Hebu jaribu kupata picha, umelima shamba lako na kupanda mahindi ambayo
umeyatunza vizuri na yako tayari kuvuna….. Unaamka siku moja na kukuta kuna mtu
kayavuna na ameanzisha biashara anapata fedha nzuri wewe huna hata fedha ya
kula. Au umenunua suti nzuri akaja mtu akaivaa harusini, kesho yake anakuja
kukutaarifu jinsi walivyomsifia harusini. Hiyo ndio picha ilivyo katika shughuli
za Sanaa Tanzania. Na haswa katika mambo ya Muziki na Filamu.
Wasanii hufanya kazi ngumu ya kutunga na kufanya mazoezi kisha kurekodi
kazi zao, kabla hawajafaidi kazi zao hukuta shamba lao likiwa linavunwa kwa
njia mbalimbali. Wengine hudurufu kazi zao, wengine huzitumia kutangaza
biashara zao, wengine huzitumia kuhamasisha mikutano yao, wengine huziuza kwa
kuwarekodia watu katika simu, katika yote haya mwenye shamba haoni mafao
yoyote. Kutokana na matumizi mengi ambayo yanaweza kutokana na kazi zilizotungwa
kutokana na ugumu wa kudhibiti kazi hizi sheria zinaitwa za Hakimiliki hutumika
katika kulinda maslahi ya mtunzi kwa upande mmoja na mtumiaji kwa upande
mwingine.
Ulinzi wa hakimiliki umekuwa mgumu sana hapa nchini kwetu hasa kutokana
na kuweko kwa utamaduni wa kutokuheshimu ubunifu wala sheria zinazolinda haki
za ubunifu.
Labda nitoe mfano, leo ukianzisha kibanda cha chips chenye mapambo
tofauti na vingine, muda mfupi baadae mtaa mzima utajaa vibanda vinavyofanana
na chako. Watu hawaoni shida kunakili ubunifu. Fundi seremala akibuni staili
fulani ya makochi baada ya muda mfupi maseremala kila mahali wataiga staili
hiyo ya makochi bila hata kuwaza kuwa wanaiba ubunifu. Katika maeneo yote ya karibu ya vyuo na sehemu za elimu ya juu utakuta
biashara kubwa ya mashine za fotokopi, kazi ya mashine hizi ni kurudufu
maandiko na vitabu mbalimbali vya watu bila kujali kuwa waliotunga vitabu hivyo
wanahitaji viuzwe ili wapate mafao yao.
Kwa masaa ishirini na nne kila siku redio na baadhi ya Tv hurusha hewani
nyimbo za watu, tena kwa vipindi ambavyo hutangazwa wazi kuwa vimedhaminiwa na
kampuni kubwa mbalimbali zenye kuheshimika. Vituo hivi vinamilikiwa na
kuendeshwa na watu wanaoheshimika katika jamii kwa kuhamasisha vijana
wajiajiri, lakini ikishafika kwenye eneo la kulipia matumizi ya kazi za wasanii
kigugumizi kikubwa kinatokea. Watetezi wa haki mbalimbali za wananchi wa Tanzania, watatetea kila
haki lakini wakati wa kampeni zao watatumia kazi za wasanii na kuwa wagumu
kulipia matumizi hayo. Wanasiasa wakiwa katika kampeni za kuwaeleza wananchi ni
jinsi gani wakipata madaraka watatetea haki zao hutumia kazi nyingi za sanaa
bila kuzilipia na wala hawaoni kuwa tayari kuna wananchi wanawanyanyasa kwa
kutumia kazi zao bila kulipia.
Sheria za hakimiliki humpa mtunzi haki zifuatazo katika tungo zake;
(a) Kurudufu
kazi
(b) Kusambaza
kazi
(c) Kukodisha
kazi
(d) Kutafsiri
kazi
(e) Kubadili
matum izi ya kazi
(f) Kuonyesha
kazi hadharani-exhibition
(g) Kuifanya
kazi hadharani-public performance
(h) Kutangaza
kazi katika vyombo vya habari-broadcasting
(i) Kuwasilisha
kazi kwa umma kwa njia yoyote
(j) Kuingiza
kazi nchini
Mtunzi anaweza akaingia katika makubalianao na
mtu mwingine ili kutumia moja au zaidi ya haki hizo ili kupata mafao yake. Nadhani
ukiangalia haki hizo hapo juu utaweza kuona jinsi haki za watunzi
zinavyovyunjwa masaa ishirini na nne.
Ununuapo CD
au DVD elewa kuwa umeipata kwa ajili ya matumizi yako binafsi, ukianza kuitumia
kwa shughuli yoyote ile nyingine unaanza kuingilia haki zilizotajwa hapo juu.
Hivyo basi kununua CD hakukupi haki ya kuanza kutoa nakala za CD hiyo, wala
kuanza kuirusha redioni au kuipiga hadharani kwenye baa au hoteli, hapana,
utahitaji kupata ruksa kuanza kutumia kwa kazi hizo za ziada. Ruksa hizi hupatikana
kwenye Chama kinachoshughulika na mambo ya Hakimiliki Tanzania yaani COSOTA.
COSOTA hutoa
leseni ambazo watumiaji wa kazi za muziki huzilipia na fedha zinazopatikana
hugawiwa watunzi. Katika nchi ambazo taratibu hizi zinafanya kazi wanamuziki na
wadau wengine wa muziki hupata fedha nyingi kutokana na matumizi ya kazi zao.
Bado kuna tatizo kubwa la hili kwani kama nilivyosema utamaduni wa kudharau
haki za watunzi bado ni mkubwa katika jamii ya Tanzania.
Jambo la
kufurahisha ni kuwa tayari kuna wafanya biashara kutoka sehemu mbalimbali
nnchini ambao wamekuwa wanalipia kwa matumizi ya kazi za muziki na COSOTA
wamekwisha gawa fedha kwa mara ya saba kwa watunzi wa kazi mbalimbali.
Ili kupata
watunzi bora na kazi bora za muziki ni muhimu kuhakikisha watunzi wanalindiwa
haki zao na kila mpenda sanaa.
No comments:
Post a Comment