Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
limevitaka vyombo vya habari kuwa mstari wa mbele katika kudhibiti kazi za
Sanaa zisizo na maadili kabla ya kwenda hewani ili kuepuka mmomonyoko wa
maadili katika jamii. Wito huo umetolewa mapema wiki hii na Mkurugenzi wa Idara
ya Ukuzaji Sanaa BASATA Vivian Shalua wakati akiiahirisha programu ya Jukwaa la
Sanaa inayofanyika kila wiki kwenye Ukumbi wa BASATA ulioko Ilala Sharif Shamba
jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa, wakati Baraza limefikia
hatua nzuri ya kudhibiti hali hiyo, wadau wakuu katika kumaliza tatizo hili ni
wasanii wanaotakiwa kutunga kazi bora na zenye maadili huku vyombo vya habari
vikiwa na wajibu wa kuchuja kila kazi ya Sanaa inayopokelewa kabla ya kuirusha
hewani. “Basata imeshaviandikia vyombo vya habari kuvielekeza kuwa na kamati za
ndani za kudhibiti maadili kwenye kazi za sanaa kabla ya hazijaenda hewani.
Hili ni muhimu sana katika kujenga maadili ya mtanzania” alisisitiza Shalua.
Awali akiwasilisha mada kuhusu Historia
ya Muziki nchini na hatua zake mkongwe wa muziki wa dansi nchini John Kitime
alisema kuwa, kumekuwa na changamoto mbalimbali miongoni mwa wasanii wa fani
hiyo hali inayoufanya usifike mbali. Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa
ni pamoja na wasanii kutozingatia sheria ya hakimiliki na hakishiriki iliyopo,
kuiga midundo ya muziki kutoka nje hali inayosababisha kutokuwepo kwa muziki
wenye utambulisho wa Tanzania kama ilivyo kwa mataifa mengine ya Afrika hususan
Afrika Kusini.
“Tatizo kubwa ni wasanii wetu kuiga
miziki na hata tamaduni za kigeni, hatuwezi kuandaa kazi za Sanaa kufurahisha
wazungu au watu kutoka nje tu, tutapotea” alionya Kitime. Kwa upande wake Rais
wa Shindano la ulimbwende la Utalii (Miss Utalii) Gideon Chipungahelo alisema
kuwa, kihistoria wanamuziki wetu ukianza na wakongwe waliopo walijikita katika
kuiga miziki ya Zaire hivyo kinachofanywa na wasanii wetu wa sasa ni mwendelezo
tu. “Ni wazi kazi iliyopo sasa ni kuwafanya wasanii kujikita katika utajiri
mwingi wa makabila yenye midundo mbalimbali tuliojaaliwa. Hapa ndipo tunapaswa
kusisitiza” alishauri Chipungajelo. Mzee Kassim Mapili aliwaeleza vijana hali
ya tasnia ya muziki ilivyokuwa huko nyuma na mabadiliko yaliyopo sasa.
No comments:
Post a Comment