SAKATA
la makada wa CCM, Hussein Bashe na Dk Hamis Kigwangala kutoleana bastola,
limechukua sura mpya baada ya Jeshi la Polisi kuingilia kati na kumnyang’anya
bastola Kigwangala huku likianza kuwahoji wapambe wa mahasimu hao.
Habari
zilizopatikana jana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, (RPC)
Antony Lutta zilieleza kuwa jeshi hilo linaishikilia silaha ya Dk Kigwangala
hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.
Kauli
hiyo ya Polisi imekuja siku moja baada ya uongozi wa chama hicho Wilaya
ya Nzega, kutaka suala hilo liondolewe Polisi ili walishughulikie kimyakimya
ndani ya chama.
Dk
Kigwangala ambaye pia ni Mbunge wa Nzega amekanusha na kusema kuwa bastola
yangu mbona ninayo, hilo halina ukweli, bastola ninayo hapa.”
Wakati
hayo yakiendelea, uongozi wa CCM wilayani humo umempa onyo kali Dk Kigwangala
ukieleza kwamba endapo ataendeleza msimamo wake wa kukataa kuhojiwa na chama,
atachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kunyang’anywa kadi ya uanachama.
KAULI YA KUJIUZULU UBUNGE
KWA DR. KIGWANGALA
Hata
hivyo, mbunge huyo alisema kuwa hana imani na uongozi wa CCM wilayani Nzega na
kwamba iwapo CCM mkoa na taifa hautaingilia kati mgogoro huo, yuko tayari
kujiuzulu ubunge.
Bashe
na Dk Kigwangala ambao ni mahasimu wa siku nyingi katika medani za siasa
wilayani Nzega walidaiwa kutoleana bastola Alhamisi iliyopita walipogongana
katika ofisi za CCM wilayani humo, wakati wakirejesha fomu za kuwania
Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kupitia wilaya hiyo.
Hata
hivyo, pamoja na taarifa hizo kuthibitishwa na viongozi wa CCM wilayani humo na
RPC Lutta, kila mmoja alikanusha madai hayo akimtuhumu mwingine kuwa ndiye
chanzo cha ugomvi huo.
Wakati
Bashe alisema Dk Kigwangala ndiye aliyetoa bastola kumtishia wakiwa ndani
ya Ofisi ya CCM Wilaya, Dk Kigwangala alieleza kuwa Walinzi wa Bashe ndio waliomtishia
yeye bastola na kwamba tayari amelifikisha suala hilo Polisi na wanalifanyia
kazi.
KAULI YA KAMANDA
LUTTA
Kamanda
Lutta alisema ingawa imemnyang’anya bastola Dk Kigwangala, mbunge huyo
anamiliki silaha hiyo kihalali.
“Taarifa
zao tutazitoa baadaye kwa sababu hivi sasa tunakusanya ushahidi na
tunawahoji wapambe wao, ambao inasemekana wakati tukio linatokea walikuwepo
eneo hilo,” alisema Lutta na kuongeza:
“Silaha
yake ipo katika Kituo cha Polisi Nzega, uchunguzi tulioufanya unaonyesha kuwa
ni yake na anaimiliki kihalali. Ni kweli ndugu yangu silaha yake
tunaishikilia.” Alisema kuwa kazi ya polisi ni kuchunguza tukio zima na
ikikamilisha uchunguzi wake, itaupeleka katika mamkala husika.
CCM WATOA TAMKO ZITO
Mwenyekiti
wa CCM Wilaya ya Nzega, Francis Shija alisema tangu kutokea kwa tukio hilo, Dk
Kigwangala alikataa kutoa maelezo katika kikao cha dharura cha Kamati ya Siasa
Wilaya kilichofanyika juzi na kile cha Kamati ya Maadili kilichofanyika jana.
Alisema
vikao bado vinaendelea ili kubaini ukweli wa tukio hilo na kuongeza kuwa
uongozi wa chama utahakikisha haki inatendeka kwa watuhumiwa hao, ili kila
mmoja apewe adhabu yake pamoja na onyo kali, kama wanastahili.
“Vikao
vitaendelea ili kubaini ukweli na mtu atakayekaidi kutoa ushirikiano hatua
zitachukuliwa dhidi yake ili iwe fundisho kwa wengine,” alisema Shija na
kuongeza:
“Kama
Kigwangala ataendelea kukaidi kila tutakapomwita ili aeleze kilichotokea
tutamnyang’anya kadi ya uanachama, ila sidhani kama itafika huko, tutajitahidi
tuyamalize kistaarabu.”
Alipoulizwa
kuwa taarifa zilizopo kuwa uongozi wa CCM wilaya hiyo unampendelea Bashe
alisema: “Siyo kweli, hatuegemei upande wowote katika suala hili. Kamati ya
Maadili haijaegemea kwa Bashe tutahakikisha haki inatendeka na chama hiki
hakina makundi kila mtu anavuna alichopanda.”
KAULI YA DR. KIGWANGALA
Kwa
upande wake Kigwangala alisema kuwa kikao cha Kamati ya Siasa kilivunjika jana
kwa sababu hakuwa na imani na wajumbe waliokuwa wakiendesha kikao hicho.
Aliwataja
wajumbe wa kikao hicho ambao hana imani nao kuwa ni pamoja na Shija na Katibu
wa chama hicho Wilaya ya Nzega, Kajoro Vyohoroka.
Alisema
hata kikao cha maadili ambacho kilifanyika baada ya kuvunjika kwa kikao cha
Kamati ya Siasa, nacho kina watu ambao hana imani nao.
‘’Siwezi
kutoa hoja zangu za msingi kwa kamati hii ya maadili, kwani hakuna
kilichobadilika kwa sababu wanaokisimamia ni Shija na Vyohoroka na wote wapo
upande wa Bashe. Siwezi kukubali kuhojiwa hadi jambo hili litakapopelekwa katika
ngazi nyingine ndani ya chama,” alisema Kigwangala.
Alisema
siasa za CCM Wilaya ya Nzega ni ‘siasa uchwara’ kwa kile alichoeleza kuwa ni
kuwapo kwa makundi yasiyo na msingi wala faida kwa CCM na kusisitiza kuwa kama
jambo hilo halitafanyiwa kazi yupo tayari kujiuzulu ili kumwacha Bashe
aendeleze siasa uchwara.
“Endapo
tatizo hili halitaingiliwa kati na CCM ngazi ya mkoa na taifa, nipo tayari
kujiuzulu ubunge na kukabidhi,” alisema Kigwangala.
”Mimi
silaha ninayo siku nyingi tu na hata mara moja sijawahi kumtishia mtu maisha,
kama unataka kuiona ipo siku nitakuonyesha,” alisema Kigwangala akimwambia
mwandishi wa habari hizi.
No comments:
Post a Comment