakati kwasasa sheria hiyo ni mita 30 kila upande kwa maana ya mita 60 kwa sheria ya mwaka 2007 iliyopitishwa na Bunge mwaka 2009.

Namnukuu Mheshimiwa Magufuli “Wote waliojenga kwenye hifadhi ya barabara waanze kujiandaa kuondoka kwasababu sheria ni msumeno,” mwisho wa kunukuu.

Pamoja na mambo mengine mheshimiwa Magufuli alimuagiza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakandarasi, Profesa Ninatubu Lema kuwapatia usajili wanafunzi wote waliohitimu Chuoni hapo na wale wanaoendelea na masomo ili watakapokuwa wanatafuta kazi wasisumbuliwe. Kwa kauli yake Mheshimiwa Magufuli alisema “Hadi sasa kuna wahandisi 11,400 waliosajiliwa na Makandarasi 9,126” Mwisho wa Kunukuu.

RAI KUTOKA KWA MWANATANGA:
Kwakuwa sheria ni msumeno kama alivyosema Waziri nashauri wale wote waliojenga kandokando ya barabara hiyo kuanza kuchukua tahadhali mapema kwa kuwasiliana na Wataalam kutoka Wakala wa Barabara ili kujua kama wanaathirika na kupata maelezo ya kina kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kujua utaratibu wa Stahiki zao ili kuepusha Migogoro isiyo ya Lazima.
 



No comments:

Post a Comment