Hii ni kwamujibu wa Bwana Ruyembe ambaye kwa sasa
ni kiongozi pale Baraza la Sanaa la Taifa
“Jerry alikulia Musoma Mjini eneo la Kigera ndani
ya Halmashauri ya Manispaa ya Musoma jirani na shule ya Sekondari Mara.
Nilikutana naye mara ya kwanza akiwa Musoma Catholic Mission club ambayo leo ni
Mwembeni Secondary School akiwa anajifunza kupiga gitaa. Alikuwa ana mazoea ya
kwenda kwenye hiyo social club ya kanisa iliyowaunganisha vijana wanamichezo
mbalimbali.
Nilimchukua katika Bendi yangu niliyokuwa nimeiunda
muda huo 1980s ikiitwa Special Baruti Band. Nilimuunganisha na Mpiga rhythm
wangu aliyeitwa Charles Koya ambaye hivi sasa anapiga na Bendi ya Mwanza Hotel
(solo guitar), ili amwendeleze na akiwa pia mwana Bendi wetu. Alikuwa
mwanafunzi mzuri alikuwa na bidii na akaweza baada ya muda mfupi kupiga
programu yetu kubwa! Mimi nilikuwa mtunzi na mwimbaji licha ya kumiliki Bendi
hiyo.
Tulirekodi naye mara ya kwanza TFC pia RTD na
baadaye tulirekodi Kenya katika studios mbalimbali na producers mbalimbali na
tumepiga muziki clubs mbalimbali Nairobi ikiwa kama vile Bombax Hotel, Kaka
Night Club, Rwadhia Night Club na nje ya Jiji katika mikoa takribani yote ya
Kenya kasoro Mombasa na Kisumu! Hapa tulishirikiana na mwanamuziki hodari
Joseph Kamaru. Muda huo yeye akipiga gitaa la rythm na Bendi yetu wakisaidiana
na Koya.
Jerry alivutiwa na uimbaji pia utunzi baada ya
kuona nafasi niliyokuwa nayo na umaarufu nilioupata enzi hizo Nairobi.
Alijifunza nikampa mwanga na kipaji chake kikajitokeza katika kuimba na utunzi
pia!.Hatimaye Jeshi la Magereza Musoma walimchukua kwa nia ya kumleta Dar
ajiunge na Bendi yao ya Magereza. Alipitia mafunzo na aliondoka baada ya kuwa
na Special Baruti kwa miaka miwili na nusu hivi au mitatu. Muda huo Musoma
kulikuwa na Musoma Jazz Band(segese) ambayo mimi na wanamuziki wengi wa Special
Baruti tulipigia baadaye tukahama na kuiacha hali mbaya! Ilikuwepo pia Mara
Jazz Band(Sensera) hizi ndizo zilikuwa Band maarufu mjini hapo wakati huo.
Aidha ilikuwapo bendi iliyomilikiwa na Parokia ya Catholic Mission Makoko
Seminary ikiitwa Juja Jazz Band lakini ilikuwa ndogo sana na haikuwa kwa
misingi ya kibiashara zaidi!. Jerry Baadae alijiunga na Bima Orchestra na kisha
Vijana Jazz mpaka mauti ilipomkuta Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi
Amina” Mwisho wa maelezo yake.
No comments:
Post a Comment