Leo ningependa kuzungumzia hatua ya Kampuni ya
Aset ya jijini Dar es Salaam chini ya mwanamama Asha Baraka ‘Iron Lady’ kuamua
kuandaa onyesho maalumu la kukusanya fedha kwa ajili ya kuchangia matibabu ya
gwiji la muziki wa dansi nchini, Muhidin Maalim Gurumo, maarufu kwa majina ya
‘Mzee wa Masaki’ au ‘Uncle Gurumo’ ambaye kwa miezi kadhaa amekuwa akisumbuliwa
na ugonjwa wa mapafu kujaa maji ambapo alilazimika kulazwa katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili na kufanyiwa operesheni lakini bado hali yake kiafya
haijakaa vema.
Katika onyesho hilo ambalo lilifanyika katika
Ukumbi wa Mango Garden, Aset iliandaa onyesho hilo ambalo liliishirikisha bendi
kongwe ya muziki wa dansi nchini ya Msondo Ngoma ambayo kiongozi wake ni Uncle
Gurumo japo kwa sasa amejiweka kando katika kuitumikia bendi hiyo kutokana na
maradhi yanayomkabili.
Jamvi la Kulonga likiwa mmoja wa wadau wakubwa wa
muziki nchini limeguswa na hatua ya Aset kuona umuhimu wa kuchangia matibabu ya
mzee huyo ambaye ameweka rekodi ya kudumu katika uimbaji kwa muda mrefu lakini
kubwa zaidi akiwa na sauti ileile iliyojaa ubora ambayo alianza nayo tangu mwaka
1950.
Katika maelezo yake kwa Jamvi hili, Asha, anasema
onyesho hilo lililenga kutunisha mfuko wa matibabu ya gwiji huyo, ambaye ametoa
mchango mkubwa katika mafanikio ya muziki wa dansi, hivyo kuona umuhimu wa
kumsaidia aweze kupona kwa sababu wanamuziki wengi hawana kipato cha kutosha
lakini pia hawana pensheni baada ya kustaafu.
Katika onyesho hilo wadau waliweza kuchangia
zaidi ya shilingi milioni 2 taslimu, mbali ya fedha zilizopatikana kutokana na
viingilio vya waliohudhuria ambazo kwa mujibu wa Asha atakabidhiwa Gurumo ili
ziweze kumsaidia katika kujitibu maradhi yanayomkabili ili aweze kurudi katika
hali yake njema kiafya.
Mzee huyo aliwapagawisha mashabiki katika onyesho
hilo pale alipopanda jukwaani kuwasalimia na kuamua kuimba wimbo mmoja ambapo
kila aliyemsikia akiimba wimbo wa ‘Piga Ua Talaka Utatoa’ alishindwa kujizuia
kukaa na kujikuta akimtunza Gurumo.
Nikirudi katika hoja ya msingi ni kwamba kitendo
kilichofanywa na Aset kimelisukuma Jamvi hili kumpongeza Asha Baraka kwa uamuzi
wa kampuni yake kuonyesha kujali afya ya Gurumo, jambo ambalo linapaswa kuigwa
na bendi nyingine katika kusaidiana wanamuziki na kushauri kuwa isiishie katika
maradhi pekee, kwani yako matatizo mengi yanayowakabili wanamuziki na yakiwa
yameshindwa kupatiwa ufumbuzi.
Unapouzungumzia muziki wa dansi nchini wa enzi na
enzi ni lazima utaje jina lake kutokana na kushiriki kuanzisha bendi mbalimbali
za muziki huo tangu mwaka 1961 ambapo alishiriki kuimba nyimbo mbalimbali za
kuhamasisha masuala mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Jamvi hili
linakumbuka mchango wa Gurumo katika kushiriki kuasisi bendi kongwe ya muziki
wa dansi ya NUTTA Jazz ambayo bado yupo nayo hadi leo ikiwa imepitia majina
mbalimbali ya JUWATA Jazz, OTTU Jazz na sasa ikiitwa Msondo Ngoma Music.
Miongoni mwa wanamuziki wakongwe ambao wameuletea
mafaniko muziki wa dansi nchini ni Gurumo, ambaye mpaka sasa anajivunia kuona
bendi zote alizoshiriki kuzianzisha zimeendelea kuwepo katika medani ya muziki
tena kwa mafanikio lakini na yeye akiwa bado ana uwezo wa kuimba. Ni mmoja wa wanamuziki walioshiriki
kuanzisha NUTTA Jazz ambayo kwa sasa inaitwa Msondo Ngoma mwanzoni mwa miaka ya
1964, lakini pia akiwa ni mwanzilishi wa DDC Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde
Ngoma ya Ukae’ iliyoasisiwa 1978 akiwa na wapiga solo Abel Baltazar na Joseph
Mulenga na nguli Hassan Rehani Bitchuka na wengineo.
Tungo zake alizowahi kutunga na anazoendelea
kutunga akiwa na Msondo Ngoma ni dhahiri zimeendelea kutesa na kumuongezea
heshima kutokana ujumbe uliomo katika kuielimisha jamii na kusaidia wakati huo
katika harakati za mapambano ya kupigania uhuru kwa nchi ya Msumbiji ambapo
aliweza kutunga wimbo wa ‘Viva Flerimo’. Kuugua kwake ni pengo kubwa kwa wadau
wa muziki huo kwani damu changa zilizopo Msondo Ngoma zinahitaji kurithishwa
mikoba ya kujua maadili ya muziki na thamani ya mwanamuziki katika kutunga na
kuimba ili nyota yake izidi kung’ara.
Gurumo ni mwanamuziki mtunzi, mwimbaji mkongwe na
mbunifu wa mitindo mbalimbali ya dansi kama vile ‘Msondo Ngoma’, ‘Sikinde Ngoma
ya Ukae’ (alipokuwa Mlimani Park) na Ndekule (alipohamia kwa muda Orchestra
Safari Sound Wana OSS) akiwa na Hassan Rehani Bitchuka na Skasy Kasambula.
Lakini sifa na heshima kubwa aliyonayo Uncle Gurumo ni kushiriki kuasisi bendi
hizo pamoja na mtindo ambapo akiwa na NUTTA Jazz ndiye aliyeanzisha mtindo wa
‘Msondo Ngoma’ na alipokwenda kuiasisi DDC Mlimani Park aliasisi mtindo wa
‘Sikinde Ngoma ya Ukae’, ambayo imeendelea kutumiwa na bendi hizo hadi leo.
Akiwa na bendi hiyo ya Nuta Jazz, Gurumo alitunga
nyimbo nyingi ambazo ni ‘Magdalena’, ‘Maneno ya Mwalimu’, ‘Maneno ya Wazee Yote
Sawa’, ‘Rehema Umefeli Shule kwa Kisa Gani’? na nyinginezo. Baadaye bendi hiyo
ilibadilishwa jina na kuitwa Jumuiya ya Wafanyakazi, JUWATA, ambapo akiwa na
bendi hiyo baadhi ya vibao alivyotunga ni ‘Dada Fatuma’, ‘Dada Sabina’ kabla
haijabadilishwa na kuwa OTTU Jazz Band ambapo moja ya nyimbo alizotunga na
kumpatia umaarufu ni ‘Usia wa Baba’ lakini akiwa alitunga ‘Majuto’. Jamvi la
Kulonga linatambua na kumheshimu mzee huyu kutokana na ubora wa sauti aliyonayo
ileile tangu enzi za NUTTA lakini nilipowahi kuumuliza siri ya mafanikio
alibainisha kuwa ni kutojihusisha kwake na ulevi na anasa zingine za dunia,
vitu ambavyo ni sumu kwa mwanamuziki.
Mwanamuziki huyo alizaliwa Masaki, Kisarawe mwaka
1940 na kupata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Sungwi huko huko
Kisarawe, na baadaye aliacha shule baada ya baba yeke kufariki dunia na kukosa
mtu wa kumgharamia mahitaji ya shule. Baada ya kuacha shule kutokana na kufiwa
na baba yake, Gurumo mwaka huo huo alijiunga na bendi ya mtaani iliyojulikana
kama Scock Jazz iliyokuwa na maskani yake katika mitaa ya Moshi na Kigoma.
Mwaka mmoja baadaye alijiunga na bendi ambayo
ilikuwa na vyombo vya kisasa wakati huo, iliyojulikana kama Kilimanjaro Chacha,
ambako alitunga vibao kama vile ‘Twende Tukalime’, ‘Mapenzi Hayana Dawa’,
‘Ushirikina ni Sumu ya Maendeleo’. Mwaka 1963 Gurumo alijiunga na Rufiji Jazz
Band, ambako alitunga kibao cha ‘Uwezo wa Binadamu Kufikiri’, ambacho
kilimpatia umaarufu mkubwa kufuatia kupendwa na wapenzi wengi wa muziki wa
dansi. Baadaye mwaka huo huo alijiunga na bendi ya Kilwa Jazz na kutunga kibao
cha ‘Wewe Mpenzi Naomba Unishauri Kabla Hatujagombana’, na kile cha ‘Siwezi
Kukununulia Gari Wakati Hata Baiskeli Sina’.Mwaka 1964 alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa
bendi ya Nuta Jazz, akiwa na kina Mabruki Khalfan, Ahmed Omary, Mohamed Omary,
Epimakus Mkundika na Rashid Abdallah. Jamvi la Kulonga linamuombea kwa Mwenyezi
Mungu ‘Uncle’ Gurumo aweze kupona kwa haraka na kurejea jukwaani japo
ameshafanya uamuzi wa kustaafu lakini bado wadau tunahitaji kusikia ladha ya
sauti yake, kuendelea kuwaburudisha wapenzi na mashabiki wa bendi ya Msondo
Ngoma na wadau wa muziki wa dansi.
No comments:
Post a Comment